Vyama 11 vyamvaa Lissu, yeye asema amewakosoa marais wote hawakuhoji

Viongozi wa vyama 11 vya siasa Zanzibar wakiwa pamoja wakati wa kutoa tamko la kulaani kauli wanazodai za Makamu Mwenyekiti Chadema Tundu Lissu. Picha na Jessy Mikofu

Muktasari:

  • Vyasema haviungi mkono kauli hizo na wanazilaani kwa umoja wao, wakiwataka wananchi kupuuza kauli zake ambazo zinalenga kuwabagua.

Unguja. Vyama 11 vya siasa kisiwani Zanzibar vimemvaa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema- Bara), Tundu Lissu kutokana na kauli zake vikidai ni za kibaguzi na zinalenga kuvuruga Muungano na kuhatarisha amani.

Miongoni mwa kauli zinazodaiwa kuwa ni za kibaguzi ni pamoja na zile alizotoa hivi karibuni mkoani Manyara na Dodoma, akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kwamba yeye ni Mzazibari na anagawa rasilimali za nchi kwa sababu hana uchungu nazo.

Hata hivyo, Lissu amejibu akisema madai ya vyama hivyo hayana maana, kwani amekuwa akikosoa tawala zote kuanzia kwa Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli lakini hawakuwahi kuhoji.

Akisoma tamko la vyama hivyo leo Mei 6, 2024 Unguja, Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea Taifa, Juma Ali Khatib,  amesema kauli zilizotolewa na kiongozi huyo hivi karibuni katika majukwaa ya kisiasa ni kutaka kuvuruga umoja na mshikamano ulipo nchini.

“Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunapata shaka na kiongozi huyu kuhusu uzalendo wake katika Taifa hili,  kwani Watanzania hawana asili ya matusi na kudharauliana, bali wamejengwa katika misingi ya kuheshimiana,” amesema.

Pamoja na Ada Tadea, vyama vingine katika tamko hilo ni NCCR Mageuzi, Chama cha Demokrasia Makini, UPDP, TLP, Sau, DP, UMD, NLD, CCK na NRA.

Khatib ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, amesema: “Watanzania wamejengewa misingi ya uhuru katika nchi yao pasipo mipaka, Mzazibari kufanya kazi Tanzania Bara na Mtanzania Bara kufanya kazi Zanzibar hakuna kosa kisheria, hivyo kauli zake zinataka kuvuruga umoja.”

Amesema wao wakiwa viongozi wa vyama vya siasa,  hawaungi mkono kauli hizo na wanazilaani kwa umoja wao,  huku wakiwataka wananchi kupuuza kauli zake ambazo zinalenga kuwabagua.

Wametumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini pamoja na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,  kufanya uchunguzi wa kina juu kauli anazozitoa kiongozi huyo wa Chadema

Viongozi hao wa siasa wamependekeza, baada ya uchunguzi huo, ikithibitika, msajili wa vyama vya siasa  achukue hatua kwa mujibu wa sheria za vyama vya siasa na vyombo vya ulinzi na usalama vichukue hatua za kisheria.

Khatib amesema Rais Samia amefungua mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hivyo wanadi sera zao kwa wananchi na viongozi wa vyama wanayo nafasi ya kuikosoa Serikali katika njia za staha na ustaarabu na sio kuwachonganisha Watanzania.

Amesema ni wakati wa kuziishi kwa vitendo R4 alizosema Rais Samia ambazo ni maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Taifa, Haji Ambari Khamis, amesema hoja ya msingi ya vyama hivyo ni kujenga mustakabali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Kitendo cha kuanza kuchokonoa Muungano tena kwa kutumia lugha ambazo sio za kiungwana, wanasiasa tumeona ni jambo la msingi la kulitolea kauli ili lisiendelee kujitokeza maana linaweza kuhatarisha amani,” amesema.

Kwa mujibu wa Ambari, kuna mabadiliko ya mifumo kwenye sheria za uchaguzi ikiwemo kuunda Tume huru na kwamba zaidi ya asilimia 60 ya waliyokuwa wakiyataka  wamefanikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia.

Naye mwanaharakati huru wa haki za binadamu na utawala bora, Ali Makame Issa amesema amejiunga na watoa taarifa kutokana na kauli za kiongozi huyo kuonyesha kujenga uhasama.

Alichoksema Lissu

Alipotafutwa na Mwananchi kujibu hoja hizo Lissu amesema yeye ni miongoni mwa watu waliopigia kelele kuhusu Zanzibar kuminywa katika Muungano lakini hawakuwahi kusema chochote.

“Mimi nimefanya mikutano ya hadhara Unguja na Pemba nimezungumza matatizo ya Muungano jinsi ambavyo viongozi wa nchi hii walivyoiumiza Zanzibar, lakini hawakusema chochote kwa hiyo hizi kelele ni kwa sababu nimemkosoa Samia, sio kwa sababu ni ubaguzi,” amesema.

Kuhusu kuchukuliwa hatua iwapo ikithibitika, Lissu amesema haoni kosa linaloweza kumtia hatiani na anasimamia misimamo yake.