Serikali yafunga mjadala wa mafao ya wastaafu EAC

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju ambaye alisema Mahakama ya Rufaa ilishamaliza kazi yake, hivyo hakuna tena mlango wa wastaafu hao kupitia.

Dodoma. Serikali imefunga rasmi mjadala kuhusu mafao ya wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika ikisema hawawezi kupata chochote na hawawezi kwenda mahakama yoyote.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju ambaye alisema Mahakama ya Rufaa ilishamaliza kazi yake, hivyo hakuna tena mlango wa wastaafu hao kupitia.

Mwanasheria huyo alisema wakati Serikali ikimaliza kulipa madeni kwa wastaafu hao, wapo wengine ambao walifungua kesi namba 73/2015 kwenye Mahakama ya Rufaa ambayo yalitupiliwa mbali, hivyo hawana mahali pengine pa kukimbilia.

Masaju alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Faida Bakari ambaye alipinga kauli ya awali ya Serikali kwamba malipo ya wastaafu hao yalishafanyika.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu Susan Mgonukulima (Chadema) alitaka kujua kama Serikali imeshalipa stahiki za wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika Juni 1977.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali ilishalipa stahiki za wastaafu. Alisema kati ya 2005 - 2010, Serikali iliwalipa wastaafu 31,519 kati ya 31,831 ambao walilipwa jumla ya Sh115.3 bilioni na kuwa waliolipwa ni wale waliojitokeza na kuthibitishwa na waliokuwa waajiri wao.

“Aidha, katika kipindi cha 2011 – 2013 Serikali iliendelea kuwalipa wale ambao walikuwa hawajalipwa ambapo wastaafu 269 walilipwa Sh1.58 bilioni na kufanya jumla ya waliolipwa kufikia 31,788 hivyo kiasi kilicholipwa kufikia Sh116.88 bilioni,” alisema Dk Mpango.

Alisema upokeaji madai mapya ulisitishwa Desemba 31, 2013 kwa mujibu wa makubaliano kati ya wawakilishi wa wastaafu na wanasheria wao kwa upande mmoja na Serikali kwa upande wa pili. Baada ya majibu hayo, Bakari katika swali la nyongeza alisema si kweli kwamba wazee walilipwa wote na anao ushahidi, hivyo akahoji kwa nini Serikali ifunge suala hilo, ndipo Masaju akajibu kwamba suala hilo limekwisha na hawana popote pa kwenda.