Mghana aipeleka Coastal nusu fainali FA, yaisubiri Azam, Namungo FC

Muktasari:

  • Bao pekee la Coastal Union limefungwa dakika ya 23 na nyota Mghana, Dennis Modzaka aliyepeleka furaha ndani ya timu hiyo baada ya mechi yao iliyopita ya Ligi Kuu Bara kuchapwa bao 1-0 na Yanga Aprili 27.

COASTAL Union imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold katika mchezo mkali uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Bao pekee la Coastal Union limefungwa dakika ya 23 na nyota Mghana, Dennis Modzaka aliyepeleka furaha ndani ya timu hiyo baada ya mechi yao iliyopita ya Ligi Kuu Bara kuchapwa bao 1-0 na Yanga Aprili 27.

Coastal ilifika robo fainali baada ya kuitoa JKT Tanzania kwa mikwaju ya penalti 5-4 kufuatia suluhu ndani ya dakika 90, huku Geita Gold ikiitoa Rhino Rangers kwa mabao 2-1.

Ushindi huo unaifanya Coastal kusubiri  mshindi kati ya Azam itakayocheza na Namungo, Ijumaa Mei 3, ili kucheza nusu fainali itakayopigwa kati ya Mei 18 hadi 19, huku ikiwa na kumbukumbu ya kutinga fainali msimu wa 2021-2022.

Coastal ilitinga fainali hiyo na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Yanga baada ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Julai 2, 2022 kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 ndani ya dakika 120.

Endapo Coastal itakutana na Azam FC itakuwa ni mechi ya kisasi kwani msimu uliopita zilipokutana kwenye nusu fainali Azam ilishindwa kufurukuta baada ya kutolewa kwa penalti 6-5 kufuatia suluhu katika dakika 120.

Fainali ya michuano hiyo msimu huu inatarajiwa kupigwa Juni 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Tanzanite, uliopo Babati Manyara.