Kesi inayowakabili watumishi 16 wa jiji la Dar yaiva

File Photo

Muktasari:

  • Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, 2024, ni baada ya upelelezi dhidi ya watumishi 16 wa Jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa taarifa na nyaraka muhimu zilizowasilishwa Mahakama Kuu, kuhusiana na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili watumishi 16 wa Jiji hilo, zimeshasajiliwa.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 142 yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia jiji hilo hasara ya Sh8.9 bilioni. 

Kusajiliwa kwa taarifa hizo, kunatokana na upelelezi wa shauri hilo kukamilika na tarehe ijayo washtakiwa watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo ili kesi hiyo iendelee kusikilizwa.

Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi, ameeleza hayo mahakamani  hapo leo Ijumaa Mei 3, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ajali Milanza, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mbilingi amedai baada ya kusajiliwa kwa taarifa hizo muhimu, wanaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na hatua inayofuata ambayo ni kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Hakimu Milanzi, amekubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Mei 30, 2024.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 32/2023 ni Tulusubya Kamalamo (53), Mkazi wa Ukonga na mwenzake James Bangu(57), Mkazi wa Kibada, ambao wote ni waweka hazina.

Wengine ni wahasibu wa jiji hilo ambao ni Mohamed  khais(41), Abdallah Mlwale(52), Deogratias Lutataza(55) na karani wa fedha, Judica Ngowo(51) maarufu Kama Lightness.

Wahasibu wengine ni Febronia Nangwa(44), Said Bakari, Glory Eugen(45), Josephine Sandewa(48), Dorica Gwichala(45), Jesca Lugonzibwa(53).

Pia yupo, Ofisa Afya wa Halmashauri hiyo, Patrick Chibwana (40), Ally Baruani(38) ambaye ni Meneja Mkuu; Khalid Nyakamande (34) Ofisa Mtendaji wa Mtaa na mhasibu Alinanuswe Mwasasumbe(60) Mkazi Mbagala Majimatitu.

Kati ya mashitaka hayo 142, lipo la kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo, ufujaji wa fedha na ubadhilifu, kughushi na kuisababishia hasara mamlaka.

Miongoni mwa mashitaka hayo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi 2019 na Juni 6, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh8.9 bilioni, mali ya halmashauri hiyo.

Katika shitaka la matumizi mabaya ya madaraka, washtakiwa wote wanadai Katika tarehe hizo, kwenye  ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nyadhifa zao mbalimbali, walishindwa kuingiza mapato ya halmashauri ya Jiji hilo yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kwenye akaunti ya jiji iliyopo katika benki ya NMB, CRDB, NBC na DCB na hivyo kujipatia manufaa yasiyo halali na hivyo kuisababishia hasara ya Sh8.9 bilioni.

Katika shitaka la kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo, washtakiwa hao wanadaiwa siku na eneo hilo, waliingiza taarifa za uongo kuonyesha mapato yaliyokusanywa  katika jiji la Dar es Salaam, waliingiza mapato hayo katika akaunti ya benki ya NBC, CRDB, NBC DCB, inayomilikiwa na Jiji hilo.

Pia wanadaiwa kughushi nyaraka kuonyesha kuwa ni halali wakati wakijua kuwa sio kweli.

Shitaka la kuisababishia hasara, washtakiwa hao wadaiwa katika kipindi hicho, wakiwa watumishi wa halmashauri hiyo, kwa makusudi walilisababishia hasara Jiji la Dar es Salama ya Sh8.9 bilioni.