Sababu kwa nini Mgunda anatosha Simba

Muktasari:

  • Mgunda ambaye alikuwa timu ya Wanawake Simba Queens alirudishwa kwenye kikosi cha wakubwa baada ya kuondoka aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha juzi, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa anasumbuliwa na matatizo ya kifamilia.

Mashabiki wa Simba wamepata mzuka upya wakiwa na matumaini makubwa kwa kocha wa timu hiyo Juma Mgunda ambaye anasaidiana na Selemani Matola.

Mgunda ambaye alikuwa timu ya Wanawake Simba Queens alirudishwa kwenye kikosi cha wakubwa baada ya kuondoka aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha juzi, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa anasumbuliwa na matatizo ya kifamilia.

Mgunda siyo mgeni kwenye kikosi cha Simba akiwa alishakaa hapo, lakini pia ana uzoefu mkubwa kwenye soka akiwa alishaifundisha Coastal Union kwa mafanikio makubwa jambo ambalo linawapa kiburi mashabiki.

Wadau wa soka wanaamini kuwa Mgunda anaweza kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri kuliko Benchikha au kocha mwingine yoyote wa kigeni kwa sasa kwenye michezo tisa iliyobaki baada ya jana timu hiyo kuvaana na Namungo.

Kocha huyo ana rekodi nzuri kwenye kikosi cha Simba, alipokaa hapo kwa miezi mitatu kama kocha mkuu na baadaye kuondoka na kumuachia Robert Oliviera Robertinho ambaye aliondoka baada ya kuchapwa mabao 5-1 na Yanga.

Mgunda mzaliwa wa Tanga, akiwa na Simba aliisimamia kwenye michezo tisa, lakini jambo la kufurahisha ni kwamba alipoteza mchezo mmoja tu, akitoka sare mmoja na sasa ana kibarua tena cha michezo tisa.


Aliibana Yanga

Mgunda alionyesha umwamba wake kwenye michezo mikubwa ambapo katika michezo yake tisa alifanikiwa kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga, ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi.

Katika mchezo huu mashabiki wa Simba pamoja na sare hiyo waliipongeza timu yao kwa kucheza kwa kiwango cha juu, huku ikitumika kauli ya ‘Acha boli litembee.’

 Mkali wa ulinzi

Baada ya timu hiyo kuwa chini ya Mgunda na Matola, awali mashabiki hawakuwa na matumaini makubwa, lakini kocha huyo aliiongoza katika michezo tisa kikosi chake kikifunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu.

Balaa alilonalo kocha huyo ni kwamba, kwenye mchezo ambao alipoteza kipindi cha nyuma ni dhidi ya Azam ambao alilala kwa bao 1-0 na sasa timu hizo zinakwenda kukutana tena baadaye mwezi huu kwenye mchezo wa maamuzi ya timu gani inaweza kumaliza kwenye nafasi ya pili je? Atalipa kisasi.

Lakini akikuta timu hiyo imeshamalizana na Yanga ambayo imefanikiwa kushinda michezo yote miwili dhidi ya Simba msimu huu, ikishinda 5-1 mzunguko wa kwanza na 2-1, mzunguko wa pili.




Akiwa na Simba Mgunda aliichapa Prisons bao 1-0 kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa ni mara kwanza Simba inaibuka na ushindi nyumbani kwa Prisons tangu mwaka 2019, akaichapa Dodoma Jiji mabao 3-0, akatoka sare ya 1-1 na Yanga.

Baada ya mchezo dhidi ya Yanga, Mgunda alikutana na kichapo cha kwanza alipolala 1-0 dhidi ya Azam, lakini kikosi chake kikarejea kwa nguvu na kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mtibwa kikiwa ni kipigo kikubwa kutolewa na Simba kwa msimu huo.

Katikati timu hiyo ya Mgunda ilicheza michezo miwili ya kirafiki, dhidi ya Kipanga na kushinda 3-0 na kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Malindi.

Kwenye ligi katika michezo hiyo mitano timu yake ilifunga mabao 10 na kufungwa mawili tu na timu kubwa za Azam na Yanga, rekodi ambazo mashabiki wa Simba wanatakiwa kuzisubiri kwa sasa wakati timu hiyo itakuwa chini yake hadi mwishoni mwa msimu.

Kimataifa yupo vizuri

Mgunda akiwa na Simba aliweka rekodi ya kuwa kocha pekee mzawa kuipeleka timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 1998, wakati marehemu Tito Mwaluvanda alipoifikisha Yanga kwenye hatua hiyo.

