Mavunde azindua viwanda vya vipuri, matairi

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza vipuri vya migodini na viwandani na kiwanda cha kutengeneza tairi za magari vilivyopo eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Baada ya kuzindua kiwanda cha kutengeneza vipuri, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka wadau kuvitumia kuagiza na kununua vipuri vya mitambo yao.

Mwanza. Tatizo la kukosekana kwa vipuri vya mitambo ya migodini na viwandani limepata suluhu baada ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kuzindua kiwanda cha utengenezaji vipuri hivyo.

 Kwa sasa wachimbaji, wamiliki wa migodi na viwanda huagiza vipuri kutoka nje ya nchi, hali inayowafanya kutumia gharama kubwa ya ununuzi na usafiri, pia shughuli kukwama kwa muda kutokana na ukosefu wa kifaa husika.

Uzinduzi wa kiwanda hicho umeenda sambamba na uzinduzi wa kiwanda kingine cha utengenezaji na uundaji matairi ya magari ambavyo vyote vipo eneo la Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza na vinamilikiwa na Kampuni la JC Gear Group.

Akizungumza jana Januari 4, 2024 wakati wa uzinduzi wa viwanda hivyo, Mavunde amewataka wadau kuvitumia viwanda hivyo kuagiza na kununua vipuri vya mitambo yao, ili kupunguza gharama ya kuagiza vitu kutoka nje ya nchi.

"Serikali inaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji wazawa zaidi na hata wale kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanawekeza nchini, ili Watanzania wanufaike na uwekezaji huo. Pia Serikali na yenyewe iongeze mapato na kukuza uchumi kupitia uwekezaji huo na ndio maana unaona viwanda kama hivi vimeanzishwa na mzawa," amesema Mavunde.

Ujenzi wa viwanda hivyo ulianza mwaka 2022 unakadiriwa kutumia zaidi ya Sh3 bilioni.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni la JC Gear Group, James Makanyaga ametaja changamoto kubwa wanayokumbana nayo wamiliki wazawa  ni kushindwa kupata kazi au zabuni za migodini, hali inayowafanya kushindwa kujiendesha na kurejesha mikopo kwenye taasisi za fedha.

Hata hivyo, Waziri Mavunde akijibu kuhusu hilo amesema leo Januari 5, 2024 anatarajia kukutana na wadau wa madini nchini katika Mkoa wa Mwanza kuzungumza nao mambo mbalimbali ikiwemo changamoto hiyo.