Wahamiaji haramu 166 wakamatwa Handeni mwaka mmoja

Raia 38 wa Ethiopia wakiwa chini ya ulinzi kituo cha Polisi Mkata wilayani Handeni mkoani Tanga, baada ya kukamatwa leo asubuhi wakiwa ndani ya lori.Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

Gari ambalo limekamatwa wakiwa wamepakiwa wa Ethiopia  hao limesajiliwa kuingia nchini kwaajili ya shughuli ya kusafirisha makaa ya mawe.

Handeni. Jumla ya raia 166 wa kigeni wamekamatwa ndani ya mwaka mmoja wilayani Handeni mkoani Tanga, wakisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini kinyume cha sheria.

Hayo yameelezwa na Afisa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, Joan Ndumbati leo Alhamisi Novemba 10, 2022 wakati akiongea na waandishi wa habari, kituo cha Polisi Mkata baada ya kuwakamata raia 38 wa Ethiopia  na kusema kuwa kundi hilo linafanya wafikie 166 kwa mwaka mmoja.


Amesema raia hao 38 walifichwa ndani ya lori ambalo ndani yake kukiwa kumehifadhiwa mikate na biskuti, ikiashiria ni chakula chao wakiwa safarini huku wakiwa wamefunikwa ili wasionekane.


"Ukijumlisha raia hawa 38 tuliowakamata leo wa Ethiopia ndani ya mwaka mmoja,  jumla tumewakamata raia 166 wa kigeni kwa wakati tofauti wakitokea Ethiopia, Somalia na raia wa Tanzania ambao wanafanya shughuli ya kuwasafirisha watu hao.

Niwaombe wananchi waendelee kutoa ushirikiano wanapoona wageni ambao hawawafahamu vizuri," amesema Joan.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amesema gari hilo liliingia Tanzania kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe, lakini limekutwa na wahamiaji haramu.


"Jeshi la Polisi Wilaya ya Handeni muendelea kuwa wazalendo na kuthibiti matukio haya, kwani matukio kama hayo Handeni yamekuwa yakijirudia hivyo ukiwepo ushirikiano tutaweza kutokomeza," amesema Mchembe.


Diwani Kata ya Kitumbi Augastino Ramadhani amesema vizuizi zaidi viongezwe barabarani ili kuongeza ufanisi katika kukagua magari ambayo yanasafirisha raia hao.