Simulizi mchunga mifugo alivyomteka mtoto kulipwa pesa, akafungwa mwingine

Muktasari:

  • Mchunga mifugo alimteka mtoto akaomba fedha kwa wazazi wake kisha Mahakama ya Wilaya ya Missenyi ikahukumu kifungo mtu ambaye mtoto huyo alikutwa kwake, lakini Mahakama Kuu imemuachia huru baada ya Serikali kumtetea kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kesi dhidi yake.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba imuachia huru mkazi wa kijiji cha Bubale wilayani Misenyi mkoani Kagera, Amon Ngwandamo maarufu Masumbufu aliyekuwa amefungwa jela miaka mitano kwa kosa la kumteka mtoto mwenye umri wa miaka minne na kujipatia pesa kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo.

Mahakama hiyo imemwachia huru Masumbufu kufuatia rufaa aliyoikata akipinga hukumu hiyo iliyomtiani hatiani kwa kosa hilo na kumhukumu adhabu hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shitaka dhidi yake, rufaa ambayo pia iliungwa mkono na Serikali.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 30, 2024 na Jaji Immaculate Banzi aliyesikiliza rufaa hiyo.

Mbali na hukumu hiyo kumwachilia huru mfungwa huyo, jambo lenye upekee ni simulizi ya namna mtoto huyo alivyotekwa, lengo la utekaji huo na jinsi Masumbufu alivyotiwa hatiani na kuhukumiwa kwenda jela na kuachiwa kwake.


Jinsi ilibvyokuwa

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, simulizi hiyo inaanzia asubuhi ya Machi 28, 2023, katika kijiji cha Bubale wilayani Misenyi mkoani Kagera, ambapo mama mzazi wa mtoto huyo alimuandaa mtoto huyo kisha akaenda shuleni yeye na dada yake.

Hata hivyo, muda wa saa 5:00 asubuhi dada wa mtoto huyo alirejea nyumbani na akamweleza mama yao (ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo) kwamba mdogo wake ametekwa na mchunga mifugo, aliyemtaja kwa jina moja la Edson.

Hivyo mama huyo aliwajulisha majirani na msako ukaanza, lakini siku hiyohiyo Edson alimpigia simu baba wa mtoto huyo, Thadeo Rwabusagara (shahidi wa nne), akihitaji pesa kiasi cha Sh15 milioni (ili kumkomboa mtoto huyo. Hata hivyo, baada ya majadiliano walikubaliana malipo ya Sh5 milioni.

Machi 30, 2023, baba wa mtoto huyo alimtuma mtu mwingine (shahidi wa pili) kwenda mahali alikokuwa ameelekezwa na Edson (mtekaji), akiwa na Sh1 milioni kwenye begi.

Alipofika kwenye kizuizi cha Kagera Sugar, aliweka begi lile chini barabarani kama alivyoelekezwa, kisha mtu mmoja, ambaye kwa mujibu wa shahidi huyo alikuwa mfupi, alilichukua begi hilo na kuondoka.

Aprili 2, 2023, Edson alimpigia simu tena baba wa mtoto huyo na akamweleza mtoto wake alikuwa katika msitu wa Bashenyi. Hivyo wanakijiji akiwemo shahidi wa tano, walikwenda katika msituni lakini hawakumpata.

Baadaye Edson alimpigia simu tena baba wa mtoto akamweleza mtoto wake alikuwa kwa Amon Masumbufu, aliyefungwa kwa kosa hilo na ambaye sasa ameachiwa).

Hivyo wanakijiji hao walikwenda tena huko ambako walianza kutafuta katika nyumba za watu wanaoishi huko na katikati ya shamba moja la mahindi waliona kibanda na walipokikaribia kibanda hicho mtu mmoja alitoka akakimbia.

Halafu Amon (Masumbufu) alitoka nje na wanakijiji waliingia ndani ya kibanda hicho wakamkuta mtoto huyo na wakamkamata.

Aprili 12, 2023 lilifanyika gwaride la utambuzi (wa mtuhumiwa wa uhalifu huo) lililoendeshwa na shahidi wa sita (askari polisi) ambapo, shahidi wa pili aliweza kumtambua Masumbufu kuwa mtu aliyechukua pesa alizotumwa na baba wa mtoto huyo kuzipeleka mahali, Machi 30, 2023 ndani ya begi.


