Simba ya Mgunda na mambo mapya

Siku chache baada ya kurudishwa Simba, kocha Juma Mgunda ametaja mambo matatu yatakayombeba kwenye mechi nane zilizobaki akianza na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo ugenini.

Mgunda ambaye ni kocha wa zamani wa Coastal Union, amerudishwa akitokea timu ya wanawake Simba Qeens kuchukua nafasi ya Abdelhak Bechikha ambaye ameachana na timu hiyo kwa kile kilichotajwa ana matatizo ya kifamilia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda ambaye ni miongoni mwa makocha wazawa wazoefu, alisema anakazi kubwa tatu kuhakikisha anairudisha Simba kwenye ushindani huku akiweka wazi kuwa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji, kurudisha morali na mbinu ambazo zitampa matokeo.

"Sio rahisi lakini nina imani kubwa kwamba nitaisaidia Simba kurudi kwenye ushindani kwa kufanya mambo hayo matatu naamini wakezaji watarudisha timu sehemu nzuri," alisema na kuongeza;

"Wachezaji waliopo Simba wote wamepevuka wanaelewa namna ya kufanya ili kuweza kuiweka timu kwenye ushindani hivyo ili waweze kufanya hivyo muhimu ni kuwajenga kisaikolojia na kuwarudisha kwenye morali nzuri." alisema.

Mgunda alisema hakuna mabadiliko makubwa ndani ya timu wachezaji wengi waliopo tayari ameshafanya nao kazi hivyo hawezi kuweka wazi kuwa anaenda kufundisha namna ya kufunga au kukaba kwania anaamini hiyo kazi tayari wanaifahamu.

"Kusema nimekuja kufundisha ni kujiweka kwenye nafasi mbaya na kutokuwaheshimu watangulizi wote walikuwa bora na walifanya kazi kwa usahihi na mimi nimekuja na vitu hivyo vitatu kwa kuanzia ili kuweza kumalizia  walipoishia wao," alisema.

Akizungumzia suala la mbinu, Mgunda alisema ni kuto kutoa mwanya kwa wapinzani wao kuwachukulia kama timu ya kuchukua pointi wanapambana na wao kusaka pointi zitakazowaweka kwenye nafasi nzuri.

"Huu ni mzunguko wa lala salama kila timu inapambana kuhakikisha inajihakikishia nafasi ya kucheza mchezo ujao huku timu nyingine kama Simba tukisaka nafasi tatu za juu hivyo nataka kuijenga timu hii kuwa ya ushindani na sio ya kugawa pointi," alisema.


MGUNDA NI KAMA KIRAKA

Mgunda kuna wakati anafanya majukumu yake kama kiraka. Baada ya Simba kuachana na Benchikha, hivyo Mgunda kapewa kukaimu nafasi yake,akisaidiana na Seleman Matola na mchezo wake wa kwanza ni sare ya 2-2 dhidi ya Namungo.


DATA ZA BENCHIKHA

Tangu atambulishwe, Benchikha ameiongoza timu hiyo katika jumla ya michezo 21 katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu.

Ligi Kuu Bara  michezo 11  ameshinda sita, sare mitatu na kufungwa miwili, mabao ya kufunga 18  ya kufungwa manane.

Ni michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara ambayo Benchikha hakuiongoza Simba ambayo ni dhidi ya Coastal Union ambayo timu hiyo ilishinda mabao 2-1 (Machi 9, 2024) na ushindi wa 3-1 mbele ya Singida Fountain Gate uliopigwa Machi 12, mwaka huu.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika aliiongoza mechi saba, alishinda miwili, sare miwili na kupoteza mitatu, kikosi chake kiujumla kikifunga mabao manane na kufungwa mabao manne.

Michuano mingine ni ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo Benchikha alijikuta akitolewa mapema tu hatua ya 16 bora dhidi ya Mashujaa, dakika 90 zilimalizika kwa bao 1-1,kisha zikapigwa  penalti 6-5.

Katika Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu baada ya kusimama kwa miaka 22, Benchikha aliiongoza timu hiyo michezo yote miwili na kushinda yote akianza na 2-0, dhidi ya KVZ kisha kuifunga Azam FC bao 1-0 kwenye fainali na kutwaa taji hilo.

