Hiki hapa alichobaini CAG matatizo afya ya akili

Muktasari:

  • Wizara ya Afya imejipanga kuimarisha mifumo ya watu kupata huduma stahiki ya matatizo afya ya akili.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere imebaini upungufu katika maeneo 12 ya utoaji huduma kwa jamii, ikiwamo ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.

Hayo yamebainishwa na CAG katika ripoti ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

“Wagonjwa wanaongezeka kila mwaka na vifo pia. Vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kupona. Kati ya mikoa 28, ni mitano pekee ndiyo ina vituo vya utengamo vya huduma za afya ya akili,” inaeleza ripoti hiyo.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk John Jingu alipotafutwa na Mwananchi Digital kuzungumzia hali hiyo amesema,“Afya ya akili ni eneo nyeti ambalo kwa sasa tunalifanyia kazi kuhakikisha tunaimarisha mifumo ya watu kupata huduma stahiki.”

Kwa mujibu wa CAG, kuna ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya akili kulingana na utendaji wa kila mwaka wa Wizara ya Afya.

“Mwaka 2022 iliripotiwa katika Hospitali ya Taifa ya Akili ya Mirembe kulikuwa na ongezeko la idadi ya wagonjwa waliopatiwa matibabu ya magonjwa ya akili kutoka kwa wagonjwa 3,472 mwaka 2019 hadi 5,060 mwaka 2022, sawa na asilimia 31 ya wagonjwa,” inaeleza ripoti ya CAG.

Hali ya afya ya akili mwaka 2020 inakadiria mzigo wa maradhi ya akili umechangia kiwango cha vifo vya kujinyonga cha asilimia 8.15 kwa kila watu 100,000.

Vivyo hivyo, mwaka 2022 ripoti ya wizara hiyo ilikadiria mzigo wa maradhi ya akili umepanda kutoka wagonjwa 386,358 hadi  2,102,726 kuanzia mwaka 2012 hadi 2021 mtawalia, ambayo imeongezeka kwa asilimia 82.

Yaliyobainishwa na CAG

Matokeo ya ukaguzi uliofanywa na CAG yanaonyesha upungufu katika utoaji wa huduma za afya ya akili katika jamii, miongoni mwa hayo ni kukosekana kwa sera ya afya ya akili.

“Licha ya kuwepo na sheria iliyorekebishwa ya mwaka 2008 haikidhi ipasavyo mahitaji na changamoto za sasa kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili. Kutokuwepo kwa sera na sheria zilizopitwa na wakati kunazuia maendeleo na utoaji wa huduma bora za afya ya akili.”

CAG ametaja kuwepo na huduma duni za afya ya akili ni matokeo ya changamoto kubwa, kwani nyingi hazipatikani na hazifiki sehemu nyingi za nchi, pia kuwepo kwa unyanyapaa na imani za kitamaduni.

“Ufahamu kuhusu afya ya akili, ugonjwa wa akili na kukubalika kwa matibabu ya afya ya akili ni mdogo sana nchini Tanzania, hasa kutokana na unyanyapaa wa kijamii,” imeeleza ripoti.

Kuhusu ugunduzi katika ngazi ya jamii, CAG ameeleza kumekuwa na ukosefu wa umakini katika kutambua watu wenye changamoto, badala yake juhudi za utambuzi zinazingatia makundi mengine yenye udhaifu.

Amesema hali hiyo inachangia ukosefu wa fedha za kutosha kwa huduma za ustawi wa kijamii na uhaba wa maofisa wa ustawi wa jamii katika ngazi za chini za utawala.

CAG ameeleza huduma za kisaikolojia na kijamii hazijaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera na programu katika ngazi mbalimbali za utawala.

“Kuna uhaba mkubwa wa wataalamu, miundombinu, vifaatiba na dawa za kufanikisha utoaji wa huduma za afya ya akili. Uhaba huu unahusisha vituo vyote vya afya kutoka ngazi ya kitaifa hadi za kikanda na za wilaya,” amesema.

Ripoti inaeleza vituo vya afya vina upungufu mkubwa wa miundombinu ya kuhudumia mahitaji ya wagonjwa wa afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa wodi za kutosha kwa watu wazima, watoto na vijana.

Imeelezwa kuna ukosefu wa fedha na mipango ya ujenzi wa wodi kwa ajili ya wagonjwa wa afya ya akili.

Ripoti inaeleza kuwepo pengo kubwa katika upatikanaji wa dawa kwa wenye matatizo ya kisaikolojia, ikielezwa ni sehemu ndogo tu ya kiasi kinachohitajika kinachotolewa na maduka ya dawa.