Mgunda alishinda michezo miwili dhidi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuichapa Big Bullets ya Malawi jumla ya mabao 4-0, lakini akaichapa De Agosto ya Angola, jumla ya mabao 4-1.  

Lakini pia aliweka rekodi ya kocha wa kwanza mzawa kuifikisha timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, alipoziondoa Nyassa Bullets kwa jumla ya mabao 4-0, De Agosto kwa jumla ya mabao 4-1.


Atoa kauli:

Akizungumza baada ya kufika Lindi juzi, Mgunda alisema amepewa kazi ya kuifundisha Simba na anaamini anatakiwa kuibeba mabegani kwake.

Hii ni kazi kama nyingine, nafurahi kwa kuwa nipo hapa kazi yangu ni kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye michezo ijayo.

“Nimeshakutana na benchi la ufundi tumeshazungumza nimeelewa changamoto ambazo zipo natakiwa kupambana nazo, naamini tutafanya vizuri kwenye michezo yote iliyobaki, tuombe Mungu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars.

Wadau wanamtaka:

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa, amesema kwa sasa timu hiyo ipo kwenye mikono salama chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda na msaidizi wake, Selemani Matola.

"Ninaiona Simba ikiwa katika mikono salama kutokana na uwezo alionao Mgunda kwa sababu hapo awali alionyesha na sasa anakwenda tena kuendelea palepale nafikiri Simba ilistahili kocha huyo tangu awali," alisema Pawasa.


Pawasa alienda mbali zaidi na kusema kwamba, kuondoka kwa Abdelhak Benchikha, ibaki kama somo kwa viongozi wa Simba, wajitafakari inakuwaje kocha mkubwa kama yule anaondoka mapema licha ya kwamba lazima uamuzi wake uheshimiwe.

"Kitendo cha Benchikha kuondoka viongozi wajitafakari kwa nini ameondoka, baada ya hapo waangalie wanakwenda wapi kabla ya kumtafuta mrithi wake.

"Wasiangalie makocha wa levo ya juu kama hawana uwezo wa kudumu nao, warudi mezani kuimarisha kikosi kwanza au kusaka kocha ambaye akija wawe na uwezo wa kusajili wachezaji kulingana na matakwa yake kwa sababu kocha ndiye anajua aina ya wachezaji wanaoingia kwenye mfumo wake," alisema Pawasa.

Kwa upande wa Kocha mkongwe nchini  na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, amesema kilichopo sasa Simba wampe ushirikiano wa kutosha Mgunda ili aifanye kazi yake vizuri, kwa kuwa anamuona anafaa kwenye nafasi hiyo.

"Yeye sio mgeni ndani ya Simba, alikuwa hapo kwenye wakati mgumu na kuiweka sawa timu, kikubwa wampe sapoti na matumaini ili aweze kuifanya kazi yake vizuri.

"Kumpa jukumu hilo Mgunda naona Simba imepata mtu sahihi ambaye anaweza kuwatoa hapo walipo sasa na kufika sehemu wanapopataka," alisema Mkwasa na kuongeza.

"Ujue kumekuwa na tabia ya makocha wazawa kutoaminika kwenye hizi klabu zetu kubwa, ifikie wakati sasa viongozi wawaamini wazawa na kuwaweka kando kidogo makocha wa kigeni ambao wanakuja na kushindwa kukaa kwa muda mrefu.

"Makocha wa kigeni wanaokuja wapo wazuri, lakini wakati mwingine lugha wanayoitumia inakuwa changamoto kwa wachezaji hasa wazawa, hivyo unapokuwa na kocha mzawa, inakuwa rahisi kwenye mambo mengi kwa sababu anajua mazingira ya nchi yetu na miundombinu ya viwanja, pia anawajua vizuri wachezaji tabia zao," alisema.

Mechi atakazosimamia Mgunda

APRILI 30, 2024

Namungo vs Simba

MEI 3, 2024

Simba   vs   Mtibwa

MEI 6, 2024

Simba   vs   Tabora United

MEI 9, 2024

Azam    vs   Simba

MEI 12, 2024

Kagera  vs   Simba


MEI 16, 2024

Dodoma Jiji vs   Simba

MEI 21, 2024

Simba   vs   Geita

MEI 25, 2024

Simba   vs   KMC

MEI 28, 2024

Simba   vs   JKT TZ