Kauli ya Mufti Zubeir kuhusu Muungano

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumanne Aprili 16, 2024. Kushoto ni mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Khamis Ngeluko. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Awaalika waumini wa dini ya Kiislamu kushiriki dua na maombi maalumu kwa Taifa.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikielekea kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mufti  wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amesema Waislamu wana kila sababu ya kujivunia mafanikio ya Muungano.

 Sheikh Zubeir amesema hayo leo Jumanne Mei 16, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwaliko uliotolewa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kushiriki dua na maombi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuliombea Taifa kwa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano.

Mwaliko huo amesema wameupata kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mufti Zubeir amesema dua itafanyika Aprili 22, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Mufti amesema miongoni mwa mambo wanayopaswa kujivunia ni uwepo wa mshikamano, amani na utulivu ndani ya nchi.

“Hivyo, Waislamu katika hili tunapaswa kujivunia mafanikio ya miaka 60, tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na rehema alizotujalia ndani ya miaka hii," amesema.

Amewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa uzalendo wa kuulinda na kuzitunza tunu za Muungano kama zilivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar.

Mufti Zubeir amewaalika viongozi na wauminu wa dini ya Kiislamu waliopo Mkoa wa Dodoma na wilaya zake zote, na mikoa jirani kushiriki kwa wingi kwenye tukio hilo ambalo yeye pia atashiriki.

Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, mwaka 1964 na tangu wakati huo zimekuwa kila mwaka zikifanya maadhimisho ya kumbukizi ya tukio hilo.