“Upungufu huu unasababishwa kwa sehemu na kupata ugavi kutoka kwa wauzaji binafsi, lakini bado ni tatizo kubwa,” imeeleza ripoti.

Amesema ni mikoa michache yenye vituo vya urekebishaji kwa huduma za afya ya akili na vingi vipo mijini, hali inayoweka vizuizi kwa wagonjwa.

Baadhi ya vituo vya urekebishaji, amesema vipo katika hali mbaya, majengo yaliyooza na miundombinu duni, huku jamii za eneo hilo zikibadilisha matumizi ya nafasi hiyo kwa shughuli nyingine.

“Kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa urekebishaji wa huduma za afya ya akili nchini. Upungufu huu unatokana na kutokuwepo kwa mpango wa kuajiri, ili kuongeza uwezo katika eneo hili, hivyo kusababisha upatikanaji mdogo wa huduma za urekebishaji,” inaeleza ripoti.

Imeelezwa kuna upungufu wa kutokuwepo miongozo ya kawaida ya kubuni na kujenga vituo vya urekebishaji, mfumo wa matumizi ya kati kwa Wizara ya Afya hauonyeshi matakwa ya bajeti maalumu iliyotengwa na ukosefu wa uwiano katika huduma.


Mapendekezo ya CAG

Inapendekezwa Wizara ya Afya iandae miongozo ya kliniki ya kitaifa na taratibu za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuunda miundombinu ya urekebishaji kwa huduma za afya ya akili.

“Wizara ihakikishe kuna upatikanaji wa wafanyakazi wenye uwezo na vifaa muhimu kwa huduma za afya ya akili,” imependekezwa na CAG.

Amependekeza Ofisi ya Rais - Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutekeleza miongozo ya usaidizi wa kisaikolojia kwa ufanisi na kuhakikisha inawatambua wagonjwa katika ngazi za mitaa na kufuatilia matibabu yao.

“Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ihakikishe inafundisha na kuwezesha maofisa wa ustawi wa jamii na wafanyakazi wengine ngazi za jamii, ili kutambua na kuandikisha wateja wapya,” imependekezwa na CAG.

Amependekeza wizara kutoa miongozo ya wazi kwa utambuzi na usajili wa wateja.

Ripoti ya uchambuzi wa hali ya afya ya akili ya mwaka 2021 ilibainisha kuenea kwa magonjwa ya afya ya akili kama vile unyogovu, wasiwasi na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.

Ilikadiriwa watu milioni saba wanaishi na matatizo ya akili na utumiaji wa dawa za kulevya na zaidi ya milioni 1.5 waliathiriwa na matatizo ya unyogovu pekee, huku idadi kubwa ya walioathiriwa na matatizo ya unyogovu ni wanawake.

Kulingana na Mwongozo wa Kitaifa wa Kutoa Huduma za Utunzaji na Usaidizi wa Kisaikolojia (2020), ni muhimu kuhakikisha huduma hizo zinatolewa na watoa huduma walioongozwa vizuri, wenye ujuzi, na maarifa ya kutosha.


Maoni ya mtaalamu

Mtaalamu wa Saikolojia, Charles Kalungu amesema bado changamoto ni kubwa kwenye Taifa katika matatizo ya afya ya akili, akieleza suala hilo limesahaulika katika vipaumbele vya Serikali.

Amesema akili ikiwa haipo sawa mambo mengi yanaweza yasifanikiwe, hivyo kuna ulazima iwepo sera inayosimamia na kusukuma hilo, kwani hata dawa kwa wenye changamoto na usambazaji wake bado ni gharama.

Amesema wapo watu hawana shida kubwa ya kuhitaji dawa wanaweza kusaidiwa kupitia huduma ya ushauri.

"Serikali iangalie namna ya kuweka vituo maofisini, mtu anaweza kuwa anafanya kazi anaonekana mzima, akili yake ina shida kuna nafasi kubwa wengi wakasaidiwa na kunusuru matatizo ya afya zao za akili ili watu wasiangukie huko,” amesema.

Ameeleza pia hakuna vituo vya kutosha vya tiba zaidi ya Mirembe.

"Wataalamu wa saikolojia ni muhimu sana, wapewe nafasi kutekeleza kile wanachoweza kukifanya, wanatamani kuyafanyia kazi yale wanayoyajua, kada hii ipewe nguvu tunaamini saikolojia ni kazi kama zingine," amesema Kalungu. Pia amesema bado elimu inahitajika hasa vijijini.

"Mijini tunawafikia kwa sababu ni rahisi, huko vijijini kuna matukio mengi sababu hawana uelewa kuhusu masuala ya matatizo ya afya ya akili," amesema.