Kunywa kiasi, ulevi kupindukia hupunguza nguvu za kiume

Muktasari:

  • Usemi wa lugha ya Kiingereza wa “Too much of anything is harmful” ambao kwa tafsiri isiyo rasmi inaweza ikawa ni “kila kitu kikizidi kina madhara” ndio unaweza kufaa kuelezea madhara ya unywaji wa pombe kupindukia.


Usemi wa lugha ya Kiingereza wa “Too much of anything is harmful” ambao kwa tafsiri isiyo rasmi inaweza ikawa ni “kila kitu kikizidi kina madhara” ndio unaweza kufaa kuelezea madhara ya unywaji wa pombe kupindukia.

Wataalamu wa afya wanasema kunywa pombe kwa kiasi si jambo baya au lenye madhara kiafya, lakini kiwango kikizidi husababisha madhara si tu ya kiafya, bali pia kiuchumi na kijamii.

Kiuchumi unywaji wa pombe kupindukia unaweza kusababisha matumizi makubwa ya fedha na kupungua kwa nguvu kazi, huku kijamii pombe husababisha mifarakano, kutenda au kutendewa makosa ya jinai, familia kukosa malezi na huduma bora.

Japo baadhi ya watu hudai kunywa pombe kunaondoa aibu kwa kumpa mtu furaha, ujasiri na kujiamini, wataalamu wa afya na viongozi wa dini wanasema unywaji pombe kupindukia una madhara kiafya, kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa kitabu cha mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza kilichotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), kuna madhara mengi ya unywaji wa pombe kupindukia, ikiwemo baadhi ya viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi kikamilifu.

Pamoja na kuathiri uyeyushaji wa chakula, ufyonzaji na utumikaji wa virutubishi mbalimbali vya chakula mwilini, unywaji wa pombe kupindukia pia hudhoofisha ubongo na kufifisha uwezo wa kufikiri kwa tija, hali inayoweza kusababisha mhusika kufanya vitendo visivyo vya kawaida, vikiwemo vya kutia aibu kama kujisaidia kwenye nguo hadharani.

“Unywaji wa pombe uliozidi na kwa muda mrefu unaweza kusababisha magonjwa ya akili, kuharibu ubongo, ini, moyo, kongosho na hatimaye magonjwa ya yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari, ugonjwa wa moyo, msukumo wa juu wa damu, utapiamlo na mwili kudhoofika,” kinaeleza kitabu hicho.


Madhara mengine yanayotajwa kusababishwa na unywaji wa pombe kupindukia ni mhusika kuugua magonjwa kama saratani ya kinywa, koo, ini, utumbo, matiti na tezi dume, bila kusahau tatizo la utapiamlo, kupungua kwa kinga mwilini na hata kupata ugonjwa wa kifua kikuu.

Maambukizi ya magonjwa ya zinaa, virusi vya Ukimwi (VVU), matumizi ya dawa za kulenya na mimba zisizotarajiwa ni madhara mengine ya unywaji wa pombe kupindukia.


Upungufu wa nguvu za kiume

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusu madhara ya pombe, Mkuu wa Programu ya Afya kutoka kampuni ya Bright Future, Dk Sila Julius anasema pamoja na madhara mengine kiafya, unywaji uliopindukia wa pombe pia husababisha tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

“Matumizi makubwa ya kilevi, ikiwemo kuvuta ugoro na sigara huathiri ubora wa utendaji kazi wa kisaikolojia na hivyo kuathiri nguvu za kiume kwa sababu ubora wa saikolojia ya mwanaume una mchango mkubwa kwenye suala la kujamiiana.

“Kiwango kikubwa cha kilevi mwilini huharibu mfumo wa mzunguko wa damu ambao ni muhimu katika kufanya kiungo cha uzazi cha mwanamume kusimama vizuri na kuwa na nguvu wakati wa tendo la kujamiiana,” anasema Dk Sila.

Anasema ulevi kupindukia huathiri mzunguko wa damu, hali inayofanya mishipa kusinyaa na kushindwa kufikisha kiwango cha damu kwa ujazo unaotakiwa kwenye kiungo cha uzazi cha mwanamume ambaye hatimaye hujikuta hana nguvu za kiume.

Anasema ni vema kama mtu hatakunywa kabisa aina yoyote ya kilevi kwa sababu vileo hulegeza mfumo wa misuli na kusababisha mwili kukosa nguvu.

“Kama mtu akishindwa kabisa kuacha, basi ni vema kunywa kwa kiasi ili kulinda afya ya mwili ambayo ndio mtaji katika kila jambo,” anasema Dk Sila.

