Gamondi hajapoa, amuulizia Fabrice Ngoma

Simba msimu huu imekuwa na kiwango ambacho hakiwafurahishi mashabiki wake lakini kuna wachezaji ambao wamekuwa vipenzi vya mashabiki na wanaamini kama wataendelea kuwepo, miamba hiyo ya Ligi Kuu Bara msimu ujao itatisha na kusahau machungu ya misimu miwili mfululizo mbele ya watani zao, Yanga.

Moja ya majina yanayotajwa yanawakosha mashabiki wa timu hiyo, ni kiungo mkabaji wa Simba, Fabrice Ngoma na pamoja na kiwango chake bora alichoonyesha tangu asajiliwe akitokea Al Hilal ya Sudan kimewamfanya aanze kuuliziwa na timu kuanza kutuma ofa zao.

Hilo ndilo lililomfanya kocha wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Miguel Gamondi kuiulizia huduma yake kwa kile alichokifanya kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Chanzo cha uhakika kimesema Kocha Gamondi aliulizia huduma ya mchezaji huyo baada ya mchezo dhidi ya watani zao Simba na licha ya kushinda dabi mbili walizokutana msimu huu, jicho la kocha huyo raia wa Argentina lilimtazama Ngoma na kugundua anaweza akaongeza kitu kwenye kikosi cha Wanajangwani.

“Baada ya dabi Kocha wa Yanga aliulizia iwapo wataweza kumpata Ngoma ingawa yeye anasisitiza bado ni mchezaji wa Simba kwani ana mkataba wa mwaka mmoja," kilisistiza chanzo hicho.

Pamoja na Gamondi, Mwananchi inajua pia kuna timu za Afrika zinazoitaka huduma ya staa huyo ambazo ni Pyramids FC na Al Ahly za Misri, Raja Casablanca (Morocco) kutokana na kiwango chake bora.

Chanzo cha uhakika kimesema pia baada ya Ngoma kuonekana kufanya vizuri kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilipocheza dhidi ya Al Ahly, kocha wa timu hiyo, Marcel Koller hakusita kuanza mchakato wa kuhitaji huduma yake.

"Koller alimwambia ni mchezaji mzuri na anatamani kuwepo naye kwenye kikosi chake, baadaye ofa ikaja, lakini mchezaji huyo ana mkataba na Simba, hivyo timu zote zinazomhitaji zitakaa mezani, kufanya dili hilo," kilisema chanzo hicho na kuongeza:

"Kuhusu kocha wa Pyramid ambaye ni raia wa Croatia, Krunoslav Jurcic, naye alimpigia mchezaji kumwambia amevutiwa na uchezaji wake, akataka kujua zaidi kuhusu mkataba wake ili aangalie namna gani, anaweza akawa sehemu ya kikosi chake."

Ikumbukwe kuwa kiungo huyo aliwahi kuichezea Raja kabla ya kuamua kutimkia Kuwait kisha kutua Al Hilal ya Sudan na baadaye aliamua kuvunja mkataba kutokana na machafuko nchini humo na kujiunga na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Alianza kuifungia Simba kwenye mchezo wa Simba Day dhidi ya Power Dynamo kwenye ushindi wa mabao 2-0, huku moja akifunga Willy Onana.

Kwenye Ligi Kuu Bara amefunga mabao mawili lakini ameonyesha ubora kiungo ya kati na kuwakosha mashabiki na makocha ambao wanatamani kufanya nao kazi.