Mfanyabiashara aliyedai kuhujumiwa na halmashauri,  achunguzwa

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Hamsini akizungumza na waandishi wa habari, HAWAPO PICHANI. 

Muktasari:

  • Kubainika kwa kampuni hiyo kumekuja baada ya hivi karibuni Chambulo kuibua tuhuma nzito za uhujumu uchumi dhidi ya halmashauri ya jiji la Arusha, akidai kuwa alilipa ushuru wa tozo ya huduma Sh24 milioni lakini anashangaa kupatiwa risiti iliyoandikwa amelipa Sh3.6 milioni.

Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha imeanza uchunguzi wa kampuni ya The Tanganyika Wilderness Camps Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara wa utalii, Wilbard Chambulo, iliyobainika kufanya kazi nchini bila kusajiliwa kwenye mfumo wa kodi wa Tausi.

Kampuni hiyo imebainika kufanya kazi za utalii hapa nchini hivi karibuni bila kusajiliwa katika mfumo wa Serikali wa Tausi, huku mauzo yake yakiwa hayafahamiki kwa ajili ya makadirio ya kodi.

Kubainika kwa kampuni hiyo kumekuja baada ya hivi karibuni Chambulo kuibua tuhuma nzito za uhujumu uchumi dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha akidai kuwa alilipa ushuru wa tozo ya huduma Sh24 milioni, lakini anashangaa kupatiwa risiti iliyoandikwa amelipa Sh3.6 milioni.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 19, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji hilo, Juma Hamsini amesema baada ya mfanyabiashara huyo kuibua tuhuma hizo, aliingia kwenye makabrasha ya ofisi kukagua fedha hizo.

Amesema walibaini kuwa fedha hizo zimelipwa kwa kampuni mbili tofauti zinazotumia usajili mmoja wa jiji, na Namba ya Mlipakodi (TIN) moja sambamba na kusajiliwa katika halmashauri moja.

“Chambulo alitaja kampuni yake ya Tanganyika Wilderness Camps Limited ambayo katika makabrasha tumeikuta imesajiliwa vema na imelipa Sh3.6 milioni kati ya Sh270.77 milioni iliyokuwa inadaiwa na sasa ana deni la Sh267 milioni, kutokana na mauzo yake kwa mwaka ambayo ni Sh90 bilioni,” amesema Hamsini.

Amesema kampuni hiyo anayozungumzia Chambulo ni tofauti na nyingine ya The Tanganyika Wilderness Camps Limited waliyoibaini ambayo  inatofautishwa na neno la awali la ‘The’ ambayo imelipa kodi ya Sh20.4 milioni.

“Kwanza, hii kampuni haijasajiliwa kwenye mfumo wa Tausi, lakini inaonekana imelipa Januari 19, 2023 Sh19.2 milioni na baadaye kulipa kidogo kidogo tena hadi kufikia Sh20.4 milioni kama kodi ya Julai hadi Desemba 2023,” amesema Hamsini.

Amesema kampuni hizo mbili tofauti zenye mkanganyiko wa majina, zinafanya kazi kila moja kivyake maeneo mbalimbali nchini na zimelipa fedha tofauti.

“Ukijumlisha hizi fedha zote ndio unapata Sh24 milioni, lakini kila moja inafanya kazi yake, hivyo tumeamua kama Serikali kuchunguza kampuni hii nyingine kwanza, mauzo yake ya mwaka na kodi yake ni kiasi gani lakini pia shughuli zake hasa ni zipi na eneo gani,” amesema.

Amesema hawana shida na kampuni ya awali anayoitambulisha Chambulo ya Tanganyika Wilderness Camps Limited dhidi ya mauzo na makadirio yake, bali wanamtaka kuhakikisha analipa kodi kwa mujibu wa deni analodaiwa huku akimtaka kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi dhidi ya kampuni ya The Tanganyika Wilderness Camps Limited,” amesema Hamsini.

Awali, Chambulo ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), katika  kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na wadau wa utalii kilichofanyika Aprili 13, 2024, alisema wamekuwa wakilipa kodi mbalimbali lakini hawampatii risiti stahiki wala kumbukumbu zao za malipo haziwekwi kwenye mfumo, hivyo akamtaka Makonda kuchunguza mara moja kwani upigaji huo unalenga kuichafua Serikali.