Kiwango cha pombe kwa siku

Kwa mujibu wa kitabu cha mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza kilichotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TANCDA, kiafya mwanamume anatakiwa kunywa si zaidi ya chupa mbili za bia kwa siku, huku mwanamke akitakiwa kunywa chupa moja pekee.

Vivyo hivyo kwa mvinyo au pombe kali, mwanamume anashauriwa kunywa glasi mbili au toti mbili za pombe kali, huku mwanamke akitakiwa kunywa glasi moja ya mvinyo au toti moja ya pombe kali.


Athari kwa mjamzito, mtoto

Licha ya madhara kwa mjamzito, pombe pia inaelezwa kuwa ni hatari kwa afya ya mtoto aliye tumboni.

“Kilevi kinapoingia kwenye mfumo wa damu wa mama mjamzito huenda moja kwa moja kwenye mfumo wa damu ya mtoto aliye tumboni na kumsababishia madhara,” anasema Dk Sila.

Anasema kilevi kinapoingia kwenye mfumo na mzunguko wa damu ya mtoto aliye tumboni huathiri ujenzi na ukuaji wa mwili wa mtoto, hali inayoweza kusababisha madhara kadhaa, ikiwemo mtoto kuzaliwa kabla ya muda kufika au hata kufia tumboni.

“Mtoto aliyeathirika kwa wingi wa kilevi akiwa tumboni mwa mama yake anaweza kuzaliwa akiwa na matatizo ya akili,” anasema mtaalamu huyo wa afya.

Madhara mengine kwa mtoto aliye tumboni ambaye mama yake anakunywa pombe ni kuzaliwa akiwa na matatizo ya kupumua, kuwa na tatizo la ukuaji, kukosa kinga ya mwili na kuugua mara kwa mara.

“Kibaya zaidi kwa afya, makuzi na malezi ya mtoto hata ukubwani ni hatari ya kurithi tabia ya ulevi sugu,” anaonya Dk Sila, huku akisisitiza kuwa si jambo jema mjamzito kunywa pombe.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Johari Mlaghwa, mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi anayesema madhara ya unywaji pombe kwa mjamzito humwathiri mtoto moja kwa moja kwa sababu mifumo ya wawili hao inakuwa inategemeana kwa kila kitu.

“Chochote anachokula na kunywa mama mjamzito humfikia mtoto moja kwa moja, hivyo kilevi anachokunywa mama humwathiri moja kwa moja mtoto tumboni. Ni vema mama mjamzito kutokunywa kabisa aina yoyote ya kilevi kumlinda mtoto,” anasema Johari.

Mtaalamu huyo anasema mfumo na ubora wa ini ni eneo lingine linaloathiriwa na unywaji wa pombe.

“Ini ndio hutumika kama mlinzi wa kemikali na vitu vyote vya aina hiyo vinavyoingia mwilini kwa kuvichuja na kuondoa visivyostahili; ini linapoathirika mwili mzima uko hatarini. Unywaji wa pombe ni kati ya vitu hatari kwa afya ya ini,” anasema Johari.

Anaongeza; “Hata udhibiti wa kiwango cha insulin mwilini huathirika pindi ini linapopata madhara. Hii husababisha uwezekano wa mhusika kupata ugonjwa wa kisukari kwa sababu ya kukosekana kwa insulin.”



Nguvu kazi ya Taifa

Katika mahubiri na mafundisho yake wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo alikemea tabia ya vijana nchini kutumia pombe kali, akieleza ni hatari kwa nguvu kazi ya Taifa.

Kiongozi huyo wa kiroho alielezea hofu yake ya kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali ambazo baadhi zina kiwango cha kilevi cha asilimia 40.

Akizungumzia ulevi uliopindukia hususani kwa kundi la vijana, Mkazi wa Majembe Makali jijini Mwanza, Juma Rashidi aliwataka wazazi wawe mstari wa mbele kuhakikisha vijana wao hawaingii kwenye ulevi ambao mara nyingi hujiingiza kwa kufuata mkumbo wa makundi kwa kufuatilia nyendo zao na kuwaelimisha kwa upole madhara yake.

Ester Justine, mkazi wa mtaa wa Igogo jijini Mwanza anaunga mkono ushauri wa kutokunywa kabisa pombe au kunywa kwa kiasi kulinda si tu maadili, bali pia uchumi, malezi na makuzi mema katika jamii.

“Huku mitaani tunashuhudia madhara ya ulevi wa kupindukia kwa baadhi ya wakuu wa familia ama baba au mama kutumia kila senti anayopata kwenye pombe bila kujali mahitaji ya familia,” anasema Ester.