Siri mvutano wa bajaji, daladala ukiota mizizi

Bajaji zikisubiri abiria katika eneo la Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Picha na Mtandao

Dar/Mikoani. Licha ya kutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi, pikipiki za magurudumu matatu maarufu kama bajaji, zimekuwa chanzo cha mivutano na watoa huduma wengine wa usafiri wa umma ‘daladala’, huku abiria wakiathirika kutokana na migomo inayoibuka.

Miongoni mwa mivutano iliyoshuhudiwa hivi karibuni kati ya madereva wa bajaji na daladala ilitokea katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Arusha, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ikitoa ufafanuzi wa kinachopaswa kufanyika.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Jafar Kismart alisema miongoni mwa vyanzo vya mgogoro ni bajaji kufanya biashara sawa na daladala kwa kupakia abiria vituoni badala ya kuwepo maeneo maalumu waliyotengewa.

Alisema kinachofanywa na madereva wa bajaji ni ukiukaji wa sheria na kanuni za leseni zao.

“Hatulalamiki tu kukosa abiria, lakini kitendo kinachofanywa ni hatari, kwani wakati mwingine wanajaza abiria kupita kiasi. Pia hata njia wanazopita ni hatari kwa usalama wao na abiria.

“Usione watu wananyamaza, jambo hili halijaanza leo, linatuathiri na ni hatari. Kwenye sekta ya usafirishaji, bado kuna matatizo makubwa, tangu nchi imepata Uhuru hakuna kiongozi mkubwa aliyetuita, jambo linalochangia matatizo kuongezeka,” alisema Kismart.

Licha ya kuilalamikia Latra kwa kushindwa kuchukua hatua, Kismart pia analilaumu Jeshi la Polisi, Kiosi cha Usalama Barabarani.

“Kweli kuna njia magari hayatoshi, lakini isiwe sababu ya kuziacha bajaji kuvunja sheria, haya yote yanatokana na kuwepo urasimu kwenye utoaji vibali kwa baadhi ya njia,” alisema.

Miongoni mwa njia ambazo bajaji zimekuwa zikifanya safari sawa na daladala kwa kuchukua abiria vituoni jijini Dar es Salaam ni kutoka Mwenge kwenda Mbezi, ambako nauli kutoka kituo kimoja hadi kingine abiria hutozwa Sh500. Kwa anayeanza safari Mwenge hadi Mbezi hutozwa Sh2,000.

Akizungumzi suala hilo, Mkurugenzi wa udhibiti wa barabara kutoka Latra, Johansen Kahatano alisema kwa mujibu wa sheria, bajaji inapaswa kuegeshwa au kupakia kwenye kituo ilikosajiliwa kufanya kazi.

Alibainisha kuwa bajaji ni kama teksi, hivyo hairuhusiwi kupakia kama daladala, akieleza mamlaka hiyo imekuwa ikiwachukulia hatua, ikiwemo kuwakamata.

“Tumekuwa tukiwaelimisha na kuwachukulia hatua wale wanaobainika wamevunja sheria, ambaye anakamatwa faini yake si chini ya Sh25,000,” alisema Kahatano.

Hali ilivyo sasa

Kutokana na vurugu zilizoibuka juzi jijini Arusha, Latra imesitisha uhakiki wa bajaji ndani ya jiji hilo uliokuwa ufanyike kuanzia Alhamisi Agosti 3 hadi 5 mwaka huu.

Awali, Latra ilitangaza kufanya uhakiki huo ikieleza bajaji zimekuwa nyingi tofauti na idadi ya walizokatia leseni.

“Bajaji zenye leseni ndani ya Jiji la Arusha hazizidi 350, lakini zilizopo ni zaidi ya 2,000, hali ambayo imekuwa kero, kwani wanatoa huduma ambayo inaingiliana na daladala," alisema ofisa mfawidhi wa Latra Mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela.

