Maisha ya uswahilini yalivyomtoa Zai Kijiwe Nongwa

Muktasari:

  • Wakati akizungumza na Mwananchi, Zai amesema kabla ya kufahamika alikuwa anapenda kuhadithiana stori na wenzake  wanacheka kwa furaha.

Vinapotajwa visa, mikasa na vioja vya uswahilini ni ngumu kuzisahau simulizi za mchekeshaji Zainabu Ally maarufu kama Zai Kijiwe Nongwa, mkazi wa Vingunguti Machinjioni, mtaa wa Butiama jijini Dar es Salaam.

Wakati akizungumza na Mwananchi, Zai amesema kabla ya kufahamika alikuwa anapenda kuhadithiana stori na wenzake  wanacheka kwa furaha.

Ikitokea mmoja kapata mitihani ya mume au mke, amepigika, mazingira yake magumu wanakutana kwenye kijiwe chao wanazungumza mawili matatu maisha yanaendelea.

                       

Hata hivyo, safari yake ya kupata umaarufu ilianza baada ya watangazaji wa Clouds ambao walikuwa wakifuatilia tukio lililotokea mtaani kwao, lililomhusu dada aliyefahamika kwa jina la Mwanahamisi. Hivyo wakamripoti ili atangazwe redioni apate uhamisho wa makazi ili wakazi wa eneo hilo waishi kwa amani.

“Kwa hiyo tulivyofikisha ile stori badala ya huzuni watu wakaipokea kwa vicheko kutokana na nilivyoihadithia, basi ndipo kazi yangu ilipoanzia.

“Nilipoanza kazi yangu sikuona ugumu wowote, nilichukulia kawaida tu kwamba ninaongea watu wanacheka maisha yanaendelea.”

“Nilivyokuwa naongea watu wanacheka naona furaha, nachukua matukio nayaleta hewani watu wanafurahi,” anasema.

Kutokana na vitu ambavyo huwa anaviongea kuwa na uhalisia wa maisha ya baadhi ya watu, anasema taarifa anazotengenezea maudhui anazipata kutoka kwa watu mbalimbali.

“Taarifa zangu ninapata kutoka kwa watu kutokana na stori za huu mji, maana umechachuka, kuna wakati unakaa kimya kuna wakati ambao watu wanachanganyika. Huu mji una makabila mengi, una wagogo, wakurya, wasambaa, una warangi, yaani kila aina ya kabila linapatikana Tanzania mchanganyiko wake uko hapa.

“Kwa hiyo kila kabila likitoa kituko chake kunakuwa na vionjo tofauti tofauti, zile tabia nilizokuwa naziona huku nilikuwa naona kwa nini watu hawazijui, kuna watu sasa hivi wanaishi maisha ya juu, wengine wako nje, kuna tabia ambazo nikiziongelea wengine wanazikumbuka kuwa haa! hii tabia hii hata mtaani kwangu ilikuwepo, kwa hiyo wanakuwa wanafurahi.

“Kuna mwingine hajui yaani ndiyo kwanza anashangaa huu mji gani una matukio haya, kwa hiyo watu wakawa wanapenda wanataka niwaeleze matukio yanayotokea huku uswahilini.
“Kadri ninavyozidi kuna wengine wakawa wananiambia mimi labda huku Chanika kuna tukio hili, lakini huwa ninajumlisha matukio yote kwa pamoja,”anasema.

Kwa nini Kijiwe Nongwa?

Eneo ambalo Zai hulitumia kutengenezea maudhui yake na anapoishi pamepewa jina la Kijiwe Nongwa ambalo pia jina hilo ndilo limebeba umaarufu wake.

“Eneo hili liliitwa jina hilo kutokana na tabia tulizonazo, tabia zetu kwanza hatupendi kuambiana ukweli. Mfano mtoto akiharibika unaweza kumwambia mzazi kuwa mtoto kaharibika, kwa nia njema kabisa lakini kumbe hujui pale umeshatengeneza tatizo, watu wanaanza kusema huyu anaona watoto wa wenzie ndiyo wabaya, lele lele…

“Yaani neno umelipeleka kwa wema lakini linakubadilikia na unakuwa wewe ndiye mbaya, kwa nini umempelekea habari, wewe mnafiki, yaani kunakuwa na nongwa ambazo hazina maana,” anasema.     

Mbali hilo pia amesema wanatabia ya kusemana endapo mtu akishindwa kutimiza ahadi alizoweka.

“Lakini pia kuna suala la ahadi huku kwetu, ukisema nitakutumia kitu fulani kesho, ukikosa tu, hata kama ulikuwa unatuma siku zilizopita zile zote zinafutwa, unaambiwa wewe ndivyo ulivyo. Wema wote unafutwa, ndiyo maana watu wakasema hiki Kijiwe Nongwa, yaani nyie mnanongwaaa.

