Jaji Warioba achambua miaka 60 ya Muungano, agusia haya

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Muktasari:

Aprili 26, 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuwa Taifa moja la Tanzania. Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amezungumzia masuala kadhaa ikiwamo mjadala wa muundo wa Muungano na miaka 60 mingine ijayo kipi kinapaswa kufanyika

Dar es Salaam. Safari ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imebakiza siku kumi kufikisha miongo sita, ingawa muundo wake unabaki kuwa jambo linaloendelea kujadiliwa mara kwa mara.

Aprili 26, miaka 60 iliyopita ndipo mataifa hayo yalipoungana na kuunda Tanzania na hadi sasa zimesalia siku chache kwa Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya Muungano.

Pamoja na ukongwe wa Muungano huo ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar, mijadala kuhusu muundo wake inabaki kuwa kitendawili kisichoteguka.

Mijadala hiyo kuhusu muundo huo wa Muungano imefikisha wananchi katika hatua ya kutaka ipewe uzito katika rasimu ya mabadiliko ya Katiba na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba analithibitisha hilo.

Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anataja muundo wa Muungano kuwa moja kati ya mambo manne yaliyozungumzwa zaidi wakati wa ukusanyaji maoni ya rasimu ya Katiba mpya.

Waziri Mkuu huyo mstaafu na Makamu wa kwanza wa Rais, katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital yaliyofanyika Aprili 5, mwaka huu ofisini kwake jijini Dar es Salaam anayataja mambo yaliyozungumzwa zaidi katika maoni hayo ni suala la maadili, madaraka ya Rais, mambo ya uchaguzi na Muungano.

Kulingana na Warioba, kitendo cha muundo wa Muungano kuzunguzwa zaidi katika ukusanyaji maoni hayo, ni ishara ya uwepo wa tatizo kwenye eneo hilo.

"Sasa ni miaka 60, hili limekuwepo tangu wakati wa Tume ya Nyalali, wakati wa G55 na wa Tume ya Kisanga hadi sasa kwenye tume ya mabadiliko ya katiba," anasema Jaji Warioba.

"Wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba tunakusanya maoni, wananchi walilizungumza sana hili na kwa uzito, hii inaonyesha tatizo lipo," anasema Jaji Warioba aliyekuwa mwenyekiti wa tume hiyo iliyoundwa 2010 wakati wa Rais Jakaya Kikwete.

Anasema tume aliyoiongoza ilipokabidhi taarifa yake, moja ya masuala manne makubwa yaliyozungumzwa kwa uzito na wananchi na kuonyesha kuwagawa wengi ni  hilo la muundo wa Muungano.

"Walitaka muungano imara, inaonyesha tatizo lipo na kama nilivyosema, tuendelee na majadiliano ili tukifika 2025, tuwe tumefikia uamuzi kwenye yale maeneo manne yaliyozungumzwa sana na wananchi likiwamo ili la Muungano," anasema.

Msisitizo wa Jaji Warioba kuhusu hilo ni kufanyika uamuzi utakaohusisha wananchi kupewa nafasi ya kuidhinisha kabla ya kwenda kupata Katiba mpya.

Katika rasimu ya mabadiliko ya Katiba maarufu Rasmi ya Jaji Warioba ilikuwa na mapendekezo ya miaka 50 ijayo.

Nchi ipo katika mchakato wa kuandaa dira ya miaka 2025/50, kipindi ambacho Jaji Warioba anasema watu wameongezeka lakini ardhi ni ile ile.

Kutokana na mazingira hayo, kiongozi huyo mwandamizi serikalini, anasema kuna haja ya kuijadili kwa makini dira ya miaka 25 ijayo ili nchi ijue inataka ifanye nini kupata maendeleo kwa haraka.

"Japo ningependa isiwe miaka 25 tu, tungeangalia miaka 50 ijayo Tanzania itakuwa wapi.

"Mara nyingi huwa napenda kuchokoza chokoza watu kuhusu dira yetu ya 2025/50, siku moja nikamuuliza kiongozi wa chama kimoja cha siasa kwamba Serikali inaanda dira hiyo, ni nini msimamo wa chama chenu akasema bado hawajalizungumza!" anasema Jaji Warioba akionyesha kushangazwa na kauli hiyo na kuongeza.

"Hiki ni kitu ambacho tunapaswa kukijadili kwa makini ili tujue tunataka tufanye nini ili tupate maendeleo kwa haraka, mbaya zaidi viongozi hatuzungumzi sana kuhusu maendeleo, yanapokuja huwa yanakuwa kama matukio tu, lakini ukweli ni lazima tuyapange," anasema.

Anasema wakati Tanganyika (Sasa Tanzania) inapata Uhuru Desemba 9, 1961, nchi ilikuwa na watu milioni tisa.

"Sasa tuko milioni 60, miaka 60 ijayo tunaweza kuwa hata milioni 200 lakini ardhi yetu ni ile ile haiongezeki.