Alisema kutokana na hilo, walisitisha utoaji leseni na kuzitaka bajaji ambazo hazina kuhamia maeneo mengine nje ya jiji hilo ili kupata kibali, lakini waligoma.

“Tuliwaita tufanye uhakiki, lakini wamekuja kama shari, tuliomalizana nao tunawaruhusu kuendelea na ratiba hawataki, tena mbaya zaidi wanazuia wengine ambao wanaendelea na kazi na mwisho wanafunga barabara na wanaleta fujo na kelele.

“Hivyo, tumeamua kusitisha kwa leo hadi tutafute eneo lingine na kubwa zaidi tutawatangazia," alisema Mwakalebela, alipozungumza na madereva hao jana.

Dereva wa bajaji, Khamis Abbas alisema wamesikitishwa na utaratibu wa Latra, akidai wananyanyaswa, ikiwemo kukamata bajaji na kuwatoza faini kila kukicha, huku wakifukuzwa kufanya kazi ndani ya Jiji.

Naye, Abdul Omary alisema anafanya safari kati ya Uswahilini na Dampo, lakini bajaji yake ilikamatwa wiki iliyopita na alipofuatilia alitakiwa kujaza fomu ikimtaka kuhamia nje ya mji.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella akizungumzia suala hilo, alisema analishughulikia.

“Hilo si jambo kubwa kama mnavyotaka kulichukulia, naenda kushughulika nalo, naamini litaisha salama,” alisema Mongella.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha bajaji Mkoa wa Iringa, Melab Kiwele aliitaka Serikali kufuata utaratibu wa kisheria juu ya madereva wa bajaji wanaokwenda kinyume cha utaratibu wa matumizi ya barabara wanazotakiwa kuzitumia.

Melab alisema kwa kuwa utaratibu wa matumizi ya njia kwa vyombo hivyo vya usafiri ulitolewa na kila dereva anauelewa, wanaokiuka wachukuliwe hatua za kisheria kama inavyotakiwa.

“Kama maelekezo alitoa mkuu wa mkoa kwamba kila mtu afuate utaratibu wake na sisi kama viongozi wa bajaji tunasimamia hapo kila mtu afuate utaratibu, hatuna neno zuri zaidi ya kusema watu wafuate utaratibu,” alisema.

Aprili, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alikutana na wamiliki na madereva bajaji, kamanda wa Polisi na mkuu wa usalama barabarani mkoani humo kujadili suala la bajaji na daladala kwa ajili ya kufikia muafaka.

Baadhi ya yaliyoafikiwa na mkuu wa mkoa ni kurekebisha matuta yaliyokuwa yakidaiwa kuwa kero kwa bajaji pamoja abiria na suala hilo lilitekelezwa kama ilivyotakiwa.

Licha ya marekebisho hayo, bado bajaji zimeendelea kutumia barabara zilizopigwa marufuku awali.

Kwa sasa hali ya usafiri wa daladala Manispaa ya Iringa unadaiwa kuzorota kwa kubakia magari machache, ikidaiwa kuwa usafiri wa bajaji umeua biashara ya daladala.

Mkoani Mbeya, mwenyekiti wa madereva wa bajaji jijini humo, Fesfo Mwasimba alisema suala la mgogoro kati yao na daladala kwa mwaka huu halijatokea tofauti na mwaka jana, kwa kuwa kuna utaratibu wamejiwekea na mipaka ya njia za kupita kusafirisha abiria.

“Kwa mwaka jana kuna migogoro mikubwa ilitokea na kusababisha mgomo wa madereva wa daladala, lakini kuna baadhi ya madereva wa bajaji katika njia za pembezoni wamekuwa wakikiuka sheria ambao tunaendelea kuwafuatilia,” alisema Mwasimba.

Imeandikwa na Fortune Francis (Dar), Bertha Ismail (Arusha), Hawa Mathias (Mbeya) na Ahazi Mvela (Iringa)