Shangingi lililosafirisha wahamiaji haramu Manyara lataifishwa

Muktasari:

  • Wakati gari hilo likitaifishwa, Waethiopia 17 wamehukumiwa kulipa faini ya Sh500, 000 au kifungo miaka miwili jela na gari lililotumika kuwasafirisha limetaifishwa.

Babati. Gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 VXR maarufu kama Shangingi lililotumika kuwabeba Waethiopia 17 walioingia nchini bila vibali na kutelekezwa Babati mkoani Manyara, limetaifishwa huku wahamiaji hao wakitakiwa kulipa faini ya Sh500, 000 kila mmoja au kwenda jela miaka miwili.

Aprili 7, 2024, gari hilo lilikamatwa eneo la Kiongozi mjini Babati baada ya dereva kusimama na kutoroka akiwatelekeza wahamiaji hao baada ya kukaidi kusimama kwenye kizuizi cha Polisi kilichopo Minjingu.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati, Juma Mwambago ametoa hukumu hiyo leo Aprili 19, 2024 baada ya kukubaliana na ushahidi uliowasilishwa na Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Yohana Malima na mawakili wa Polisi.

Gari hilo lilipokamatwa lilikuwa na namba mbili za usajili ikiwemo namba za Serikalina za binafsi ambazo zimebainika ni za kughushi.

Hilo ni gari la pili kutaifishwa na Mahakama hiyo baada ya lingine aina ya Toyota Land Cruiser V8 VXR lililokamatwa likipeperusha bendera ya CCM, likiwa na Waethiopia 20.

Gari hilo lilikamatwa Machi 23, 2024 likiwa limetoka nchi jirani kupitia mkoani Kilimanjaro, likiwa safarini kwenda Afrika Kusini kupitia mikoa ya Dodoma na Mbeya.

Raia hao 20 wa Ethiopia walikamatwa na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kwenda jela miaka miwili.

Huko Iringa, wahamiaji haramu 16 pia raia wa Ethiopia walihukumiwa adhabu kama hiyo na gari lililotumika kuwasafirisha aina ya Land Cruiser V8, linalodaiwa kuwa ni mali ya mkazi wa Tabata, Dar es Salaam likataifishwa.