Mtanzania ashinda tuzo ya kimataifa

Muktasari:

  • Wakati dunia ikiendelea kupambana katika kutokomeza umasikini, Mkurugenzi wa na Mwanzilishi wa taasisi ya Her Initiative ameshinda tuzo ya kimataifa, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kile anachokifanya kwa jamii.

Dar es Salaam. Uthabiti katika kukabiliana na umaskini na kuwezesha wasichana, wanawake na vijana kiuchumi imetajwa kuwa sababu ya Mtanzania, Lydia Moyo kutwaa tuzo ya Shirika la Kimataifa ya Global Citizen.

Global Citizen ni shirika la utetezi na uchechemuzi la kimataifa linalopigania kuondoa umaskini duniani, huku katika muongo mmoja, likiwa limetumia zaidi ya Sh112.7 trilioni ambayo imegusa maisha ya watu takriban bilioni 1.3 ulimwenguni.

Akizungumzia tuzo hiyo, Lydia ambaye ni mwanzilishi wa Shirika la Her Initiative amesema tuzo hiyo inathibitisha uimara na azimio la wanawake na wasichana vijana, ambao wana ndoto na malengo makubwa huku wakifanya kazi kwa bidi, ili kuboresha maisha.

Amesema kwa kutumia mikakati na mbinu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi, shirika lake linakusudia kuvunja mzunguko endelevu wa umaskini na kuimarisha uwezo wa kiuchumi kwa wasichana na wanawake vijana wa Kitanzania.

Amesema kiini cha mikakati yao ni uwezeshaji kiuchumi na uvumbuzi wa kiteknolojia, kama ilivyoonyeshwa na jukwaa la kielimu la Panda Digital.

“Jukwaa hili ni la kujifunza mtandaoni linalotumia Kiswahili limewawezesha zaidi ya wasichana na wanawake 5,000 kote Tanzania kupata ujuzi muhimu wa masoko na biashara, huku pia likiwawezesha kuunganishwa na fursa na mtandao muhimu kuanzisha na kukuza kwa biashara zao,” amesema Moyo.

Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Shirika la Her Initiative, Anna Kulaya amesema hamasa ya Lydia haina ufananisho na dunia inapaswa kuwaunga mkono viongozi wanawake wenye uthubutu kama yeye.

“Tunaposherehekea mafanikio yake tunapaswa kurudi nyuma na kuweka nia ya kuwa na juhudi za pamoja kufanya dunia iwe jumuishi, mahali ambapo watu wote, hasa wasichana na wanawake vijana wanawezeshwa kutimiza malengo yao,” amesema Kulaya.

“Nguvu zaidi ielekezwe katika kuwaunga mkono viongozi wanawake wenye uthubutu na ambao wanafanya kazi kubwa kuelekea kwenye dunia jumuishi na yenye usawa,” amesema.

Kupitia jarida la Global Citizen, Rais wa jarida hilo, Liza Henshaw amesisitiza umuhimu wa uongozi wa vijana katika kuleta mabadiliko halisi.

“Tushughulikie masuala muhimu zaidi ulimwenguni, tunahitaji kuwasaidia viongozi vijana wanaochukua hatua sasa, ni heshima kuwasherehekea watu hawa wa kipekee waliojenga njia, ambao wanajitolea maisha yao kuinua wale walio hatarini zaidi katika jamii zao za ndani na kusukuma harakati ya kukomesha umasikini duniani kote,” amesema Henshaw.

Washindi wa Tuzo ya Global Citizen mwaka 2024 watatambuliwa wakati wa mkutano wa ‘Global Citizen Now utakaofanyika Mei mosi na 2, 2024 jijini New York, Marekani.