"Tunahitaji tuwe na mipango, tuone kama  tunaongezeka na ardhi ni ile ile ni nini tufanye  kwa rasilimali tulizonazo tukitumia sayansi na teknolojia ili tupate maendeleo," anasema.

Kinachotakiwa sasa kwa mujibu wa Jaji Warioba ni kuweka msingi wa maendeleo kwa kuwa rasilimali watu ipo ya kutosha, kwa kufanya hivyo, Taifa litapiga hatua kwa haraka.

Hata hivyo, anaeleza kutoridhishwa namijadala ya Watanzania kwa miaka 30 iliyopita kujikita kwenye siasa zaidi badala ya maendeleo.

Adui watatu

Jaji Warioba anaeleza namna nchi ilivyoweka dira ya maendeleo kupambana na adui watatu baada ya kupata Uhuru.

Anasema waasisi (Nyerere na Karume) walitoa dira ya maendeleo ambayo ndiyo inatumika hadi sasa.

Dira hiyo ilieleza, ili kuwe na maendeleo lazima kupambana na adui watatu, ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

"Hii ilikuwa na maana kwamba maendeleo ni ya wananchi. Sasa ni miaka 60, pamoja kwamba tuko nyuma kulinganisha na nchi nyingine, lakini tumepiga hatua fulani fulani.

"Mfano kwenye ujinga, wakati ule tumepata uhuru shule za msingi zilikuwa ni chache na hata waliosoma nao walikuwa ni wachache," anasema akijitolea mfano yeye.

"Mimi nimesoma shule ya tarafa ambayo kila darasa kuanzia la kwanza hadi la nne lilikuwa na wanafunzi 45, shule nzima tulikuwa wanafunzi 180 ilikuwa ni idadi ndogo."

Anasema siku hizi, shule ni nyingi na wanafunzi ni wengi, kwani zama zile mara tu baada ya uhuru hata sekondari  zilikuwa ni chache na sasa kila kata ina sekondari na nyingine ni zaidi ya moja.

Pia, kwenye elimu ya juu, anasema nchi ilipopata uhuru anakumbuka muda mfupi kabla uhuru ndiyo ilikuwa imeanzisha chuo, kilikuwa na wanafunzi 13.

"Hivi sasa tuna vyuo vikuu vingi, japo hii haina maana kwamba taifa limetokomeza ujinga kwamba ndio umepungua," anasema.

Jaji Warioba anasema, pamoja na kuwepo watoto wengi kwenye shule za msingi, bado hakuna madarasa na walimu wa kutosha, wengine wanasoma chini ya miti na hii ndio inasababisha hadi wengine wanasoma na kuhitimu elimu ya msingi miaka saba na bado hawajui kusoma.

Anasema hata vifaa vya kufundishia, bado ni tatizo na wanafunzi wengi wamekuwa wakijifunza kwa nadharia hivyo bado kuna kazi kubwa kuimarisha elimu ya sasa.

"Hata kwenye maradhi, hadithi ni ile ile, mfano ni kwenye huduma za afya, wakati wa ukoloni hospitali kubwa haikuwa kwa ajili ya mwananchi wa kawaida bali kwa ajili ya wazungu.

"Tulipopata uhuru tukawa na Sewaaji ambayo ilikuja kuwa Muhimbili, Dispensari zilikuwa ni chache, vituo vya afya na hospitali za wilaya, hivi sasa tunaona zipo nyingi tumepanua wigo, japo hazijatosheleza lakini tumepanua wigo, hata hivyo huko napo kuna matatizo yaleyale.

"Unalo jengo zuri la hospitali, lakini hauna madaktari wa kutosha, hauna vifaa tiba wala wahudumu wa afya wa kutosha, bado huduma hazijaimarika, tulisema kila wilaya ijengwe hospitali, lakini zipo hospitali huko ukienda ni jengo lipo, lakini huduma sio imara, bado tuna kazi kwa kuwa  maendeleo ni watu sio kitu," anasema Jaji Warioba.

Vijana, wakulima ni masikini

Kwenye masuala ya kijamii, Jaji Warioba anaeleza namna ambavyo wananchi wengi ni masikini, akigusia taarifa ambayo ilionyesha wakati wa janga la uviko-19, ilionyesha watu wanaoishi chini ya uwezo wa kuishi iliongezeka.

Anasema, nchini hali ilivyo, kundi kubwa la watu masikini ni wale wa vijijini na vijana, akifafanua watu wa vijijini wengi wao wanategemea kilimo kiendeshe maisha yao.

"Elimu aliyonayo mkulima wa sasa ni tofauti na aliyokuwa nayo baba yangu,  huyu wa sasa anajua ni lazima aandae shamba mapema, apate mbegu nzuri, apate mbolea na pembejeo, lakini mazingira ya kuvipata vyote hivyo kwa mkulima wa kawaida ni magumu.

"Tunajua mbolea, pamoja na kwamba ni ya ruzuku, lakini ukiifuatilia utakuta inaishia kwa watu wa katikati, wakulima wanabaki kuendelea na matatizo yao mengi waliyonayo.

