Ihefu yatangulia mapema nusu fainali FA

Muktasari:

  • Mchezo huo wa robo fainali unaifanya Ihefu kusubiri mshindi wa mechi ya baadaye kati ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga itakayocheza na Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex ili kujua mpinzani wake wa nusu fainali.

TIMU ya Ihefu imefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuifunga Mashujaa kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia miamba hiyo kutoka suluhu ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida.

Mchezo huo wa robo fainali unaifanya Ihefu kusubiri mshindi wa mechi ya baadaye kati ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga itakayocheza na Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex ili kujua mpinzani wake wa nusu fainali.

Nusu fainali itapigwa Mei 18 hadi 19 huku fainali ikipigwa Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite, uliopo Babati Manyara.

Tangu kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1967 ikifahamika kwa jina la FAT kabla ya 2015 kubadilishwa na kuitwa ASFC, Yanga ndio timu iliyotwaa mara nyingi ikifanya hivyo mara saba kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.

Mbali na Yanga ila timu nyingine iliyofika hatua hii na kuchukua ubingwa wa michuano hiyo ni Azam FC iliyofanya hivyo msimu wa 2018-2019 baada ya kuifunga Lipuli ya Iringa kwa bao 1-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa Ilulu uliopo mjini Lindi.

Ihefu ilifika hatua hiyo kwa kuiondoa KMC katika hatua ya 16 bora kwa kuitandika mabao 3-0 huku Mashujaa ikiitoa Simba kwa penalti 6-5 kufuatia kufungana bao 1-1 ndani ya dakika 90 za mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.

Kwa sasa kuna mchezo mwingine wa robo fainali kati ya Coastal Union na Geita Gold unaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwan, jijini Tanga.