Mashtaka yalivyoendeshwa

Hivyo, Masumbufu alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Misenyi yeye na wenzake wenzake watano, ambako walisomewa shtaka la utekaji wa mtoto kwa nia ya kuiba kinyume cha kifungu cha 252 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Iliyorejewa mwaka 2022.

Walidaiwa Machi 28, 2023, katika kijiji cha Bubale, wilayani Misenyi, mkoani Kagera, walimteka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 4 kwa kusudi la kujipatia pesa kiasi cha Sh15 miloni kutoka kwa Thadeo Rwabusagara (baba wa mtoto huyo).


Utetezi

Walikana shtaka hilo na katika utetezi wao, Masumbufu alikana kutenda kosa hilo, akieleza Aprili 2, 2023, alimuona mtoto shambani mwake na kwamba alimjulisha mjumbe wa nyumba 10, ambaye alimweleza kuwa asiondoke (yeye Masumbufu) nyumbani kwake.

Alidai muda mfupi baadaye alivamiwa na kundi la watu ambao walimtia mbaroni.

Ushahidi wake uliungwa mkono na shahidi wa pili wa utetezi (kiongozi wake, mjumbe wa nyumba 10) ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa Aprili 2, 2023 Masumbufu alimpigia simu akamweleza kuwa alimuona mtoto akiwa na sare za shule shambani mwake.

Shahidi huyo mjumbe alidai kuwa wakati alipokwenda shambani kwa Masumbufu alikuta tayari mtoto huyo akiwa ameshachukuliwa na askari Polisi.


Hukumu, adhabu na rufaa

Hata hivyo, mahakama hiyo baada ya kukamilisha usikilizaji wa kesi hiyo iliwaachilia huru washtakwa wengine watano, lakini ikamtia hatiani Masumbufu peke yake ndipo ikamhukumu adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela.

Masumbufu hakukubaliana na hukumu hiyo hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu kuipinga huku akitoa sababu nne zilizojikita kuonyesha upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka dhidi yake bila kuacha mashaka yoyote.

Siku ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, Masumbufu alijiwakilisha mwenyewe bila kuwa na wakili huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Erick Mabagala.

Kwa kuwa hakuwa na uelewa wa masuala ya kisheria, Masumbufu hakuwa na cha kusema badala yake aliiomba mahakama izingatie tu sababu zake za rufaa kama alivyoziwasilisha kwa maandishi na imwachilie huru.


Serikali ilivyomtetea

Hata hivyo, wakili Mabagala kwa upande wake aliieleza mahakama hiyo kuwa anaunga mkono rufaa hiyo huku akidai upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka dhidi yake.

Wakili Mabagala alifafanua ushahidi wa shahidi wa kwanza, wa pili na wa tatu wa upande wa mashtaka unaonesha mtoto huyo alitekwa na Edson.

Hata hivyo, alieleza kuwa Edson hakuwahi kukamatwa badala yake alikamatwa mdogo wake, aliyekuwa mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi ambaye baadaye aliachiwa na Mahakama kwa kutokuwa na hatia.

“Shahidi wa saba na wa tisa ambao walikuwa askari Polisi hawakueleza sababu za kushindwa kumkamata Edson. Kushindwa kumkamata Edson, ambaye alitajwa na mashahidi wote kama ndiye mtekaji kunaacha shaka kubwa kwa kesi ya upande wa mashtaka,” alieleza Wakili Mabagala.

“Ukweli kwamba mwathirika (mtoto huyo) alikutwa katika moja ya nyumba za mrufuni (Masumbufu) si uthibitisho na hitimisho kwamba mrufani alikuwa mtekaji.”

Pia, Wakili Mabagala alieleza shahidi aliyedai kumtambua Masumbufu kwenye gwaride la utambuzi (kuwa ndiye aliyechukua pesa alizotumwa kuzipeleka), hakutoa maelezo ya utambulisho wa Masumbufu kabla ya kumtambua kwenye gwaride la utambuzi.

Vilevile alieleza shahidi huyo mtambuzi hakueleza alikuwa umbali gani naye na alitumia muda gani kumchunguza (wakati akichukua begi la pesa kama alivyodai).

