Kiteto waonja adha ‘uhaba’ wa petrol, yauzwa Sh5,000 kwa lita mtaani

Muuza petroli akisubiri wateja wilayani Kiteto

Muktasari:

  • Uhaba wa mafuta uliodaiwa kujitokeza maeneo mengi hapa nchini umetajwa kuathiri wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini wilayani Kiteto. Awali lita moja iliuzwa Sh3,330 na sasa inauzwa Sh5,000 kwenye ‘vibobo’ mitaani

Kiteto. Uhaba wa mafuta uliodaiwa kujitokeza maeneo mengi hapa nchini umetajwa kuathiri wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini wilayani Kiteto.

Wakizungunza na Mwananchi Digital baadhi ya wananchi leo Alhamisi Julai 3, 2023 wamesema kwa sasa wanaathirika kwa kukosekana mafuta hayo kwenye vituo vya mafuta.

"Biashara ya mafuta ya petroli inafanywa na madereva wa bodaboda ambao wao wanaenda wilaya za jirani ambazo ni Kongwa na Chemba mkoani Dodoma kuchukua nishati hiyo na kuja kuuza huku Kiteto," amesema Mussa Jamal ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Amesema hakuna kituo cha mafuta Kibaya kinachouza sasa mafuta aina ya petroli kati ya vituo vinne vilivyopo mjini Kibaya Kiteto hivyo wanaosaidia kupatikana nishati hiyo ni bodaboda ambao wanauza bei ya juu.

"Mafuta tunatoa eneo la Mjiro iliyopo wilaya ya Chemba km 49 na awali tulitoa Dabalo iliyopo wilaya ya Kongwa na kuja kuuza hapa kiteto kwa lita moja Shilingi elfu 5,000," amesema Hamisi Abrahamani dereva boda Kibaya.

"Pamoja na kazi ya boda ninayofanya ila kuuza mafuta ya vibobo inanipa faida kubwa sana. Napata faida mara mbili natamani kuacha sina hata haja ya kupiga tripu ya boda tena," amesema Abrahamani.

Nao baadhi ya wananchi wa mji wa Kibaya wamesema wanashindwa kufanya shughuli zao kwa wakati kutokana na kupanda kwa gharama hiyo ya mafuta ya petrol.

"Zamani nilikuwa nikienda shambani Porikwapori nilitumia Sh2,500 hadi elfu 3,000 na sasa nalazimika kutumia shilingi Sh6,000 mpaka Sh7,000 jambo ambalo ni gharama kubwa," amesema Thomas Njama.

Amesema hali hiyo imekuwa tatizo kubwa siyo kwake tu, bali kila kona kuna malalamiko na ni kilio ambacho hakina majibu na kuiomba Serikali kuingilia kati kwani mpaka sasa hakuna anayejua hatima ya tatizo hili.

"Naomba mama Rais Samia Suluhu Hassan afuatilie hili tupate majibu sahihi…tuliambiwa mafuta ni mengi na yanatosha, sasa kama yapo kwanini hayapatikani vituoni kila kitu sasa kimepanda vikiwemo vyakula," amesema Njama.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Kamati ya Usalama Kiteto ambaye hakutaka majina yake kutajwa, amesema wanaendelea kufuatilia tatizo hili ili ijulikane hatima yake.