Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zali jingine la Mzize ambalo Gen Z hawawezi kulijua

HISIA Pict


MUDA mrefu tumemkosa Clement Mzize uwanjani. Ameumia. Hatujui atarudi kuwa fiti uwanjani lakini huwa tunamuona mitandaoni akiwa anafanya mazoezi mepesi. Inaonekana hayupo mbali na kurudi uwanjani.


Ana miezi kadhaa sasa nje ya uwanja. Nikaamua kudadisi kilichoendelea kati yake na Yanga. Kimya kimya nikawatafuta baadhi ya watu wangu walio ndani ya Yanga. Nilitaka wajibu maswali yangu ambayo miaka ya nyuma yangekuwa maswali magumu, siku hizi ni maswali mepesi.


Nikaambiwa kwanza kabisa alienda Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutibu jeraha lake lililokuwa linamsumbua. Awali Mzize alikuwa anasita kufanyiwa operesheni. Alijaribu kurudi uwanjani na hapo hapo akaumia tena. Kilichofuata kilikuwa ni operesheni.

Alienda Afrika Kusini na mmoja kati ya madaktari wa Yanga kwa ajili ya kufanyiwa operesheni. Inamaanisha nini? Timu zetu siku hizi zinajitutumua. Hatuangalii upande huu na kuvisifu vilabu hasa hivi vitatu vikubwa. Simba, Yanga na Azam. Zimekuwa zikipeleka wachezaji wake kutibiwa nje. Tumetoka mbali.

HISI 01

Zamani mchezaji alikuwa akiumia basi shauri yake. ikishindikana kutibiwa Muhimbili basi shughuli inakuwa imeishia hapo. Wachezaji wengi wa zamani walikatisha maisha yao ya soka kwa majeraha ambayo yangeweza kutibika Afrika Kusini, Morocco au Uturuki. Kweli tumetoka mbali.

Jambo jingine ambalo limenifanya nishike kalamu na penseli kuandika hili ni kwamba watu wa Yanga wanamlipa Mzize mshahara wake kama kawaida. Na hapo hapo nikaambiwa kwa sasa Mzize analipwa mshahara mkubwa kuliko Djigui Diarra, Pacome Zouzoua na Maxi Nzingeli. Analipwa vizuri pia kuliko Star Boy, Allan Okello.

Nikaambiwa kwamba licha ya kuwa majeruhi Mzize amekuwa akipatiwa bonasi zake zinazotokana na ushindi wa mechi za Yanga licha ya kwamba hapewi kiasi kile kile kama wachezaji waliovaa jezi. Bado ni ushindi mkubwa kwake.

HISI 03

Tumezoea kuwaongelea vibaya mabosi wa timu zetu. Inawezekana na wachezaji wa timu nyingine kubwa wanafanyiwa haya wanapokuwa majeraha lakini hili la Mzize nilihitaji Ushahidi kidogo ikiwa sehemu ya uchunguzi wa namna ambavyo klabu zetu zinajali wachezaji wao tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kwa Mzize hii ni Bahati. Unaanzia katika bahati ya namna ambavyo kipaji chake kilitoka katika udongo mpaka kufikia kuwa dhahabu. Kuanzia kuwa dereva wa bodaboda hadi kufikia kuwa mchezaji staa wa Yanga. Ni juhudi na Bahati.

Na sasa unaangalia namna ambavyo timu zetu zinaishi maisha tofauti na yale ambayo walikuwa wanaishi wakati ule Wenyeviti wa hizi timu wakiwa akina Rashid Ngozoma Matunda, Ali Bamchawi, Hassan Hazali na wengineo. Maisha yalikuwa magumu kwa wachezaji.

HISI 02

Watoto wa Gen Z hawawezi kuelewa. Kwa kuanzia tu mchezaji kama Mzize kama nilivyosema kwa asilimia kubwa ndio ingekuwa mwisho wake wa kucheza soka. Tunawajua wachezaji wengi walioshia njiani kwa majeraha ya kawaida kabisa.

Akina Ngozoma Matunda wasingeweza kumpeleka nje mchezaji nje ya nchi kwa kutegemea viingilio vya mashabiki peke yake pale Shamba la Bibi. Kiasi hicho hicho cha pesa wachezaji walipaswa kugawana na timu ilipaswa kuchukua mgawo wake kwa ajili ya kujiendesha.

Kumpeleka mchezaji nje ya nchi lingekuwa jambo la anasa. Mchezaji ambaye aliwahi kutushangaza zamani kwa Kwenda kutibiwa nje alikuwa ni beki wa Yanga, John Mwansasu ‘Nyauba’. Alienda kwa pesa zake binafsi. Mama yake alikuwa anafanya nzuri pale Uswisi. Wengine maisha yao ya soka yaliishia hapa hapa nchini.

HISI 04

Kitu kingine ambacho kisingewezekana kwa Mzize wa wakati huo ni kugawana bonasi au viingilio na wachezaji wenzake. Nimewahi kushuhudia kwamba wachezaji ambao walikuwa wanacheza au wamevaa jezi walikuwa wakali pesa zao kupelekwa kwa wachezaji wasiocheza hata kama walikuwa na majeraha.

Ambacho walau kingeweza kuwa hisani kwa wachezaji wenye majeraha ni kwa wachezaji wenyewe kuamua kuchanga kupitia pesa ambazo tayari wameshapewa katika mgawo wao wa getini na viongozi. Mchezaji ambaye hakujisikia kuchanga asingechanga.

Leo suala la bonasi linatoka moja kwa moja kwa mabosi wa timu Kwenda kwa wachezaji. Hakuna mchezaji anayejali sana kama Mzize anapewa bonasi licha ya kutocheza kwa sababu kila mchezaji kivyake anapata stahiki zake na hana sababu ya kuwa na husda kwa mwenzake.

HISI 05

Sijazungumzia kuhusu mshahara. Wachezaji zamani hawakuwa na mishahara ambayo akina Mzize. Sio kwamba hawakuwa hawana mishahara mikubwa, Hapana, hawakuwa na mishahara kabisa. Mchezaji alikuwa anasaini katika fomu ya usajili kisha anapewa kiasi Fulani cha pesa na baada ya hapo anaishi kwa posho pamoja na viingilio vya getini. Tumetoka mbali.

Mara nyingi nawasikiliza wachambuzi wetu wengi huwa wanaongea zaidi vitu hasi kuhusu mpira wetu na timu zetu. Wengi huwa nawalewa kwa sababu hawakuishi katika zama za giza za mpira wetu. Nawashangaa zaidi wale ambao ni wakongwe na hawaoni vitu chanya katika mpira wetu.

 Nimeamua tu kuigusia hii kwa sababu ya Gen Z. Fasihi andishi wakati mwingine ina jukumu kubwa la kutunza kumbukumbu kwa ajili ya kupasisha kwa vizazi vijavyo. Watu wajue tulikotoka na tunakoelekea.

Maisha hayakuwa rahisi hivi. Na kama viongozi wetu wataendelea kupambana sana basi maisha yanaweza kuwa rahisi zaidi kwa Mzize ajae. Na haipaswi kuwa katika timu kubwa tu, hata katika timu ndogo.

Na katika ukweli halisi hata timu ndogo ya leo sio kama timu ndogo ya zamani. Na ninachoweza kugusia tu ni kwamba hata maisha ambayo Namungo wanaishi leo ni maisha ya anasa sana kuliko ambayo akina Edibily Lunyamila waliishi miaka ya tisini.