Watumishi Veta wapanda miti zaidi ya 40,000

Muktasari:

 Serikali imeelekeza kila halmashauri nchini kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka na kuitunza

Dodoma. Watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) wamepanda miti zaidi ya 40,000 ikiwa ni mwitikio wao kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Serikali imeelekeza kila halmashauri nchini kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka na kuitunza, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwaka jana Serikali ya Norway ilisema Tanzania itanufaika na ufadhili Sh7.3 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa nchini.

Takwimu zinaonesha asilimia 65 ya nguvu kazi ya Watanzania iko katika sekta ya kilimo kinachotegemea mvua kwa asilimia kubwa, hivyo athari za mabadiliko ya tabianchi zinavuruga pia uchumi wa Watanzania na Taifa.

Akizungumza wakati wa  upandaji miti lililohusisha wafanyakazi wa Veta Makao Makuu, jijini Dodoma jana Machi 28, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore amesema kazi ya upandaji miti imefanyika kwenye vituo vya chuo hicho nchini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kila mwananchi na kila taasisi kupanda miti ili kutunza mazingira.

Kasore amewaasa watumishi hao kutunza miti iliyopandwa ili ikue na kuleta maana halisi ya mpango wa upandaji miti na amewahimiza watumishi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi.

“Kupanda miti ni jambo moja na kutunza miti hiyo ni jambo lingine la muhimu sana. Nasisitiza tukatunze miti hii ili ikue na kutupa uhai pamoja na kuboresha muonekano wa mazingira yetu,” amesema Kasore.

Ameshukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kutoa miti hiyo bure na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu na utunzaji mazingira.

Ofisa Misitu wa TFS Kanda ya Kati, Jenipha Elius amesema anaamini miti hiyo itatunzwa na kukua vizuri hasa kwa kuzingatia kuwa imefuata hatua zote muhimu za kitaalamu za upandaji miti.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Veta Anthony Kasore (wa nne  kushoto) akiwa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo kwenye shughuli ya kupanda miti Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amewasihi watumishi wa Veta kujenga utamaduni wa kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi na kujipatia faida mbalimbali ikiwamo hali nzuri ya hewa pamoja na matunda na kuwakaribisha kupata miti bure kutoka TFS.

Furaha Paul ni miongoni mwa watumishi walioshiriki zoezi hilo, amesema amejisikia fahari kupanda miti itakayonufaisha Watanzania wengi kwa miaka mingi ijayo.

“Kwa kweli najisikia furaha kushiriki kwenye zoezi hili la kihistoria kwa kuwa naamini miti hii itatumiwa na sisi, watoto wetu, wajukuu hadi vitukuu vyetu,”amesema Furaha.

Kilele cha maadhimisho ya miaka 60 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinatarajiwa kuwa  Aprili 26, 2024.