Mikopo kaushadamu ilivyotikisa bungeni, Serikali yatwishwa zigo

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aongoza kuhoji mawaziri wawili kuhusu riba kubwa.

Dodoma. Taarifa ya Serikali ya hoja ya mbunge kuhusu mikopo ‘kaushadamu’ imewaweka kitimoto mawaziri wawili, Bunge likiwapa muda wa kwenda kufanya kazi zaidi na kurejesha majibu upya.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson leo Alhamisi Mei 2, 2024 ndiye ameongoza kuwabana mawaziri, Dk Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) na Nape Nnauye (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), kuhusu riba kubwa na mikataba kati ya wakopeshaji na kampuni za simu.

Spika amewaagiza mawaziri hao kwenda kulifanyia kazi suala hilo kwa kuwa liko kwa mapana na wananchi wanaumia. Pia ameitaka Serikali kuangalia namna ya kupunguza riba kwa lengo la kuwasaidia wananchi.

Bunge limeipa Serikali muda wa hadi Septemba, 2024 kuwasilisha bungeni hatua za awali za utafiti na namna watakavyoanza kulifanyia kazi suala la mikopo hiyo, kabla ya kuwasilisha taarifa rasmi ya namna ya kutatua tatizo la mikopo ‘kaushadamu.’

Taarifa ya Serikali kuhusu hoja ya mikopo ‘kaushadamu’ imewasilishwa bungeni na Dk Nchemba baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Felista Njau kutaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa kuwa wananchi mitaani wanaadhirika kwa kusombewa mali zao wanapochelewa kulipa.

Hoja ya Njau iliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond, ambaye pia amezitaja taasisi za fedha zinazokopesha mikopo ya ‘chapchap’ kupitia Aplikesheni (App) kwenye simu.

Amesema taasisi hizo za fedha zinadhalilisha watu kwa kutuma ujumbe mbaya kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote ambao namba zao za simu ziko kwenye simu ya mkopaji.

“Wanatukanwa, wanadhalilishwa ndiyo maana tunasema kuna uhusiano kati ya taasisi hizi za ukopeshaji na kampuni za simu,” amesema.

Mbali ya Bunge kuvalia njuga mikopo hiyo yenye riba kubwa, gazeti la Mwananchi kwa nyakati tofauti limeandika habari kuhusu kaushadamu.

Dk Nchemba amesema wanaichukua hoja hiyo kwenda kuifanyia kazi na watakutana na wabunge wote kwa lengo la kujua changamoto wanazozipata wananchi kwa wakopeshaji wenye riba kubwa ambao wapo wenye leseni na wengine hawana.


Ngoma ilivyokuwa mjengoni

Awali, Dk Nchemba amelieleza Bunge hakuna kampuni ya simu yenye leseni ya kutoa mikopo kwa wananchi na kwamba kila taasisi inayotoa mkopo lazima iwe na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pia amesema hakuna mikopo ‘kaushadamu’ na hata alipoulizwa na Spika Dk Tulia kuhusu riba kubwa amesema inatokana na soko.

Spika akahoji kama riba inatokana na soko, kwa hiyo mtu yeyote mwenye fedha kijijini akiamua kukopeshwa watu kwa riba ya asilimia hadi 100, atakuwa hajatenda kosa lolote.


Moto wa riba

“Kwa mujibu wa Waziri (Dk Nchemba) ni kwamba kampuni za simu hazitoi mikopo. Kama nimeelewa sawasawa, ni benki zinatoa kupitia simu, nimeelewa sawasawa?” amehoji Spika.

Waziri Nchemba amesema kampuni za simu hazina leseni za kutoa mikopo, ila wanachofanya wanakifanya kwa ushirikiano na benki zenye leseni ya kutoa mikopo.

Spika amehoji, “Kama kampuni za simu hazina leseni za kutoa mikopo na wananchi hawaendi benki wanapata mikopo kupitia simu, maana yake mkataba upo kati ya benki na kampuni ya simu ambayo haina leseni, sasa huu mkataba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaukubalije? Kwamba wewe katoe mkopo wakati huna leseni.”

Dk Nchemba amesema, “Naomba niishie kwenye hiki kipengele cha kwanza mwenzangu anayesimamia mitandao (Waziri Nape) aeleze kwenye upande huo wa teknolojia.”

“Sisi tunachofanya kwa sababu mabenki yetu hayajaenda nchi nzima, kwa hiyo tunawarahisishia wananchi kwa kuruhusu benki kufanya kazi na mitandao ya simu. kumrahisishia mwananchi aweze kufikiwa kule kijijini,” amesema Nape.

Waziri Nape akijibu hoja ya Spika amesema kazi ya Tehama ni kuwezesha shughuli zingine zifanyike kwa namna ambayo bila Tehama ingekuwa ni ngumu.

“Ndiyo maana kwa mfano kupitia Tehama tunaweza kununua bidhaa mtandaoni.  Lakini, ‘platform’ (mitandao ya simu) hizi hazichukui leseni ya biashara,” amesema.

Nape amesema, “Hata ‘platform’ haichukui leseni ya  kutoa mikopo, kwa kuwa ni wawezeshaji wa kutoa huduma wanaenda kwa mtoa huduma wanaingia mkataba na mtoa huduma na kwa sababu hii ‘platform’ yao inatumiwa na mpokea huduma, wao wanakuwa katikati ni kama barabara kwamba, biashara inatoka huku inapita huku kwa hiyo leseni haiwezi kuchukuliwa na kampuni ya simu.”

Nape amesema kampuni ya simu haiwezi kufanya kazi ya kutoa mkopo ndiyo maana BoT inampa mwenye huduma mwenye leseni na inampa masharti ya kufanya hivyo.