Wakili Mabagala pia alieleza gwaride la utambuzi lilikiuka masharti ya Muongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi (Police General Order – PGO) ya 232, kwa kutokumweleza mrufani huyo kusudi la gwaride, haki ya kuwa na mwanasheria, ndugu au rafiki.

Aliongeza kulikuwa na uchelewaji usioelezeka wa kuendesha gwaride hilo baada ya kukamatwa na kwamba, kasoro hizo zinalifanya gwaride hilo la utambuzi thamani yake kupungua.

Alihitimisha kwa kuiomba mahakama hiyo iikubali rufaa hiyo kwa kuwa kesi dhidi ya mrufani (Masumbufu) haikuweza kuthibitishwa bila kuacha mashaka yoyote.


Uamuzi wa Mahakama

Jaji Banzi baada ya kuzingatia sababu za rufaa alizoziwasilisha Masumbufu pamoja na hoja za wakili wa Serikali kuhusiana na ushahidi uliowasilisha, katika uamuzi wake amekubaliana na sababu hizo za rufaa na hoja wakili wa Serikali, Mabagala.

Amesema ni jambo lisilobishaniwa kuwa mtu aliyekuwa na mtoto huyo wakati anadaiwa kutekwa kwake (dada yake) alimweleza mama yao kwamba, mtoto huyo alitekwa na Edson na kwamba kama alivyoeleza wakili wa Serikali, Edson hakukamatwa.

“Mbaya zaidi hakuna hata mmoja miongoni ma mashahidi wa upande wa mashtaka aliyeeleza uhusiano baina ya Edson na mrufani, (Masumbufu)”, amesema Jaji Banzi na kuongeza kuwa pia ushahidi wa shahidi wa pili kuhusiana na gwaride la utambuzi (wa mtuhumiwa) unaacha shaka kubwa .

Jaji Banzi amesema pia hakuna shaka kuwa mrufani alikuwa ni mgeni kwa shahidi huyo wa pili na kwamba, Mahakama ya Rufani ilishaweka msimamo kuwa shahidi anapomuona mtuhumiwa eneo la tukio kwa mara ya kwanza anapaswa atoe maelezo ya utambulisho wa mtuhumiwa aliyemuona.

Amefafanua utambulisho huo ni pamoja na mwonekano, rangi, kimo na alama yoyote ya pekee na kwamba, katika kesi hiyo shahidi huyo alieleza tu kuwa alikuwa mfupi, akieleza kuwa ni maelezo ya jumla ambayo si lazima yawe yanamhusu mrufani tu.

Pia amesema kuwa polisi hakuna mahali walikoeleza kama walimpa haki zake mtuhumiwa wakati wa gwaride la utambuzi wala hawakueleza sababu za kuchelewa kuandaa gwaride hilo na kwamba, kasoro hizo zilifanya lisiaminike na haliwezi kuunga mkono ushahidi wa shahidi wa pili.

Amesema maelezo kwamba mwathirika (mtoto huyo) alikutwa katika nyumba ya mrufani si uthibitisho hitimisho kuwa ni mrufani aliyemteka, kwa kuzingatia kuwa aliripoti kwa mjumbe (mtoto huyo kuonekana shambani kwake).

“Itakumbukwa kuwa kwa mujibu wa shahidi wa tano baada ya kufika katika kibanda cha mrufani kuna mtu alikimbia. Hii inaonesha kuwa kuna uwezekano kwamba, mtu aliyekimbia ndiye mtekaji wa mwathirika (mtoto) na alimpeka kwenye kibanda cha mrufani,” amesema Jaji Banzi.

Amesema kwa kuzingatia kasoro zilizotajwa hapo ni dhahiri upande wa mashtaka ulishindwa kutimiza wajibu wake wa kuthibitisha kesi dhidi ya mrufani bila kuachama shaka yoyote.

"Hivyo ninaamua kuwa rufaa ina ustahilifu. Ninaikubali kwa kutengua hatia na kutupilia mbali adhabu iliyotolewa kwa mrufani. Niaamuru aachiliwe mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama ataendelea kushikiliwa kihalali kwa sababu nyingine,” amehitimisha Jaji Banzi.