Hakuna mtoto atakayeachwa elimumsingi

Muktasari:

Serikali yajipanga kuwa na miundombinu kwa ajili ya kuchukua wanafunzi wote watakaomaliza elimu ya msingi mwaka 2027. Ndio mwaka ambao wanafunzi wanaoishia darasa la sita na wanaoishia la saba watamaliza shule kwa pamoja.


Dar es Salaam. Serikali imesema imejipanga kuhakikisha wanafunzi wote watakaomaliza elimu ya msingi mwaka 2027 wanajiunga na sekondari.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,  alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu  sera, mitalaa mipya na hatua mbalimbali za utekelezaji wake, huku  akibainisha kuwa vyote vimeanza kutumika mwaka 2024.

‘’Mwaka huo  2027 tutakuwa na double cohort ( madarasa mawili yanayomaliza  elimu ya msingi  na kuingia kidato cha kwanza), lazima wote waende sekondari. Hadi mwaka 2027 tutakuwa tumekamilisha miundombinu. Mmeona Rais Samia amekuwa akijenga miundombinu,’’ amesema Profesa Mkenda.

Kwa mujibu wa sera ya elimu toleo la  mwaka 2023 elimu ya msingi itakua miaka sita, hivyo mwaka 2027 wanafunzi wa darasa la tatu wanaosoma mtalaa mpya watamaliza shule sambamba na wenzao wanaosoma kwa mtalaa wa zamani ambao mwaka huo watamaliza darasa la saba.


Mtalaa mpya

Katika utekelezaji wa mtalaa huo mpya ambao Profesa Mkenda na wataalamu wa wizara hiyo wamesema umeshaanza kutumika,  kwa  elimu ya awali, darasa la kwanza na la tatu.

Pia umeanza kutumika sekondari ambapo kuna mikondo miwili; mkondo wa  amali na jumla. Mkondo wa elimu ya amali unajumuisha  masomo na mafunzo ya ujuzi wa kazi mbalimbali,  huku elimu ya  jumla ikijikita zaidi kwenye  taaluma.

Hata hivyo, amesema mkondo wa elimu ya amali kwa mwaka huu umeanza kutekelezwa na shule chache .Kwa sasa  zipo shule 96 ambapo 68 ni za binafsi na 28 za Serikali.

Amesema vibali vya kuanza mtaala huo wa amali vilitolewa katika shule hizo  baada ya  ofisi ya kamishna wa elimu  kujiridhisha kuwa zina miundombinu stahiki  katika utoaji wa elimu hiyo.

 “Tungependa kuona shule za sekondari mkondo wa  amali ni  nyingi hata zaidi ya nusu,  tunaziongeza kidogo kidogo na kwanza tuhakikisha ziko tayari kutoa elimu hiyo ikiwa na vifaa, walimu na miundombinu ya inayohitajika. ”amesema Profesa Mkenda.

Akizungumzia maeneo makuu ya  mabadiliko ya mtalaa huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba, amesema mkondo wa elimu ya amali unaruhusu unyumbufu, hivyo mwanafunzi aliyesoma elimu hiyo anaweza kurudi mkondo wa jumla,anapojiunga na kidato cha tano au kuendelea na mafunzo ya ufundi sanifu.

‘’ Mwanafunzi katika mkondo huu anajifunza masomo ya fani yanayotolewa kwa kutumia mtaala wa VETA na kupimwa na NACTVET pamoja na masomo ya taaluma yanayotolewa kwa kutumia mtaala wa TET na kupimwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), amesema.

Kuhusu mkondo wa jumla, amesema  umejikita kwenye masomo ya kitaaluma na utakuwa na michepuo 11 ambayo ni: sayansi, kilimo, michezo, Tehama, biashara, muziki, sayansi ya jamii, sanaa, upishi, ushoni na lugha.

Kuhusu mtalaa kwa walimu, Dk Aneth amesema: ‘’Mtaala umejikita kuimarisha umahiri na weledi kwa wahitimu wote wa programu za ualimu. ‘’

Aidha ameongeza kuwa watafanya kazi kwa vitendo chini ya uangalizi  wa walimu wazoefu kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla hawajapewa leseni ya kufundisha.

Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amepongeza wizara kwa hatua hiyo ya kutoa elimu kwa Wahariri huku akiahidi kuwa vyombo vya habari vitaendelea  kuisemea sera na mitaala ili   jamii iweze kupata taarifa na elimu.

“Kumekuwa na tatizo la upotoshaji na kuizungumzia vibaya elimu yetu sasa tubadili mtazamo.Mitalaa ni mizuri tuendelee kushirikiana kuisemea vizuri ajenda hii... ‘’ amesema.