Loemba ataka mataji Simba
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Loemba alisema tayari ameonja ladha ya ubingwa baada ya kutwaa taji moja la Muungano akiwa na Simba, lakini bado anaamini kikosi hicho kina nafasi ya kuongeza mengine mawili yaliyosalia ya Ligi Kuu na Kombe la FA.
KIUNGO wa Simba, Inno Loemba, amesema ameanza vizuri maisha yake ndani ya kikosi hicho tangu alipojiunga akitokea Colombe ya Cameroon, huku akitamani msimu wake wa kwanza Msimbazi uwe wa mafanikio makubwa kwa timu na kwake binafsi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Loemba alisema tayari ameonja ladha ya ubingwa baada ya kutwaa taji moja la Muungano akiwa na Simba, lakini bado anaamini kikosi hicho kina nafasi ya kuongeza mengine mawili yaliyosalia ya Ligi Kuu na Kombe la FA.
“Nina furaha kuwa sehemu ya Simba. Ni msimu wangu wa kwanza na tayari nimepata kombe moja, lakini bado tuna malengo makubwa ya kupigania mataji mengine yaliyobaki,” alisema Loemba.
Nyota huyo alieleza kuwa pamoja na mafanikio ya timu, anatamani pia kuwa na msimu mzuri kwake binafsi kwa kuchangia takwimu bora zitakazosaidia Simba kufikia malengo yake.
“Kila mchezaji anatamani kuwa na takwimu nzuri. Nami nataka kutoa mchango wangu mkubwa ndani ya uwanja ili kusaidia timu kufikia mafanikio zaidi,” alisema.
Loemba alisema alipojiunga Simba alijua anakwenda kwenye moja ya klabu kubwa Afrika, jambo ambalo limempa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuendana na matarajio ya mashabiki na benchi la ufundi.
“Simba ni timu kubwa yenye historia kubwa. Nimekuja hapa kuongeza ushindani na kujifunza zaidi, lakini pia kupambana ili kupata nafasi na kuisaidia timu,” alisema.
“Ushindani ndani ya timu ni mkubwa, lakini hilo ni jambo zuri kwa sababu linamfanya kila mchezaji kupambana na kutoa kiwango chake bora."
Tangu Loemba amejiunga na Simba amecheza mechi 13 za Ligi Kuu, mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika bila kufunga bao.