Mwakinyo aitwa mahakamani, aomba siku 21 kujiandaa

Bondia Hassan Mwakinyo

Muktasari:

  • Bondia Hassan Mwakinyo Mwakinyo amefunguliwa kesi na kampuni ya kampuni ya PAF Promotion, ikimtaka bondia huyo kuilipa Sh150 milion kwa kampuni hiyo ikiwa ni madhara waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.

Dar es Salaam. Bondia maarufu nchini, Hassan Mwakinyo, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu impe siku 21 ili ajiandae majibu kuhusu kesi ya madai alivyofungukiwa na Kampuni ya PAF Promotion.

Mwakinyo kupitia wakili wake, Azadi Athumani ametoa ombi hilo, leo Novemba 20, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi, baada ya kuitikia wito wa Mahakama.

Katika kesi hiyo ya madai namba 227/2023, kampuni ya PAF Promotion imewasilisha madai nane, likiwemo la kumtaka bondi huyo kuilipa Sh150 milion ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.

Kampuni hiyo imemfungulia Mwakinyo kesi hiyo baada ya kushindwa kupanda ulingoni katika pambano lililoandaliwa na kampuni hiyo,  lililopangwa kufanyika Septemba 29, 2023 jiji hapa; kwa kile alichonukuliwa akisema ni waratibu hao kukiuka masharti ya makubaliano.

Novemba 13, 2023 Mahakama hiyo ilielekeza wito upelekwe kwa bondia huyo kupitia gazeti la Mwananchi ili afike mahakamani, baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito wa kufika mahakamani iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.


Awali, Wakili anayewakilisha kampuni hiyo ya PAF Promotion, Herry Kauki amedai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama taarifa ya wito iliyotolewa kwenye gazeti la Mwananchi imemfikia Mwakinyo.

Wakili Kauki amesema kuwa wamepata taarifa kuwa taarifa imemfikia Mwakinyo na tayari ametuma wakili wake mahakamani hapo.

Kauki baada ya kueleza hayo, ndipo mahakaka ilipompa nafasi wakili wa Athuman.

Katika maelezo yake, wakili Athuman kutoka Kampuni ya uwakili ya Cosmic Attorneys, amedai kuwa taarifa ya wito wameipata na ndio maana leo amekuja mahakamani.

Athuman amedai kutokana na hoja zilizotolewa na wadai, anaomba mahakama impe siku 21 ili aweze kuja kujibu hoja zilizowasilishwa na Kampuni ya PAP Promotion.

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alikubaliana na ombi la Mwakinyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11, 2023 itakapotajwa.

Nje ya mahakama

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, nje ya mahakama wakili wa Mwakinyo na wakili wa PAF Promotion walikutana na kujadiliana na kwa pamoja wamekubaliana kufanya usuluhishi nje ya mahakama.

"Kama majadiliano yatakwenda vizuri, tutaifahamisha mahakama na tarehe ijayo ya kutajwa kwa kesi, tunaweza kuiondoa kesi hii mahakamani na kuisikiliza nje ya mahakama," amesema Kauki.

Madai ya PAF Promotion

Kwa mujibu wa hati ya madai, kampuni hiyo inaiomba Mahakama, kwanza itamke kwamba bondia huyo amevunja mkataba wa kupigana.


Pili inaomba Mahakama kumtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kuichafua kutokana na kutoa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari alivyotumia kuichafua kampuni na Wakurugenzi wake.

Tatu, PAF inaomba ilipwe fidia ya Sh 142.5 milioni kutokana na hasara ya kukosa mapato iliyotegemea kutoka kwa wadhamini.

Nne, inaomba Mahakama imwamuru Mwakinyo arejeshe dola 3,000 (Sh 7.51 milioni) alizopewa kuelekea pambano hilo alilotakiwa kupigana.

Tano, PAF inaomba kurejeshewa Sh8 milioni yakiwa ni malipo ya kulipia ukumbi.

Sita, inaomba kurejeshewa zaidi ya Sh1.28 milioni ikiwa ni gharama za malazi ya mpinzani wa bondia huyo.

Saba, kampuni hiyo, inaomba Mwakinyo kurejeshewa zaidi ya Sh3.83 milioni ambazo ni gharama za tiketi za ndege za mpinzani wake pamoja na wasaidizi wake.

Nane, PAF inaomba Mwakinyo kuilipa kampuni hiyo jumla ya Sh 150milioni ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.