Watuhumiwa kulinda bangi wanazolima kwa 'bunduki'

Kamishna Msaidizi wa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya kanda ya kati, Mzee Lasuwi (kushoto) akimkabidhi silaha aina ya Gobore Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ACP Theopista Mallya. (Picha na Hamis Mniha)

Dodoma. Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya (DCEA), imewakamata watu 18 kwa kuhusika na kilimo cha bangi huku wawili kati yao wakikamatwa na magobore waliyokuwa wakiyatumia kulinda mashamba hayo.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Machi 3, 2024 na Kamishna Msaidizi wa DCEA, Kanda ya Kati Mzee Kasuwi wakati akikabidhi silaha mbili kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya.

Silaha hizo zilipatikana kwenye operesheni iliyofanyika kati ya Aprili 24 hadi 28, 2024.

Kasuwi amesema katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata silaha hizo zilizokuwa zinamilikiwa na wakazi wa Segera, Hamisi Chambo (46) na Abdalah Juma (45).

"Aprili 24 hadi 28 mwaka 2024, mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kanda ya kati Dodoma imefanya operesheni katika maeneo ya Wilaya ya Chamwino na Dodoma Mjini na kufanikiwa kuteketeza ekari 9.5 za mashamba ya bangi," amesema Kasuwi.

Pia, amesema pia wamekamata jumla ya kilo 156.23 za bangi na misokoto 127. Watu 16 wamekamatwa kuhusika na dawa hizo na watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika," amesema Kasuwi.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Kasuwi amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga simu kupitia namba ya 199 bila gharama.

Kamanda Theopista ameishukuru mamlaka hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutokomeza uhalifu.

Ametoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kumiliki silaha hatarishi, badala yake wafuate sheria za nchi na taratibu zake.

Amesema Jeshi la Polisi lipo na litaendelea kutokomeza matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

“Kuna maeneo ambayo tumeelekezwa na tutaenda kuwakamata sababu hawa watu wanalinda haya mashamba kwa kutumia silaha za moto kwa hiyo wananchi waone uhatari uliopo wa hawa watu ambao wanajihusisha dawa ya kulevya,” amesema.

 Amewataka wananchi kuwafichua watu wanaojihusisha na biashara hizo kwani wamekuwa hatari kwa jamii na kwa Taifa.