Dk Mwinyi atoa maagizo kwa ZSSF

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ( ZSSF).

Muktasari:

  • Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umefikisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake huku Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akiutaka kwenda kujifunza kwa wengine wanaofanya vizuri ili kuongeza tija.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 25 ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), bado haujawekeza kwenye miradi mikubwa zaidi.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mwinyi ameutaka uongozi wa mfuko huo kujifunza kwa wengine ili kuongeza ufanisi kwenye uwekezaji wenye tija zaidi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 25, 2023 wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya mfuko huo kisiwani Zanzibara ambapo amesema sekta ya hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu ya uchumi inayotegemewa na nchi pamoja na wafanyakazi.

“Licha ya mafanikio makubwa ya ZSSF ndani ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, bado haijawekeza kwenye miradi mikubwa zaidi, hivyo ni wajibu wetu kujifunza kwa wengine ili kuongeza ufanisi kwenye uwekezaji wenye tija,” amesema

Amesema lengo la kuanzishwa kwa sekta za huduma za jamii ni kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa mujibu wa sheria zilizopo na kwamba mataifa yaliyoendelea pia yalichangiwa kutokana na uimara wa huduma hizo.

Hata hivyo, amesema hana mashaka na miradi inayotekelezwa na mfuko huo na inayopangwa kutekelezwa kwani itaongeza tija na kukuza uchumi na kutoa fursa nyingi za ajira nchini huku akiupongeza kutekelza agizo lake la kuongeza pensheni kwa wastaafu wa kima cha chini kutoka Sh90,000 hadi Sh180,000.

Naye, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Nassor Shaaban, alisema mfuko unatekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 90 na kusajili wanachama wapya.

Alisema mfuko umeongeza uwekezaji wake kwa asilimia 58 kwa kipindi cha kuanzia Desemba 2020 hadi Juni mwaka huu ambapo mfuko umefanya uwekezaji wa Sh350 bilioni huku ukisajili wanachama 146,081.

Miongoni mwa mafao yanayotolewa na ZSSF ni pamoja fao la kustaafu, uzazi, fao la wenye ulemavu, kuumia kazini na fao la wajasiriamali.