Suala la ndoa kuvunjika latinga tena bungeni

Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk David Mathayo David akizungumza wakati akiuliza swali kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Ijumaa Aprili 19, 2024 jijini Dodoma.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

S  Mbunge ataka wananchi kuelimishwa, kuwapa elimu watoto wa kiume jinsi ya kuwa baba pindi watakapooa.

Dodoma. Mbunge wa Same Magharibi, Dk David Mathayo amehoji Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa Watanzania kuonyesha umuhimu wa watoto kulelewa na wazazi wawili, kutokana na ndoa nyingi kuvunjika.

Dk Mathayo amehoji hayo katika swali la nyongeza leo Ijumaa Aprili 19, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.

Amesema siku hizi ndoa zimekuwa zikivunjika na watu wamekuwa wakiachana, jambo linalochangia kuwapo kwa watoto wasiolelewa na wazazi.

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kwenda kutoa elimu kwa Watanzania hasa kuonyesha majukumu ya wanawake na wanaume katika ndoa, ili watoto waweze kulelewa na wazazi wote wawili,” amehoji.

Pia amesema kwa miaka mingi kumekuwa na kampeni ya kuelimisha na kuwezesha mtoto wa kike na kuwasahau wa kiume.

“Serikali ina mkakati gani wa kuwapa upendeleo maalumu watoto wa kiume ili waweze kupata elimu nzuri, kujiamini ili baadaye waweze kuoa wanawake waliosoma,” amesema.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis akijibu swali hilo, amesema Serikali kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inatoa haki sawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume wakiwemo wenye ulemavu.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kujenga madarasa kila mkoa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu na waweze kufikia malengo waliyokusudia,” amesema.

Amesema Sera ya Wanawake ya mwaka 2023 inatambua ushiriki wa wanawake na wanaume kuwa wakala muhimu wa kuleta mabadiliko ya kuimarisha maendeleo na familia nchini.

Katika swali la msingi, Dk Mathayo amehoji kuna mpango gani wa kumwelimisha mtoto wa kiume kujitegemea, kujiamini na kufahamu majukumu ya baba wa familia pindi atakapooa.

Naibu waziri amesema wizara imeandaa mwongozo wa wajibu wa wazazi katika malezi ya watoto kwa kuzingatia jinsi ambao unajulikana ‘Familia bora, Taifa imara’ wenye lengo la kuimarisha ushiriki wa wazazi na walezi katika malezi ya watoto.

Amesema eneo moja lililoainishwa katika mwongozo huo ni kumuandaa mtoto wa kiume ili aweze kumudu majukumu ya baba katika nyanja tofauti, ikiwa ni pamoja na kutambua wajibu na nafasi katika malezi ya watoto na familia.

Kasi ya kuvunjika ndoa iliwahi kuzungumzwa bungeni Septemba 5, mwaka 2023.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilieleza kushtushwa na kasi ya kuvunjika kwa ndoa nchini.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, chanzo kikubwa ni mmomonyoko wa maadili, Mkoa wa Dar es Salaam pekee ndoa zaidi ya 300 zilielezwa kuvunjika kwa mwezi.