Miaka 20 ya Poland ndani ya Umoja wa Ulaya

Balozi wa Poland nchini Tanzania, Krzysztof Buzalski (katikati) akizungumza na waandishi wa habari waandamizi kutoka kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL). Kushoto ni Peter Elias na kulia ni Jacob Mosenda. Picha na Michael Matemanga.

Leo, Mei Mosi, Poland inaadhimisha miaka 20 tangu ilipojiunga na Umoja wa Ulaya (EU) mwaka 2004. Kipindi hicho, ilipokea kundi kubwa la nchi 10 za Ulaya Mashariki na Kati, ikiwemo Poland ambazo kwa pamoja zilijiunga na umoja huo wenye nguvu duniani.

Tangu ilipojiunga na EU, Poland imeshuhudia mabadiliko mengi ya kijamii na kiuchumi ambayo yamelifanya taifa hilo kupiga hatua, tofauti na awali kabla ya kujiunga na Umoja wa Ulaya na kufurahia maisha ndani yake.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Balozi wa Poland nchini Tanzania, Krzysztof Buzalski, anayezungumzia namna nchi yake inavyojivunia kujiunga na EU na somo ambalo mataifa mengine yanalipata kutoka kwenye umoja huo.

Buzalski anasema mahali walipoanzia ilikuwa ni kuanguka kwa ukomunisti mwaka 1989. Mwaka huo, Poland na mataifa mengine ya Ulaya ya Kati na Mashariki yalipata tena uhuru wao kutoka Muungano wa Kisovieti uliofuata mfumo wa kisoshalisti (ujamaa).

“Hatukulazimika tena kutii amri ya kisiasa na kiuchumi ya Moscow. Wasomaji wakongwe wa Mwananchi watakumbuka kwamba katika miaka ya 1960, 1970 na 1980, Poland na Tanzania tulikuwa marafiki wa karibu, tulishirikiana katika miradi ya pamoja ndani ya mfumo wa ujamaa.

“Hata hivyo, ikumbukwe kwamba kwetu kilikuwa kipindi cha giza cha uchumi duni, uliopangwa na serikali kuu, uhuru mdogo, vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali, na zaidi ya yote - hisia ya kunyimwa uhuru wetu,” anasema Balozi Buzalski.

Anasema kuporomoka kwa ukomunisti ilikuwa nafasi kwao kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wao wa kisiasa na kiuchumi. Chaguo hilo lilikuwa dhahiri na walishuhudia jinsi nchi za kidemokrasia na ustawi wa Ulaya Magharibi zilivyokuwa zikifaidika kutokana na ushirikiano wao.

Buzalski anasema idadi kubwa ya Wapoland waliunga mkono njia hii mpya iliyochukuliwa na serikali yetu mpya iliyochaguliwa kidemokrasia, na kusababisha mageuzi ya mfumo wa kisiasa na kiuchumi na mwelekeo wake kimagharibi. Anasisitiza kwamba ilikuwa ni njia ngumu, kwani tulianza kwa kiwango cha chini sana cha maendeleo.

“Mwaka 1990 pato la Taifa kwa kila mtu lilikuwa chini ya Dola za Marekani 5,000. Uchumi ulimilikiwa na serikali na haukuwa na tija sana wananchi. Miundombinu yote nchini ilikuwa katika hali mbaya. Mifumo wa kisheria ilihitaji marekebisho ya jumla ili kuhakikisha haki za binadamu na uhuru. Marekebisho ya haraka yalihitajika kusaidia biashara binafsi kukita mizizi na kuendelea.

“Kipindi cha miaka ya 1990 – 2004 kilikuwa katika wakati wa mabadiliko ya haraka na mageuzi makubwa. Mengi yalifanyika ili kurekebisha mifumo yetu ya kisheria na kukidhi mahitaji ya kujiunga na Umoja wa Ulaya,” anasema Balozi Buzalski.

Hata hivyo, anasema waliungwa mkono kifedha na katika masuala ya utaalamu na Umoja wa Ulaya. Anasema wataalamu wengi wa Ufaransa, Uingereza, Uhispania na wengine Umoja wa Ulaya walikwenda Poland na kuwasaidia kuboresha sekta ya utawala, kanuni za bajeti ya serikali na kuongeza ufanisi wa mifumo ya kodi.

Anabainisha kwamba ilikuwa ni juhudi kubwa ya mamilioni ya watu wa Poland kurejesha nchi kwenye miguu yake. Anasema hali hiyo hiyo inatumika kwa mataifa mengine ya Ulaya ya Kati na Mashariki, kama vile Wacheki, Waslovakia, Wahungaria, Waslovenia, Walithuania, Walatvia na Waestonia ambao tulijiunga pamoja nao kwenye Umoja wa Ulaya mwaka wa 2004.
 