Benchikha alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, 2023 akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Yanga kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya 2-2 na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri.


MGUNDA 2022/23

Kwa mara ya kwanza Simba, ilimchukua Mgunda kutoka Coastal Union 2022/23 ambapo mchezo wake wa kwanza kusimama benchi ilikuwa dhidi ya Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10/2022) wa Ligi ya Mabingwa Afrika, alizipa pengo la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Zoran Maki.

Mgunda alikaa benchi mechi 16 za Ligi Kuu, akisaidiana na Matola kabla ya kuja kocha Roberto Oliveira 'Robertinho ambaye naye akatimuliwa mikoba akapewa Benchikha ambaye pia kasepa na timu imerudi mikononi mwa Mgunda.


MECHI ZA MGUNDA 2022/23

Mechi alizokaa Mgunda benchi ni dhidi ya Prisons 0-1 Simba (Sep 14/2022),Simba 3-0 Dodoma Jiji (Oktoba/2022),Yanga 1-1 Simba (Oktoba 23/2022),Azam 1-0 Simba (Oktoba 27),Simba 5-0 Mtibwa Sugar (Oktoba 30/2022),Singida Big Stars 1-1 Simba (Nove11/2022),Simba 1-0 Ihefu (Nov 12/2022),Simba 1-0 Namungo (Nov 16/2022),Ruvu Shooting 0-4 Simba (Nov 19/2022).


Mbeya City 1-1 Simba (Nov 23/2022),Polisi Tanzania 1-3 Simba (Nov 27/2022),Coastal Union 1-3 Simba (Des 3/2022),Geita Gold 0-5 Simba (Des 18/2022),Kagera Sugar 1-1 Simba (Des 21/2022),KMC 1-3 Simba (Des 26/2022),Simba 7-1 Priosns (Des 30/2022).


Mabao ya kufunga -  37

Ya kufungwa -9

Pointi- 37


HAKUPOTEZA CAF

Big Bullets 0-2 Simba (Sept 10/2022),Simba 2-0 Big Bullets(Sept 14/2022),Primeiro de Agosto  1-3 Simba (Oktoba 9/2022)

Simba 1-0 Primeiro de Agosto (Oktoba 16/2022)

ASFC

Simba 8-0 Eagle

Simba 1-0 Coastal

Baada ya ujio wa

Ujio wa Benchikha ukamuweka kando Mgunda, akaonekana na kikosi cha Simba B, hakukaa sana akapelekwa  Simba Queens, akisaidiana na Mussa Mgosi na inaongoza Ligi Kuu ya Wanawake Bara (SWPL).


TAIFA STARS NAKO

Wakati Stars, inacheza michuano ya fainali  za Afcon iliyofanyika nchini Ivory Coast, kocha  Adel Amrouche alipewa adhabu na kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kosa la kutoa kauli ya utata dhidi ya Morocco, Mgunda alikwenda kuzipa pengo.

Kocha Jamhuri Kiwelu 'Julio' alisema kinachoendelea kwa Mgunda kiliwahi kutokea kwake miaka ya nyuma; "Timu kupita nyakati ngumu ni jambo la kawaida kipindi cha nyuma, nilikuwa naifundisha Simba kwa vipindi tofauti, hivyo naamini Mgunda atamaliza vizuri michezo iliyosalia."

Kauli yake iliungwa mkono na kocha mkongwe, Abdallah Kibadeni alisema "Mgunda anawajua wachezaji, wengi wao aliwafundisha baada ya kuondoka Maki na timu ilibakia chini yake na Matola na waliweza kufanya vizuri, naamini watamaliza msimu salama."


MECHI ZILIZOBAKI


Simba vs Mtibwa, Mei 5

Simba vs Tabora, Mei 6

Azam vs Simba, Mei 9

Kagera Sugar vs Simba, Mei 12

Dodoma Jiji vs Simba, Mei 16

Simba vs Geita Gold, Mei 21

Simba vs KMC, Mei 25

Simba vs JKT Tanzania, Mei 28