Chumvi inavyochochea shinikizo la juu la damu

Dar es Salaam. Iwapo unataka kuepuka shinikizo la juu la damu na maradhi yanayoambatana na ugonjwa huo, wataalamu wameeleza mambo matano mtu unayopaswa kuyafuata kuepuka tatizo hilo wanalolitaja ni ‘muuaji msiri.’

Mambo ya kuzingatia ni ulaji wa chumvi iliyopikwa pamoja na kupunguza matumizi makubwa ya bidhaa hiyo.

Mwili wa binadamu unahitaji chumvi, kutokana na bidhaa hiyo kuwa na madini ya sodium ambayo ni muhimu katika mwili. Hata hivyo, uhitaji wake si wa kiwango kikubwa.

Uhitaji mdogo unashauriwa, hii ni kutokana na mwili kuwa na uwezo wa kudhibiti upotevu wa chumvi. Matumizi ya bidhaa hiyo yanaweza kupunguzwa.

Tafiti zinaonesha uwekaji wa chumvi ambayo haijapikwa kwenye chakula hutoa asilimia 90 ya madini ya sodium ambayo humweka mtu hatarini kupata shinikizo la juu la damu, kifafa cha mimba, saratani ya tumbo, magonjwa ya figo, moyo na mishipa na mengineyo.

Chuo Kikuu cha Harvard na Taasisi ya Taaluma ya Mapishi nchini Marekani, wamependekeza njia mbalimbali zinazokubalika kisayansi za kupunguza ulaji wa chumvi nyingi kupita mahitaji ya mwili.

Moja ya njia pendekezwa ni kuwa na mlo nusu sahani, ulioambatana na matunda pamoja na mboga za majani.

Jambo lingine ni kupunguza matumizi ya kupitiliza ya sukari na mafuta ya kupikia, kufanya mazoezi yanayoufanya mwili kutoa jasho na kuepuka msongo wa mawazo.

Kuhusu mafuta ya kupikia, hayo yameelezwa hupunguza kiwango cha mafuta mazuri mwilini na kuongeza mafuta yasiyohitajika.

Njia za kujikinga na ugonjwa huo zinatajwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Tulizo Shemu katika mahojiano maalumu, akizungumzia maadhimisho ya siku ya Shinikizo la Damu Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Mei 17.

Ukubwa wa tatizo hili unaoneshwa kupitia takwimu za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambako wagonjwa 100,025 waliofika kupata matibabu, asilimia 52 walibainika kuwa na shinikizo la damu.

Dk Tulizo anafichua kuwa kati ya watu wazima 10, watatu mpaka watano kwa Tanzania wana shinikizo la juu la damu na zaidi ya asilimia 60 hawajitambui.

“Ugonjwa huu madhara yake ni makubwa, unasababisha watu kupata kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, mshtuko na vifo vya ghafla, kupumua kwa shida na kuvimba miguu, macho kutoona, kifafa cha mimba na kupoteza ujauzito,” anasema.

Unaweza kutambua kama unashambuliwa na ugonjwa huu kama utahisi maumivu makali ya kichwa, macho, kifua kubana na mapigo ya moyo kwenda haraka, lakini wataalamu wanasisitiza hakuna dalili za moja kwa moja za ugonjwa huu, hivyo ni muhimu kufanya vipimo.


Uelewa ukoje

Utafiti uliofanywa kwa mikoa mbalimbali na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dk Pedro Pallangyo kuangalia uelewa wa sababu za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, hususan ya moyo na kama watu wanaishi kulingana na uelewa kama wanayo.

Mikoa iliyohusishwa kwenye utafiti ni Arusha, Dar es Salaam, Mtwara na Geita pamoja na Zanzibar kwa visiwa vya Unguja na Pemba ambapo jumla ya watu 5,121 walihojiwa.

Dk Pallangyo anasema katika mikoa yote mitano uelewa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni wa kuridhisha, asilimia za uelewa zilikuwa kati ya 74.6 hadi 83.7 katika mikoa yote ambapo kwa vifaa tulivyotumia uelewa ulipaswa kuwa juu ya 50.

Dk Pallangyo anasema pamoja na uelewa kuwa mzuri, sababu za hatarishi za moyo zilikuwa kwa kiwango cha juu bila kuzingatia uelewa, wakiangalia uvutaji wa sigara, uzito kupitiliza na kutofanya mazoezi.

“Ukiacha uvutaji wa sigara ambao ulikuwa wa kuridhisha, kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, uzito kupindukia na shinikizo la damu zilikuwa juu kwenye jamii husika, sasa hii inazua maswali mengi watu wanafahamu sababu hatarishi lakini hawajabadili mwenendo wa maisha yao, hivyo mwenendo wa maisha uko vibaya sana,” anasema.


Ugonjwa unavyowatafuna watu

Kwa mujibu takwimu za Wizara ya Afya, kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 magonjwa yaliyoongoza kwa wagonjwa wa nje (OPD) wenye umri chini ya miaka mitano shinikizo la juu la damu liliathiri kundi hilo kwa asilimia 5.9, sawa na wagonjwa 737,730.

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya iliyowasilishwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu mapema wiki hii, magonjwa yaliyoongoza kwa wagonjwa waliolazwa wenye umri chini ya miaka mitano ni shinikizo la juu la damu lililochukua asilimia 8.81.

Pia, kupitia hotuba hiyo, Waziri Ummy anasema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, idadi ya wagonjwa waliohudhuria katika vituo vya kutolea huduma kutokana na magonjwa yasiyoambukiza walikuwa milioni 4.65, sawa na asilimia 13 ya wagonjwa wasiolazwa.

Idadi hiyo ni ongezeko la wagonjwa milioni 4.263, sawa na asilimia 12.8 waliohudhuria katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

“Wagonjwa waliolazwa walikuwa 271,068, sawa na asilimia 20.1 ikilinganishwa na wagonjwa 242,596 sawa na asilimia 19.9 katika kipindi kama hicho, mwaka 2022/23.

Kipindi cha mwaka 2023/24 shinikizo la juu la damu liliongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa nje kwa magonjwa yasiyoambukiza, wakichangia asilimia 26.1,” anasema Waziri Ummy.

Aidha, asilimia 25 ya sampuli za chumvi zilizofungashwa katika pakiti zilizokusanywa kutoka katika maduka ya rejareja hazikuwa na madini joto.

Kuhusiana na sampuli za chumvi kutoka ‘supermarkets’, mchanganuo wa kimaabara unaonesha kuwa asilimia 54.6 ya chumvi hizo hazikuwa na madini joto.