Matumaini Tanesco kufanya biashara ya umeme Afrika

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Abubakar Issa akizungumza hii leo Mei 13, 2024 wakati wa mkutano wa wakuu wa sekta ya nishati kutoka nchi 13 Afrika wakijadili sheria na miongozo ya biashara ya umeme.

Muktasari:

  • Vigogo sekta ya umeme kutoka nchi 13 Afrika wamekutana hii leo Jijini Dar es Salaam kupanga mikakati ya  biashara ya umeme Afrika.

Dar es Salaam. Ile ndoto ya kufanya biashara ya kuuza na kununua umeme pamoja na kuwa na gridi moja ya bara la Afrika iko mbioni kutimia, baada ya wakuu sekta ya nishati kutoka nchi 13 Afrika kukutana kupanga mikakati ya biashara hiyo jijini Dar es Salaam.

Mikakati iliyojadiliwa leo Jumatatu, Mei 13, 2024 ni pamoja na kanuni, sheria na miongozo ya kibiashara katika nchi za Afrika zilizopo kwenye Jumuiya ya nishati ya nchi zinazoungana kimiundombinu ya umeme.

Nchi zilizokutana ni pamoja na mwenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Misri, Ethiopia, Libya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Sudan, Djibouti, Somalia pamoja na Congo DRC kwa pamoja zinajadili namna ya kufanya biashara hiyo ya kuuza na kununua umeme.

Katika biashara hiyo Tanzania itafanya kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambapo faida itakayoipata ni kuuza na kununua umeme pamoja na kupata pesa pale umeme utakapopitishwa kwenye miundombinu ya shirika hilo.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Abubakar Issa amesema Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Nishati (EAPP), ambazo lengo lake ni kusaidiana kupata umeme wa uhakika katika nchi hizo.

"Hii itakuza uchumi wa Tanzania pamoja na bara letu kwa ujumla kwa kuwa umeme ni uchumi," amesema Mhandisi Issa.

Amesema hadi sasa miundombinu inaendelea kuunganishwa na malengo ni kwamba biashara ianze mara tu muunganiko wa miundombinu hiyo itakapokamilika.

"Tunaunganisha ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, mfano sisi na Kenya tayari na sasa hivi tunaendelea na Zambia ambapo kwa Tanzania tupo  tayari na tutakuwa tayari zaidi pale miundombinu itakapokamilika," amebainisha.


Amesema kwa kuanzia Tanzania inaunganisha Kusini na Mashariki kisha Kanda za Magharibi na Kaskazini zitakuwa tayari halafu kutakuwa na muunganisho wa gridi Afrika nzima ili nchi ziuziane umeme.

Wakati Mhandisi Issa, akiyabainisha hayo kwa upande wake Katibu Mkuu wa EAPP, James Wahogo amesema hii leo wanaangalia namna ya mashirika hayo ya umeme yatakavyotumia sheria zitakazofikiwa.

"Baada ya kujadili kisha zitapelekwa baraza la mawaziri wa nishati katika nchi hizi ambao wana mamlaka ya kuzipitisha ili iwe sheria kamili," amebainisha na kuongeza.

"Hadi 2027 tunategemea Jumuiya ya Mashariki na Kusini zitakuwa tayari zimeshakamilika ambapo wananchi watafaidika kwa kuwa watakuwa wanapata umeme kwa bei nafuu."

Naye, Crispen Zana kutoka Shirika la Maendeleo  Afrika AUDA NEPAD yenye lengo la kuwa na umeme mmoja wa Afrika amesema kuna Waafrika takribani milioni 600 wanaishi gizani, hivyo faida ya jambo hili ni kuwamulika Waafrika wote.

Amesema hadi 2040 tayari kutakuwa na nguzo za umeme mkubwa unaosafiri bara zima la Afrika huku akisema lazima wazingatie zaidi waafrika walio masikini.

"Nchi moja ikizalisha umeme mkubwa itauzia nyingine na hii ndivyo itakavyokuwa. Lazima tuangalie mikakati ya kuwasaidia wananchi wetu katika miaka 10 ijayo.”

"Kwa sasa kuna watu bilioni 1.2 na hadi mwaka 2050 inakadiriwa kutakuwa na watu bilioni 2.2 hivyo lazima tuangalie watu wetu masikini," amesema Zana.

Amesema jitihada za kila nchi ni kuwa na umeme ambao unatumiwa na watu pamoja na uchumi kwa ujumla.