Wawili kortini kwa kukutwa na nyara za Serikali

Muktasari:

  • Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa Desemba 23, 2022 eneo la Malamba Mawili, wilaya ya Ubungo, ambapo walikutwa na jumla ya vipande 45 yakiwemo meno mazima ya tembo.

Dar es Salaam. Damas Mapunda (34) na Method Kusogo (43) wamefikishwa katika Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka ya kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh735.21 milioni kinyume na sheria.

Washtakiwa hao ambao ni wakazi wa jiji hilo, wamefikishwa mahakamani hapo leo, Aprili 19, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye shitaka moja

na wakili wa Serikali, Pancransia Protas mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.

Akiwasomea shitaka hilo, wakili Protas amedai Desemba 23, 2022 katika maeneo ya Malamba Mawili Wilaya ya Ubungo, washtakiwa wanadaiwa kukutwa na vipande 30 vya meno ya tembo.

Pia imedaiwa kuwa siku  na eneo hilohilo  wanadaiwa walikutwa na meno mazima 15 ya tembo bila kuwa na kibali cha  Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Baada ya kusomewa shitaka hilo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha kesi ya uhujumu uchumi, isipokuwa kwa kibali maalumu.

Wakili Protas ameieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa

Wakati hayo yakiendelea,  mshtakiwa Kusogo alinyanyua mkono juu akiashiria kuwa anaomba Mahakama impe nafasi ya kuongea.

Hata hivyo alivyopewa nafasi hiyo, aliomba upande wa mashitaka waharakishe kukamilisha upelelezi wa kesi ili waweze kujua hatima ya kesi hiyo.

Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza maelezo hayo, amesema kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ndivyo hivyohivyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kosa hilo.

Aliwataka washtakiwa hao kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa ndio yenye mamlaka ya kutoa dhamana.

Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 2, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.