Tahadhari kwa wanaotumia dawa holela, vinywaji vya kuongeza nguvu

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo

Muktasari:

  • Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Upimaji wa afya kwa jamii wa JKCI, Dk Pedro Pallangyo amesema matumizi holela ya dawa au vinywaji vya kuongeza nguvu  yanataharisha afya za watumiaji kwa kupata magonjwa ya moyo, kiharusi.

Iringa. Wakati matumizi holela ya dawa na vinywaji vya kuongeza nguvu yakiongezeka, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Palangyo amesema watumiaji wapo hatarini kupata magonjwa ya moyo.

  

Dk Palangyo amesema matumizi ya dawa za kuongeza nguvu yapo ya aina mbili, moja ikiwa ni nguvu za kiume na pili kuongeza nguvu za mwili.

Amesema wakati ushauri wa kitabibu ukitaka mtu anywe walau chupa mbili za vinywaji vya kuongeza nguvu kwa maana ya mills 250 kwa kila moja, wapo wanaokunywa kati ya chupa nne mpaka 10.

Dk Palangyo amesema hayo keo Aprili 16, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Madaktari bingwa kutoka JKCI wameweka kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanachi wa mkoa huo na maeneo ya jirani.

Amesema mtu anayetumia hovyo dawa au vinywaji hivyo ni rahisi kupata kiharusi, shinikizo la damu, mfuko wa umeme wa moyo kufeli ghafla na hata kifo.

"Tafiti zinaonyesha wanaotumia dawa au vinywaji hivi wengi hawafuati ushauri wa kitaalamu. Hii ni hatari sana kwa sababu mtu anaweza kupoteza maisha ghafla," amesema Dk Palangyo.

Amewataka watu wenye tabia hiyo kuacha matumizi holela na badala yake wapate ushauri wa kitaalamu, ili kuokoa afya zao.

Mmoja wa wagonjwa aliyefika hospitalini hapo kufanya uchunguzi, Beatus Saliba amesema kutokana kazi yake ya kuchimba mitaro kuwa ngumu, hutumia vinywaji vya kuongeza nguvu kwa wingi.

"Hii ni wiki ya tatu kichwa kinauma na nahisi mapigo ya moyo yanaenda kwa kasi. Kwa siku nilikuwa nakunywa mpaka chupa nane," amesema Saliba.


Mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia, Geoffrey Mgina amesema mfumo wa maisha ndio umeongeza matumizi makubwa ya dawa hasa za nguvu za kiume.

"Maisha yamekuwa magumu, kijana anajikuta anapata msongo wa mawazo kiasi kwamba akifika kwenye tendo la ndoa anahisi nguvu hana. Anaamua kubust na hapo ndio shida inapoanzia," amesema na kuongeza;

"Mwingine amejikita kwenye mazoezi magumu, chakula hafifu, hivyo anaamua kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu. Mfumo na tabia za maisha zimeleta magonjwa mengi yasiyoambukiza,” amesema.

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Pamoja Foundation, John Ihanu amesema badala ya kutumia dawa na vinywaji holela, ulaji mzuri unaweza kuongeza nguvu za mwili na hata nguvu za kiume.

"Mfano, mbegu za maboga zina vitutibisho vinavyoweza kuongeza nguvu za kiume, maziwa kwa mama anayenyonyesha na wazee zamani walitumia hivi vitu. Siku hizi maisha yamebadilika,” amesema.

Amesema ulaji mzuri unaweza kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, kwani mengi yanasababishwa na ulaji mbovu.