Namna lugha inavyoweza kuathiri biashara ya huduma za kifedha

Kiswahili ni lugha kuu inayotumika na Watanzania wengi wanaotumia huduma rasmi za kifedha nchini. Taarifa za Ripoti ya Utafiti wa Maoni ya Watumiaji wa Huduma za Kifedha nchini (Finscope,2023), inaonesha asilimia 79 ya watu nchini wanatumia Kiswahili kama lugha ya kuwasiliana katika kupata huduma hizo.

Katika utoaji huduma matumizi ya lugha ni jambo muhimu linaloweza kustawisha au kubomoa biashara.

Katika kujenga, lugha ni nyenzo muhimu ya kuwasiliana na wateja, kuhabarisha, kuelimisha kuhusu huduma au bidhaa. Namna rahisi lugha itakavyotumiwa ndio ujumbe utaweza kufika kwa ufanisi, kukubaliwa na kushawishi wateja na mwishowe kuongeza wigo wa soko la huduma fulani inayotolewa na kampuni.

Aidha, lugha ni mtego wa kumnasa mteja, ukiachilia mbali yenye kueleweka, matumizi ya lugha kwa maana ya maneno mazuri inaongeza mguso, na kufanya mteja kujihisi salama zaidi na mwenye kusikilizwa, na mwishowe kuwa mwaminifu kwa biashara hiyo.

Mifano sote tunayo, mtu anaweza kukata mitaa kufuata bidhaa duka fulani kwa sababu tu ya wahudumu wanaosikiliza na wenye lugha nzuri!

Hivyo, watoa huduma za kifedha kama benki, bima, mitandao ya simu kuna mambo kadhaa wanaweza kufanya kuongeza tija zaidi kimasoko, utafutaji wateja, na kuongeza mauzo ya huduma au bidhaa kwa kuzingatia kigezo lugha;

Kwanza, lugha rahisi itumike na kwa baadhi ya wakati watoa huduma wawe makini na matumizi ya misamiati ya kitaalamu katika kuwasiliana na wateja, kwa sababu wengi wanaweza kuwa hawajui kabisa lugha ya Kiingereza au wengine wanaweza kuwa kiwango cha uelewa tofauti.

Hivyo, maneno kama deposit, transaction, interest, fixed account, na mengine ni rahisi, lakini inategemea na aina ya mteja, wengine wanaweza kupata changamoto ya istilahi hizo na ikapelekea ujumbe usieleweke kwa urahisi.

Pili, sambamba na hilo, jumbe za kwenye mbao za matangazo, vipeperushi, mabango ya barabarani, na kampeni za kuelimisha kuhusu bidhaa, namna ya kutumia huduma, yanaweza kufika vizuri kwa wateja ikiwa lugha wanayoielewa itatumika.

Tatu, uandaaji wa kampeni au matangazo unaweza pia kuzingatia lugha za rika ili ujumbe uweze kufika kwa urahisi, mathalan, kaulimbiu kama; Akiba ndio Mchongo!, Mpunga Mrefu Bila Tozo!, Mkopo kama Wote!, na mengine, inaweza kutumika kunadi huduma zinazolenga kundi la vijana na itasaidia kueleweka kwa haraka na urahisi.

Nne, matumizi ya lugha yaongezewe taswira ya utamaduni kulingana kundi la wateja linalolengwa na mtoa huduma. Kwa mfano, kama huduma inalenga kuhamasisha Jamii ya Wavuvi Pwani ya Tanga kufungua akaunti za Benki, tangazo linaweza kuwa na mvuto zaidi kuonesha mhusika amevaa seruni, kofia, kuliko picha ya mhusika aliyevaa suti nzuri na miwani.

Tano, yapo baadhi ya maeneo lugha za makabila zinatumika zaidi kuliko Kiswahili, watoa huduma wanaweza kubuni mbinu za kuyafikia masoko hayo, kwa mfano kuwa na mbinu ya maofisa wanaojua lugha hizo na kuwatumia katika kuwasilisha elimu kuhusu bima ya mazao kwa Kisukuma, Kihehe na lugha nyingine inaweza kuleta tija nzuri.

Sita, ajenda kuhusu huduma mbalimbali za kifedha inaweza kuchopekwa katika maudhui yanayofuatiliwa na Watanzania wengi, kwa mfano, ujumbe kuhusu kuweka akiba, kukopa, namna ya kutuma au kupokea fedha inaweza kuakisiwa katika tamthilia na maigizo ya Kiswahili.

Vilevile, kuna umuhimu kwa watoa huduma za kifedha kwa kushirikiana na taasisi za usimamizi wa lugha ya Kiswahili kuendelea kubuni misamiati ya kifedha kwa Kiswahili ambayo itatumika katika mawasiliano ya utoaji huduma hizo kati ya watoaji huduma na wateja.