ZFDA yapiga marufuku maziwa ya Infacare kuuzwa Zanzibar

Maziwa ya kopo aina ya Infacare yaliyopigwa marufuku Zanzibar.

Unguja. Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) imepiga marufuku uingizwaji, uuzwaji na usambazaji wa maziwa ya kopo aina ya Infacare kutokana na kuwepo maandishi kwenye bidhaa, yanayokataza kuuzwa nchini hiyo.

 Kaimu Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula, Khadija Ali Sheha amesema hayo jana kwamba hatua hiyo inalenga kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla.

Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanafanya udanganyifu wa kuchuna maandishi hayo na kubandika stika juu yake au kubadilisha mifuniko halisi na kuuza bidhaa hiyo, jambo alilosema ni kosa kisheria.

“Hatua mbalimbali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa walioghushi na kuingiza nchini bidhaa hiyo, kinyume na taratibu zilizowekwa na ZFDA,” amesema bila kuwataja majina wala idadi yao.

Khadija amesisitiza kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini wafanyabiashara wababaishaji na kuwachukuliwa hatua za kisheria watakaobainika kuwa na makosa.

Alisema ZFDA imesitisha matumizi ya maziwa hayo kutokana na kutokidhi matakwa ya sheria na vigezo vya bidhaa za chakula, kutosajiliwa na kutothibitishwa kwa ubora na usalama na wakala wa dawa, chakula na vipodozi.

Amesema maziwa yaliozuiliwa kuwa ni Infacare 1, 2 na 3 ambayo yapo kwa nambari tofauti za mkupuo na tarehe za uzalishwaji ndani ya Zanzibar.

Maziwa hao yanauzwa kati ya Sh18, 000 hadi Sh20, 000 kwa kopo.

Aliishauri jamii kutumia vyakula vilivyothibitishwa na kutoa ushirikiano pale wanapokuwa na shaka juu ya bidhaa zilizopo sokoni, kwa kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja.

Katika ukaguzi uliofanya na wakala wa chakula, dawa na vipodozi wamefanikiwa kutoa sokoni zaidi ya makopo 1,000 ya maziwa hayo, yakiwa na maandishi yanayosomeka ‘not for resale in Tanzania’ yaani yasiuzwe tena nchini.

Baadhi ya wananchi wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusu kuzuia maziwa hao wengine wakipongeza.

Ameir Said amesema ipo haja mamlaka kuongeza usimamizi ili kuzuia mapema bidhaa ambazo zinakuwa hazikubaliki, badala ya kusubiri zinaanza kutumika ndipo wanakuja kuchukua hatua.

“Nadhani umakini uongezwe zaidi kwenye kudhibiti na si kukamata, kwa sababu kama ni madhara tayari yameshatoke,” amesema.

Ashura Khamis amesema alikuwa anatumia maziwa hayo kwa watoto wake, hata hivyo hakuwahi kubaini madhara yoyote. 

“Haya maziwa ndio nilikuwa natumia kwa watoto wangu wote watatu, japo sikuwahi kuona madhara kwao,” alisema.