Luke Shaw kukatwa mshahara Man United
Muktasari:
- Shaw mwenye umri wa miaka 30 anaingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa sasa, ambao hauna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
LONDON, England: BEKI Luke Shaw atalazimika kukubali kupunguziwa mshahara ikiwa anataka kusaini mkataba mpya na Manchester United.
Shaw mwenye umri wa miaka 30 anaingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake wa sasa, ambao hauna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Kwa sasa, beki huyo wa kushoto analipwa pauni 200,000 kwa wiki, lakini Manchester United hawatarajiwi kumpatia mkataba mpya wenye kiwango hicho cha mshahara.
Shaw atakuwa na umri wa miaka 32 kabla ya kuanza kwa msimu wa 2027-28, na tayari United wanatafuta beki wa kushoto wa muda mrefu wa kurithi nafasi hiyo siku zijazo.
Hata hivyo, Shaw alikuwa na msimu bora wa 2025-26, ambapo alikuwa mchezaji wa tano kuanza katika mechi zote 38 za ligi kwa Manchester United ndani ya msimu mmoja.
Anaweza kupewa mkataba kama wa Maguire
Iwapo United wataamua kumbakiza Shaw, huenda wakatumia mfumo uliotumika kwa Harry Maguire mwezi Aprili.
Katika makubaliano hayo, mshahara wa msingi wa Maguire ulipunguzwa kutoka pauni 200,000 kwa wiki. Hata hivyo, kufuzu kwa Manchester United katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa pamoja na bonasi mbalimbali kulimpa nafasi ya kupata mapato makubwa zaidi kwa ujumla.
Mkataba wa Maguire ulikuwa wa mwaka mmoja na ulijumuisha chaguo la kuongeza mwaka mwingine.
Mchezaji aliyedumu zaidi United
Shaw alijiunga na Manchester United kutoka Southampton FC kwa ada ya pauni31 milioni mwezi Juni 2014.
Kwa sasa ndiye mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika kikosi cha United.
Nyota huyo ambaye amefika fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya mara mbili akiwa na England, alimaliza msimu uliopita bila kupata jeraha lolote, jambo lililotokea kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka akiwa United.
Katika misimu 12 aliyocheza Old Trafford, Shaw amecheza jumla ya mechi 325, wastani wa mechi 27 kwa kila msimu.
Hata hivyo, ameshindwa kufikisha mechi zaidi ya 20 katika misimu sita tofauti kutokana na matatizo ya majeraha yaliyokuwa yakimsumbua mara kwa mara.