Kilichobadilika Poland

Balozi Buzalski anasema ushirikiano wa kimataifa ndani ya kizuizi cha kikomunisti mara nyingi ulikuwa wa kiitikadi zaidi kuliko ufanisi au matokeo yanayoonekana. Hivyo, baada ya kusambaratika kwake walirithi muundo wa sera ya kigeni usiofaa na wa gharama kubwa, ambao ulihitaji marekebisho ya kina.

Anasema malengo yao ya sera za kimataifa yalibadilika kabisa. Kipaumbele chao kilikuwa ni kusisitiza usalama wa Poland kwa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharini (Nato), na uchumi wa Poland kwa Jumuiya ya Ulaya.

“Kitu kilichotusumbua kutokana na hali hiyo ilikuwa ni uhusiano na nchi nyingine duniani kama vile washirika wetu wa Kiafrika. Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ilibidi tufunge balozi zetu nyingi nje ya nchi. Kwa muda hatukuweza kutoa fursa ambazo nchi hizi walistahili.

“Mwenendo huo umebadilika hivi karibuni tu, kwani Poland imejiunga na kundi la nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi na kuwa wafadhili wanaoibukia kimaendeleo. Sababu nyingine ni kwamba Afrika inakua kwa haraka kuwa bara la fursa ya kibiashara na uwekezaji,” anasema.

Anasema anaamini Umoja wa Ulaya unafaa zaidi sasa kuliko hapo awali. Anasema hawapaswi kusahau kwamba umoja huo unawakilisha mafanikio makubwa ya ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi nyingi katika historia ya dunia.

“EU umeleta uhuru na ustawi mkubwa kwetu sote raia wa nchi wanachama wake. Umetupa sauti thabiti, mwonekano madhubuti na uwezo bora wa kukuza maadili yetu kwenye jukwaa la kimataifa,” anasisitiza Balozi Buzalski.

 

Kujitoa kwa Uingereza

Balozi Buzalski anaeleza kwamba akirejelea kujitoa kwa Uingereza katika Umoja huo, anadhani lilikuwa tukio la pekee na hafikirii kama kuna nchi nyingine itakayofuata.

Anasema kama Wapolandi wengi wanavyofikiri, yeye pia anatumaini kwamba Waingereza wanaweza kufikiria upya uamuzi wao wa kujitoa kwenye EU baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa faida na hasara.

Anasema hivi sasa, vyama vya siasa vya mrengo wa kulia vinaelekeza ajenda zake kuboresha Umoja wa Ulaya badala ya kujitoa kabisa.

“Ikiwa tutachukua mrengo wa wa busara juu ya masuala yenye mizozo ya kijamii kama vile uhamiaji usiodhibitiwa ninatarajia kuongezeka kwa nchi mpya kwenye Umoja kuliko kujitoa,” anaeleza Balozi huyo kwenye mahojiano na Mwananchi.
 

Somo kwa EAC

Balozi Buzalski anasema kama mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Poland kwa kawaida imekuwa mtetezi na mfuasi wa upanuzi wa haraka wa Jumuiya. Wamekuwa wakijishughulisha na usalama wa nchi za kidemokrasia wa Ulaya ya Kati na Mashariki.

Anasema wametetea kujumuishwa kwa nchi zote zilizotayari kufanya hivyo, hata kwa gharama ya ushirikiano wa dhati wa EU. Hata hivyo, kama ilivyo kwa muundo wa maendeleo, huwezi kunakili sera kama ilivyo kutoka bara moja hadi jingine.

“Nadhani ni wananchi na viongozi wa EAC pekee wanaoweza kujiuliza maswali haya; Je, uanachama wa washiriki wapya kwenye jumuiya utawasaidia kutatua migogoro yao ya ndani na migogoro na majirani zao? Je, mimi kama mwananchi wa EAC nitafaidika vipi na ongezeko za umoja huo? Je, itanufaisha vipi familia yangu, wilaya yangu, mkoa wangu na taifa langu? Je, itapanua fursa katika masuala ya masomo, usafiri, kazi, kupata faida katika kampuni yangu?

“Maswali kama hayo yana afya kwa majadiliano juu ya uandikishaji mpya katika kila nchi ya EU. Na kwa hakika, baada ya kuijadili, huwa tunapaswa kufikia makubaliano yanayoheshimu sheria za demokrasia na sauti ya wananchi,” anasema.