Spika Dk Tulia amehoji, “Kwenye hiyo mikataba wanakubaliana mpaka riba. Riba ile ni ya benki au ni ya kampuni ya simu?”

Nape amesema, “Kama nilivyosema kampuni za simu haziwezi kufanya biashara ya mkopo, anayehusika na riba siyo kampuni ya simu, anayehusika na riba ni yule mwenye leseni ya kutoa mkopo, yeye ndiye amepewa masharti na BoT afuateje masharti, huyu ni mwezeshaji wa biashara tu.”

Spika amesema, “Nirejee kwa Waziri wa Fedha (Dk Nchemba), BoT ina mwongozo wowote kuhusu riba au benki inaamua kuanzia asilimia 0 ya mkopo mpaka asilima 100, yaani umekopa laki moja na utalipa laki. Kuna sharti lolote kutoka BoT au hakuna kwa hiyo benki inaweza kusema asilimia 80, asilimia 90 au 100 kuna mwongozo wowote au hakuna?”

Dk Nchemba amesema, “Masuala yoyote yanayohusiana na riba kuna sheria ambazo zinalinda walaji, lakini soko linaamua masuala ya riba, kwa mujibu wa sheria za kimataifa riba katika nchi ambazo zinafuata mfumo wa soko Benki Kuu haipangi riba kwamba kuanzia kesho riba za mabenki itakuwa asilimia tano, hatufanyi hivyo na taasisi za kifedha zinazosimamia mabenki.”

“Soko linaamua masuala ya riba, lakini kwa nchi yetu tuna taratibu za kuwalinda walaji, hapo ndiyo kuweka utawala wa riba ili kuweza kuwalinda walaji, kuna miongozo kuhusu namna ya kuwalinda walaji, kwa hiyo kuna sheria inayolinda walaji,” amesema.

Spika amehoji: “Je nitakuwa sahihi nikisema hivi nchi hii hatuna mikopo ‘kaushadamu’ kwa sababu hata BoT inajua soko linajiendesha lenyewe, nitakuwa niko sahihi?”

Dk Nchemba amesema, “Kisheria hatuna mikopo kaushadamu. Kaushadamu ni mimi naenda kuchukua fedha kwa Nape halafu nakaushiwa damu kufuatana na makabuliano niliyokubaliana na Nape, hii hata mwenyekiti wa kitongoji anakuwa hajui, ni mimi nimeenda.”

Spika amehoji, “Swali langu lilikuwa kwamba mimi kama mwenyekiti wa kitongoji ninazo fedha na naamua kukopesha kwa riba ya asilimia 100, sikosei popote kwa sababu hakuna sheria ninayokosea wala mwongozo wowote. Kama ambavyo benki pia inaruhusiwa kuanzia asilimia 0 mpaka 100, kwa hiyo iko sawa nimeelewa sawasawa?”

“Ukifanya hivyo, unakosea kwa sababu mikopo yoyote  inatawaliwa na sheria utakuwa huna leseni ya kufanya hivyo,” amesema Dk Nchemba.

Spika amehoji, “Kwa hiyo mwenye leseni kama benki asilimia yoyote anayotaka inaruhusiwa, isipokuwa huyu ambaye hana leseni ndio haruhusiwi nimeelewa vizuri? hoja ni leseni.”

Dk Nchemba amesema, “Hata mwenye leseni siyo asilimia yoyote lazima azingatie mwongozo, lakini wale wanaofanya ‘kaushadamu’ yale ni makubaliano ya kirafiki ambayo hayako kwenye utaratibu, ambalo ni kosa kisheria.”

“Kabla sijawaruhusu wabunge, Waziri (Dk Nchemba) sasa hapo umenichanganya kidogo, kwa sababu kama hakuna mwongozo maana yake hata mabenki yanaruhusiwa kutoza riba yoyote, kwa sababu si soko lipo, kwa sababu yenyewe yana leseni kwa hiyo riba ni yoyote,” amehoji Spika.

Waziri Nchemba amesema, “Ingekuwa hivyo kungekuwepo ‘fluctuation’ kubwa ya riba kwenye mabenki, lakini sasa ukiangalia kwenye mabenki kuna ‘range’ ambayo mabenki yanatumia na yanaenda kufuatana na mwongozo. Ingekuwa hivyo hata mabenki kungekuwa na ‘kaushadamu’.

Katika moja ya habari kuhusu mikopo kaushadamu iliyoandikwa na gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alikiri benki hiyo kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu mikopo hiyo, akisema kwa sasa wamechukua hatua ya kutoa elimu kwa wakopeshaji, halmashauri kupitia Ofisi ya Rais (Tamisemi) na wakopaji.

Alitaja makundi manne ya mikopo, akieleza midogo ipo kundi la pili na la kwanza ni ya benki.

Kundi la tatu ni la vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) na la nne ni la vikundi vya kijamii (Vicoba).

“Ni kweli tumesikia hayo malalamiko ya wakopeshaji na wengine wanaita mikopo kaushadamu na wengine mikopoumiza. Sheria yetu imetungwa mwaka 2018, lakini mikopo imekuwepo miaka mingi kabla hata Yesu Kristo hajazaliwa, ndiyo maana utasikia huyu alipewa talanta akazizika chini ya ardhi na mengineyo,” alisema.

“Sisi Benki Kuu tumekuwa tukitoa elimu, kwanza kwa wakopeshaji kukata leseni na pia waweke wazi masharti na vigezo vyao. Halafu hivyo vigezo visiwe vigumu kwa wakopaji, hata kama tuko kwenye uchumi wa soko huria, visilete taharuki,” alisema Tutuba.