Hapi: Wananchi hawaiamini CCM kwa mavazi, nyimbo bali inavyoshughulikia kero zao

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ali Hapi akizungumza na wakazi wa Nyang'oro, Wilayani Iringa. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ali Hapi amewaka viongozi wa CCM kujikita katika kushughulikia kero za wananchi badala ya kutumia nafasi zao kuwakandamiza.

Iringa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi, Ali Hapi amesema kuwa imani ya wananchi kwa CCM, haitokani na mavazi wala nyimbo, bali wanavyoshughulikia kero za wananchi.

Kutokana na hilo, amewakumbusha viongozi wa chama hicho na jumuiya zake kushughulikia kero wa wananchi, badala ya kuwa sababu ya kuwakandamiza na kuanzisha migogoro.

Hapi ameyasema hayo leo Mei 3,2024  wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nyang’oro wilayani Iringa, katika ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe na halmashauri kuu ya chama hicho kushika wadhifa huo.

Ziara hiyo ilianza jana mkoani Iringa, kisha atakwenda Dodoma, Singida na kumalizia mkoani Tabora Mei 12-14, mwaka huu.

Amesema wapo baadhi ya watendaji wa umma ambao wamekuwa kero kwa wananchi, huku baadhi ya viongozi wa CCM wakishuhudia bila kuchukua hatua.

Hapi amesema imani ya wananchi kwa CCM haitokani na mavazi wala nyimbo, bali  ni namna wanavyoshughulikia kero za wananchi.

Amesema ni ajabu kuona baadhi ya watendaji hawatekelezi wajibu wao katika sekta mbalimbali wakati viongozi wa chama wapo.

“Msikae na kuzunguka na mashati ya kijani tu, ukiona mtendaji wa kata hatendi haki, mwenyekiti wa CCM kata unayo nafasi ya kumuita kwenye ofisi yako umuulize,” amesema Hapi.

Amesema, “CCM itapendwa na kuaminiwa tukitimiza wajibu wetu, watendaji miungu watu na wanaoonea watu lazima tushughulike nao.”

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin alisema kati ya mambo wanayosimamia ni kila kiongozi kutimiza wajibu wake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo amewataka waliofikisha miaka 18 kujiunga na jumuia hiyo na kuondokana na dhana kuwa ni ya wazee pekee.

“Jiungeni na jumuiya hii na siyo ya wazee peke yake, sote ni wazazi kama siyo leo kesho,” amesema.