DPP aondoa rufaa ya mwisho dhidi ya Sabaya, wenzake watano

Muktasari:

Rufaa hiyo iliyokuwa imepangwa kusikilizwa leo Mei 3, 2024 ilikuwa inapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/ 2021, iliyowaachia huru Sabaya na wenzake sita.

Arusha. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amewasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Arusha, nia ya kutoendelea na dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano.

Kufuatia nia hiyo, Mahakama hiyo imeridhia na kuiondoa rufaa hiyo ya jinai namba155/2022.

Mbali na Sabaya, wengine ambao rufaa dhidi yao imeondolewa ni, Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Rufaa hiyo iliyokuwa imepangwa kusikilizwa leo Mei 3, 2024 ilikuwa inapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/ 2021, iliyowaachia huru Sabaya na wenzake watano.

Leo kesi ilipoitwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi ili aendelee kusikiliza rufaa hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Akisa Mhando ameieleza mahakama kuwa DPP amewasilisha hati hiyo chini ya kifungu cha 386(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kufuatia hatua hiyo, Jaji Maghimbi ameiondoa rufaa hiyo iliyokatwa na Jamhuri ikipinga hukumu ya Juni 10, 2022 ya kesi ya uhujumu uchumi iliyowapa kina Sabaya ushindi, baada ya mahakama kuona ushahidi uliotolewa na Jamhuri uligubikwa na utata na hivyo kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Hii ni rufaa ya mwisho iliyokuwa imesalia mahakamani ikimkabli Sabaya ambaye kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani Juni 4, 2021 akikabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyofungulia baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumsimamisha kazi Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi, kisha kukamatwa akiwa Kinondoni jijini Dar es Salaam Mei 27 mwaka huo.


Rufaa iliyoondolewa

Rufaa iliyoondolewa na DPP ilikuwa ikipinga Sabaya na wenzake kuachiwa huru katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kwenye kesi hiyo, washtaakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 22, 2021 waliongoza genge la uhalifu, kupokea Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa, utakatishaji fedha na matumizi mabaya ya ofisi kwa Sabaya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.


Aenda kuchugua gari, fedha  Takukuru

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Wakili Mosses Mahuna aliyekuwa akiwawakilisha Sabaya na wenzake, alieleza kwa sasa Sabaya na wenzake hawakabiliwi na kesi nyingine.

“Kwa sasa kesi zote hazipo, zote zimeisha na sasa anaenda kuchukua gari lake Takukuru na mali zake zingine. Kulikuwa na fedha na vitu vingine vilivyokuwa kama vielelezo katika kesi ile,” amesema.

Amesema mteja wake hatarajii kuchukua hatua yoyote ya kuomba fidia wala chochote, kikubwa wanamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea.

“Mteja wangu amepitia changamoto nyingi na zimemjenga mno na hategemei kuchukua hatua yoyote. Tunaishukuru mahakama na haya yote tunasema ilikuwa mipango ya Mungu na ameimarika zaidi, amekuwa bora kuliko alipofikishwa mahakamani mara ya kwanza,”amesema Mahuna.


Kesi nyingine

Licha ya kesi hiyo, Oktoba 15, 2021 Sabaya na wenzake wawili, Daniel Mbura na Sylyvester Nyegu walikuwa na kesi ya jinai namba 105/ 2021 ambao walitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya kuthibitika kufanya unyang’anyi wa makundi na kuhukumiwa jela miaka 30 kila mmoja, walikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kupinga hukumu hiyo na kushinda.

Hata hivyo, waliendelea kukaa mahabusu kutokana na kuwa na kesi nyingine.

Mei 30, 2022 Sabaya alifunguliwa kesi nyingine ya uhujumu uchumi namba 2/2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ambapo alishtakiwa yeye na wenzake Nyegu, Aweyo, Msuya na Antoro Assey wakikabiliwa makosa saba ikiwemo ya rushwa.

Mahakama hiyo ilimwachia kwa masharti ya kutofanya kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh5 milioni baada ya kukiri kosa la kula njama na kuzia utekelezaji wa haki, chini ya makubaliano na DPP.

Novemba 17, 2023 Mahakama ya Rufaa Tanzania pia ilitupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na DPP dhidi ya Sabaya, Nyegu na Mbura na kuwaachia huru.