Wadau waja na mkakati kuongeza simu janja mtaani

Dar es Salaam. Wakati utafiti wa umiliki wa simu janja uliofanywa na Taasisi ya utafiti ya PEW ukionyesha Tanzania ni nchi ya mwisho kwa kumiliki aina hiyo ya simu kwa nchi kubwa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, wadau wa sekta ya mawasiliano wamezindua mkakati wa kupunguza tatizo hilo.

“Afrika Kusini inaongoza kwa umiliki wa simu janga kusini mwa jangwa la Sahara na Tanzania inashika mkia katika takwimu,”imesema sehemu ya utafiti huo ulioitwa Spring 2017 Global Attitude Survey uliochapishwa mwaka 2018.

Katika jitihada za kuongeza upatikanaji na matumizi hayo ili kuziba pengo la kidijitali nchini, kampuni za Vodacom Tanzania PLC na Benki ya CRDB wamezindua mpango wa kuwezesha Wateja wao kumiliki simujanja zenye ubora kwa gharama nafuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo wa kukopesha simu jijini Dar es Salaam, Machi 27, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema kampuni hiyo ya simu inatekeleza mipango mbalimbali ya kupunguza gharama za vifaa vya mawasiliano ili kuwawezesha wateja wake kuhama kutoka kwenye matumizi ya mtandao wa 2G na kumiliki simu zenye uwezo wa 4G na kutumia fursa hiyo ili kunufaika na faida kemkem zinazopatikana kupitia mtandao huo.

"Tukiwa ni mdau na mshirika mkubwa wa sekta ya mawasiliano na teknolojia, Vodacom tunajivunia kuzindua mpango huu na Benki ya CRDB ambayo ni taasisi kubwa ya fedha nchini. Ushirikiano wetu unalenga kuwawezesha wateja kutoka pande zote mbili kupata aina mbalimbali za simujanja kwa bei nafuu na mpango wa malipo kwa awamu kwa kipindi Fulani,”amesema Besiimire.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema, “ushirikiano huu baina yetu na Vodacom ni fursa nzuri kwa Watanzania kupata huduma za kifedha na mawasiliano kwa gharama nafuu. Kwa hiyo kama wadau muhimu tunapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuhakikisha wananchi wake wanafaidika na ukuaji na maendeleo katika sekta hizi.”

Nsekela ameongeza kuwa, “Kwa mtandao wetu ulioenea nchi nzima, CRDB tumekuwa na mchango muhimu katika maendeleo ya Watanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha. Hivyo basi, kwa kushirikiana na Vodacom, tutaweza kutoa mchango wetu ili kuongeza matumizi ya simujanja nchini.”

Justin Msengi, ambaye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Habari amesema simujanja ambazo hutumia intanenti ni muhimu katika uchumi wa sasa kwani shughuli zote hufanyika huko.

“Matumizi ya simujanja na intaneti yana faida kwa jamii kama vile kukuza ukuaji wa kiuchumi kwa kuwezesha ujasiriamali wa kidijitali na kuchochea uvumbuzi, utafutaji masoko mitandaoni pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi wanaoamua kujiajili kupitia dijitali.

Nsekela alimalizia kwamba anaamini kuwa taasisi hizo mbili zina huduma mbalimbali za kibunifu ambazo zitawanufaishana kuboresha maisha ya wateja wao.