Wabunge wataka hatua za ziada kudhibiti tembo

Muktasari:

Serikali yaeleza hatua inazochukua kudhibiti tembo kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara ikiwemo vifo na kuharibu mazao shambani.

Dodoma. Wabunge wametaka mikakati ya ziada kukabiliana na tembo wanaovamia maeneo ya makazi, ikiwamo kuwavuna wanyama hao.

Hatua hiyo ilitokana na maelekezo yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo kutoa hoja bungeni kuhusu wanyama hao Aprili 30, 2024.

Mbunge huyo amesema tembo waliingia katika makazi ya watu na kusababisha shughuli za kiuchumi na kijamii kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu.

Dk Tulia aliitaka Serikali kutoa majibu kuhusu hatua walizochukua kushughulikia changamoto ya wanyamapori katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na maeneo mengine nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki, amesema wizara imeendelea kuchukua hatua, ikiwamo mkakati wa utatuzi wa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu ambao ni wa miaka mitatu.

Hatua nyingine ni mkakati wa kusimamia na kuhifadhi tembo ambao ni wa miaka 10 na mpango kazi wa kuongoa shoroba 61.

Amesema wanaendelea kufanya doria ya wanyama waharibifu, wakiwamo tembo. Pia wamejenga vituo 154 vya ofisi za kanda kuimarisha shughuli za udhibiti.

Amesema wamejenga vituo vya askari wanyamapori 16 kwa mwaka 2022/23, lakini kwa mwaka 2023/24 wamejenga vituo 15. Pia  wametoa mafunzo ya mbinu rafiki kwa ajili ya kukabiliana na wanyapori waharibifu.

Amesema wametoa mafunzo kwa wakufunzi 1,626 katika wilaya 44 ambazo zina changamoto kubwa ya wanyamapori.

Waziri Kairuki amesema wanaendelea kufuatilia mienendo ya wanyama hao kwa kutumia teknolojia mbalimbali.

“Tumeendelea na operesheni mbalimbali zikiwemo za kutumia helikopta kuwafukuza tembo ambao wamekuwa wakizagaa kutoka katika hifadhi kwenda maeneo mbalimbali,” amesema.

Amesema Mei 8 hadi 9, 2024 wanakwenda kufunga mikanda maalumu kwa tembo watatu na watakuwa huko kufuatilia mienendo ya wanyama hao wakati na baada ya kuwaondoa katika maeneo ya makazi.

Amesema wamepanga kununua helikopta tatu kwa sababu wanayoitumia ni kutoka kwa mdau.

Waziri amesema kazi ya kuwaondoa wanyama hao katika Wialya ya Mvomero mkoani Morogoro imegharimu Sh70 milioni.

Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Mwanga, Joseph Tadayo ameitaka Serikali kujikita katika sababu badala ya hatua za dharura ambazo huchukuliwa wakati tukio linapojitokeza.

“Kwa upande wa mwananchi wa kawaida anahisi tembo wameongezeka na kuwa wengi. Lakini katika taarifa za miaka miwili zinaonyesha tembo wamepungua, Serikali wanasema wananchi wameingia katika shoroba,” amesema.

Amesema suala hilo ni mtambuka na Serikali inapaswa kulishughulikia.

Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso amesema hatua hizo hazitoi suluhisho la muda mfupi kulishughulikia tatizo hilo, hivyo wananchi wataendelea kupata adha.

“Mtalii anapoenda Serengeti anahitaji kuona tembo mmoja na si 10,000 kwa nini tusiwavune na kuwaweka katika kanda ili kupunguza athari hii. Serikali inatakiwa kuweka mkakati wa kuipanga ardhi ya nchi hii,” amesema.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema maeneo yote ambayo Wizara ya Maliasili na Utalii iliwashirikisha wameshafanya matumizi bora ya ardhi ambayo ni vijijini zaidi ya 21.

“Hata hivyo tunaendelea na kazi, tunaamini kama mipango hii itakamilika na viongozi wa vijiji watazingatia matumizi bora ya ardhi basi itapunguza mwingiliano kati ya wanyamapori na wananchi,” amesema.

Spika Dk Tulia ameagiza Serikali kutoa majibu ya haraka pale wanapoombwa maombi ya fedha, rasilimali watu na vifaa.