Usiyoyajua kuhusu Dk Nchimbi, Katibu Mkuu mpya CCM

Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi

Muktasari:

  • Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imemteua Mwanadiplomasia Dk Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Dk Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wake wakati chama hicho kikijipanga kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Dk Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo aliyejiuzulu Novemba 29, 2023 akiwa ametumikia nafasi kwa siku 943 tangu alipoteuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) Aprili 30, 2021.

Chongolo alijiuzulu Novemba 27, 2023 kwa kile kilichoelezwa kwenye barua yake iliyosambaa mitandaoni kuwa ni “kuchafuliwa kupitia mitandao ya kijamii”, hivyo akaamua kuwajibika kama kiongozi.

Akizungumzia uteuzi wa Balozi Nchimbi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imepokea pendekezo la Kamati Kuu kuhusu jina la katibu mkuu mpya wa CCM.

“Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wameridhia kwa kauli moja pendekezo hilo na kumchagua Balozi Emmanuel Nchimbi kuwa katibu mkuu wa CCM,” amesema Makonda baada ya kikao hicho kilichoketi Zanzibar.

Uteuzi wa Dk Nchimbi katika nafasi hiyo ulitabiriwa na wadau mbalimbali wa siasa na kutajwa na Gazeti la Mwananchi yeye pamoja na wenzake akina Martin Shigella, William Lukuvi na Amos Makalla, wote wakiwa ni makada wa kitambo ndani ya chama hicho.

Ni mtu sahihi

Makada wa CCM, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya upinzani, wanasema ni mtu sahihi kwenye nafasi hiyo kwa sababu ya uzoefu wake katika uongozi ndani ya CCM, si mnafiki na ana msimamo.

Unaweza kuilinganisha historia ya Dk Nchimbi ndani ya CCM na umri wa mtu mzima wa miaka 35. Ameanza kuwa kiongozi katika chama hicho mwaka 1998 alipochaguliwa kuwa mjumbe wa NEC.

Hakuishia hapo, alichaguliwa na wajumbe wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuwa mwenyekiti wao na hivyo aliiwakilisha jumuiya hiyo kwenye kamati kuu na halmashauri kuu.

Mwaka 2005, mwanasiasa huyo alijitosha katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge katika Jimbo la Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma. Alipata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya mpinzani wake mkuu kutoka Chadema, Edson Mbogoro.

Ubunge wake, ulifungua milango mingine ya nyadhifa ndani ya Serikali, Januari mwaka 2006, Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Alidumu kwenye wadhifa huo kwa miezi tisa na Oktoba mwaka huo alihamishiwa Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana akiwa na nafasi ileile hadi Februari mwaka 2008.

Mwanasiasa huyo alihamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa naibu waziri, alikohudumu hadi mwaka 2010.

Kipenga cha uchaguzi kilipopigwa mwaka 2010, aliwania tena ubunge katika eneo lilelile, alishinda na kuanzia hapo nyadhifa zake ndani ya Serikali ziliongezeka.

Rais Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo hadi Mei 2012, alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013.

Sababu ya kujiuzulu kwake ni shinikizo, baada ya kuguswa kwenye ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na mbunge wa Kahama, James Lembeli kuhusu “Oparesheni Tokomeza Ujangili (Otu).

Operesheni hiyo iliyoanzishwa na Serikali, ilizua mtikisiko uliowang’oa madarakani mawaziri wanne akiwemo Dk Nchimbi ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.

Mbali na Dk Nchimbi, wengine waliong’olewa ni Khamisi Kagasheki wa Maliasili na Utalii, Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.

Baada ya uchaguzi huo, mwaka 2016, Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil na baadaye mwaka 2022 aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Misri alikohudumu hadi mwaka 2023 alipomaliza muda wake na kurejea nchini.

Misukosuko aliyopitia

Machi mwaka 2017, akiwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk Nchimbi aliwahi kukumbwa na msukosuko ndani ya chama chake, akapewa onyo kali na adhabu ya kutogombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.

Adhabu hiyo ilitokana na kilichoelezwa na CCM kuwa, ni usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo, makada wengine wa chama hicho walifutwa uanachama akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba.

Katika uchaguzi huo, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kumpendekeza Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.

Dk Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba walikuwa wanamuunga mkono Edward Lowassa aliyekuwa akiwania urais mwaka 2015 kupitia CCM kabla ya jina lake kukatwa na kutimkia Chadema.

Hata hivyo, baada ya mgombea urais kupatikana, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani na kueleza kwamba kama chama kimefanya uamuzi, mtu akiendelea kuupinga, huo ni usaliti.

Wasifu zaidi

Kada huyo alizaliwa Desemba 24, mwaka 1971 mkoani Mbeya na alianza masomo katika Shule ya Msingi Oysterbay, Dar es Salaam mwaka 1980 hadi 1986.

Mwaka 1987 hadi 1989 alisoma elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Uru na baadaye kuhamia Shule ya Sekondari Sangu alikomalizia kidato cha nne mwaka 1990.

Kidato cha tano na sita alisoma katika Shule ya Sekondari ya Forest Hill mkoani Morogoro mwaka 1991 hadi 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala 1997.

Baadaye alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara katika chuo hicho, mwaka 2001 hadi 2003 akibobea kwenye maeneo ya benki na fedha na mwaka 2011 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hicho.

Dk Nchimbi ni mume na baba wa watoto watatu.