Jeanine, Shikangwa katika vita ya kiatu WPL
Muktasari:
- Simba Queens imekabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa mzunguko wa 20 kutamatika na kuifanya timu hiyo kucheza michuano ya Cecafa kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.
KAMA ulikuwa unajua Ligi Kuu ya Wanawake imetamatika baada ya Simba Queens kukabidhiwa kombe lao basi nikupe pole, kuna ligi nyingine ya mfungaji bora imeshika kasi.
Simba Queens imekabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa mzunguko wa 20 kutamatika na kuifanya timu hiyo kucheza michuano ya Cecafa kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.
Sasa wakati Simba inachukua taji hilo na kuandika rekodi ya kuwa timu pekee iliyobeba taji hilo mara nyingi ikichukua mara tano kuna vita ya mfungaji bora haijamalizwa inasubiriwa hadi mwishoni mwa msimu.
Anayeongoza hadi sasa kwa ufungaji bora ni mshambuliaji wa Yanga Princess, Jeanine Mukandayisenga mwenye mabao 20 anayemfuata ni Jentrix Shikangwa wa Simba Queens mwenye mabao 16.
Imesalia mechi moja kutamatisha msimu wa 2025/26, na Mukandayisenga anayeongoza orodha hiyo alipewa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya JKT Queens ambayo aliisawazishia timu hiyo bao moja dakika za jioni na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare ya 1-1.
Sasa ikiwa imesalia mechi moja kama Shikangwa atafunga mabao matano dhidi ya Geita Queens anaweza kubadilisha upepo wa kiatu baada ya kukosekana Mukandayisenga ambaye ni msimu wake wa pili kuitumikia Yanga.
Akizungumzia ushindani huo Shikangwa alisema "Mimi napambana kwa sababu ya timu hata nikifunga sababu ya kusaidia timu kisha mimi binafsi kwahiyo huwa sizingatii sana ushindani ingawa ni mzuri,"
Kwa upande wa Mukandayisenga alisema :"Natamani nichukue kiatu cha ufungaji bora kwa sababu ni kitu nimekipambania muda mrefu tangu msimu uliopita nilimaliza nafasi ya tatu."