"Hata njia za mkulima kupata mapato zinasimamiwa na Serikali kwa manufaa ya umma, mtu mwenye kiwanda anaweza kutengeneza bidhaa atapanga bei yake na kuuza popote, lakini kwa mkulima anabanwa na soko," anasema.

Jaji Warioba anasema, kwenye kilimo kwanza kuna changamoto ya soko huru, akifafanua kwamba mara nyingi hawezi kupata bei ambayo itamfidia gharama aliyoitumia.

"Anawekewa masharti wapi pa kuuza, haya ni matatizo tangu zamani, hapo bado hujaongelea mabadiliko ya tabia nchi na huyo mkulima kukosa uhakika wa mazao, inatakiwa kazi kubwa ya kumuangalia huyu."

Anasema yaliyofanywa kwa wakulima huko nyuma ndiyo msingi wa nchi kujitegemea kwa chakula, akitolea mfano mkakati wa ‘Big 4’ uliofanyika miaka ya nyuma.

"Japo sasa kuna mikoa mingi, lakini wakati ule ilikuwa ni Iringa, Mbeya, Ruvuma na Rukwa, walipewa elimu ya kilimo, iliyofanya wapate mazao mengi tukaweza kujitegemea, tusipokazania kilimo itafika mahali tusiweze kujitegemea kwa chakula," anasema.

Anasema eneo jingine la kupambana nalo ili kuondoa umasikini ni kwa vijana ambao kwenye elimu wengi wamesoma lakini hawana kazi, jambo ambalo amesisitiza huko napo kunapaswa kuangaliwa.

"Mfano mdogo tu ukipita kwenye maeneo mengi ya Dar es Salaam iwe wakati wa mvua au jua kali na joto, utawaona vijana wanatembeza vitu vidogo vidogo ili wajikimu," anasema Jaji Warioba.

Waziri Mkuu huyo mstaafu pia aligusia hali ya uchumi wa nchi kwa jumla na kueleza ulivyo kwa sasa ni kama mgonjwa aliyekuwa akiumwa na kuanza kupata ahueni.

"Kwenye hili wananchi lazima waambiwe ukweli kwamba tunayo matatizo kwenye uchumi, sio kila kitu tuseme kinaenda sawa, unafahamu uchumi wa dunia unapoyumba, ndipo hata bei ya mafuta na gharama nyingine nyingi zinapanda.

"Tumekuwa na matatizo ya kupata dola, hii inasababisha shilingi yetu inateremka, hiyo inasababisha madhara na kufanya uwezo wetu kununua vitu kuwa mdogo na madeni yetu kuzidi kuwa makubwa, tunayo matatizo hivyo tujadiliane namna ya kuyatatua."

Anasema vita vinavyoendelea Ulaya, mabadiliko ya tabia nchi, janga la Uviko-19, mvua za El Nino vimefanya na vitaendelea kufanya fedha nyingi kutumika, ikiwamo kwenye ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua.

Anasema, kuna haja sasa wa kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima akitolea mfano moja ya nyakati, nchi ilipokuwa katika hali ngumu ya uhaba wa mafuta.

Anasema, wakati ule walijadiliana namna ya kubana matumizi na kupunguza baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima.

'Wenye magari walihimizwa kuwasaidia lifti majirani zao, tulijifunga mkanda na kupunguza vitu vingi visivyo vya lazima, hivyo katika matatizo kama hayo tunapaswa kwanza kusimamia kila senti tunayoipata itumike kwa makini, tupunguze mambo yasiyo ya lazima."

Anasema, siku hizi vinafanyika vitu vingi vya anasa, akigusia safari na kufafanua kwamba zinakuwa ni misusururu ya magari pasipo ulazima huo.

"Inabidi tufike mahali tuseme katika hali hii, lazima tujibane, pia suala la kupunguza matumizi ni la wakati wote ili tunachokipata tukipeleke katika maeneo ya kusaidia wananchi,

"Huu pia ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani kuna uchaguzi mkuu, hiki ni kipindi cha kukiangalia sana, kama Serikali isipokuwa makini tusishangae mapato ya nchi yakaingia kwenye mifuko ya watu sababu ya mambo ya kisiasa kwani ni kipindi ambacho kina mchwa wa kutafuna pesa hizo," anasema Jaji Warioba akitoa angalizo kwenye matumizi ya pesa za Umma.

Suluhisho kuporomoka maadili

Jaji Warioba amezungumzia pia kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa matukio ya kikatili huku akishauri nchi iangalie msingi wa hilo na kutafuta suluhu.

"Tunaona matatizo yatatokea kila wakati, wataalamu wanasema tuangalie tiba ya maradhi ya afya ya akili, nadhani ni zaidi ya hilo.

"Yawezekanna ni ugumu wa maisha pia unachangia, lakini maadili yameporomoka, huwa sielewi nini kinamsukuma mtu kwenda kumbaka mtoto mdogo, au mtoto wake, wengine wanaua wake zao.”

Anasema kuna haja ya kutafuta msingi wa matukio hayo, sababu zake ni nini na kuangalia suluhisho.