“Kwa hiyo tukapewa Nongwa na sisi tukaona kwanini tusiite kijiwe, kwa hiyo ile Nongwa tuliyopewa tukamalizia Kijiwe Nongwa,” anasema.


Uhusiano

Anasema kutokana na kipaji chake cha kuongea na kuchekesha kilisababisha aachane na mume wake wa kwanza kwani alikuwa hapendi anachofanya.

“Kwa mara ya kwanza mahusiano yalikuwa magumu kwa sababu ya mume wangu, ilikuwa ugomvi ananiambia mara hivi mimi sitaki, unajua kila mtu katika maisha ana fomula yake alivyoipanga, mimi napenda maisha yangu yawe hivi, kwa hiyo mwanaume wangu wa kwanza alikuwa hapendi, yaani familia yangu itakuelewaje,  mimi nikamwambia kama hawezi kunielewa basii, mimi siwezi kuacha kipaji changu.

“Kwa hiyo nashukuru, kwa huyu niliyempata ananielewa, na ninapogombana naye mimi ninakaa pale katikati ya uwanja ninachamba mpaka mjumbe anauliza huyo anayechambwa mwanamke mwanaume? Maana ninamaliza maneno yote, lakini hapo anakuwa amenikera, nimevumilia nimeshindwa,” anasema.


Safari ya uigizaji

“Safari yangu ya uigizaji kwa mara kwanza nilijiona siwezi, ila kuna siku nikiwa Kariakoo kuna kaka anaitwa Isike aliniita akaniambia anataka afanye kazi na mimi. Tamthilia yangu ya kwanza ilikuwa Pazia, nilipofika tu kila mtu akanipokea kwa furaha, wakanielekeza namna ya kufanya.

“Mara ya pili nikaonekana kwenye tamthilia ya Dhohar, ambapo waliniambia wanataka waniweke kwenye mtu smati, nitoke kwenye ule ukijiwe nongwa wa uswahilini, kweli nikafanya vizuri.
“Nikaja kwenye tamthilia ya Siri na nimekuwa nikiomba kila ninachofanya kizidi kuwa kikubwa na bahati nzuri kila nikifanya huwa sikosei na nikisoma ‘skripti’ tu nanyoosha,” anasema msanii huyo.


Changamoto za umaarufu

Zai anasema kwa sasa anakutana na changamoto za kushangawa na watu na kuzidishiwa bei za bidhaa kutokana na kufahamika kwake kwani waliowengi wanadhani yeye ni tajiri.

“Changamoto ni umaarufu, zamani nilikuwa naweza kwenda Kariakoo nafanya shoping zangu wala sishobokewi na mtu, sasa hivi unaweza kwenda kwenye duka mtu anamwambia mteja nguo Sh20,000, lakini akishaona tu uso wa Kijiwe Nongwa unashangaa anaweza kubadilisha bei na kukwambia Sh40,000, kwa hiyo nikagundua kumbe ukiwa maarufu hata bei ya kuuziwa bidhaa inabadilika.

“Suala jingine ni watu kutaka kupiga picha kila unapopita, au ukiwa kwenye daladala unakosa uhuru, kila mtu anakushangaa na wengine wanakuuliza maswali ya hapa na pale,” anasema Zai.

Mbali na changamoto hizo anazokutana nazo kwa mashabiki pia amesema kuna watu walikuwa wakimuona kama kachanganyikiwa

“Nilipoanza kufanya kazi yangu hii kuna watu walikuwa wakiniona kama mwehu, chizi, wengine wanaona kama siwezi kuwa na siri, kwa hiyo nikaona kumbe hawa wananichukulia mimi kama sieleweki, kwa hiyo ikabidi niwe nawaeleza kuwa hii ni kazi.”

Maisha ya kijiwe nongwa

“Huku Kijiwe Nongwa kwanza unatakiwa uwe mwaminifu, unaweza kukopa chakula kutwa nzima ukala na ukipata ulipe.

“Kuna pombe ya viswanta, ambayo inauzwa Sh200, huku wakishaamka asubuhi, wengi kazi zao ni machinjioni wanafanya kazi usiku asubuhi wanalala,” anasema msanii huyo huku akitupa mikono.

Mara ya kwanza walikuwa wanatumia akina baba lakini sasa hivi hadi akina mama na wasichana wanatumia.

“Mtu akienda zake gengeni ananunua vichupa vitatu Sh600 wakati anapika mboga yake anakunywa viswanta taratibuu, msingi hamira na majani ya chai.

“Ile pombe ukinywa, ukikaa kama nusu saa ukitaka kuongea na mtu ukae mbali, maana ile inakwenda kuvunda mdomoni anamalizia na kucheka.