Ushindi wa Perez... Jose Mourinho, Olise haooo Real Madrid
Muktasari:
- Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, alisaini mkataba wa miaka mitatu mwezi uliopita ili kuwa kocha mkuu wa Real Madrid, lakini mkataba huo ungeanza kutumika tu iwapo Perez angeendelea kubaki madarakani.
MADRID, HISPANIA: JOSE Mourinho anatarajiwa kuthibitishwa rasmi kuwa kocha mkuu mpya wa Real Madrid baada ya Florentino Perez kuchaguliwa tena kuwa rais wa klabu hiyo hadi mwaka 2030.
Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, alisaini mkataba wa miaka mitatu mwezi uliopita ili kuwa kocha mkuu wa Real Madrid, lakini mkataba huo ungeanza kutumika tu iwapo Perez angeendelea kubaki madarakani.
Perez, mwenye umri wa miaka 79, ambaye alipata asilimia 65 ya kura, amekuwa madarakani tangu mwaka 2009 na alitangaza kuitishwa kwa uchaguzi huo katika mkutano maalum na waandishi wa habari mwezi uliopita.
“Tumeshinda uchaguzi na tutaendelea kufanya kazi ili kuendelea kutwaa mataji,” alisema Perez. “Bado niko hapa na niko hapa kuilinda Real Madrid.
“Tutaendelea kufanya kazi kuhakikisha Real Madrid inaendelea kushinda mataji, na tutapambana hadi mwisho ili kutwaa Kombe la 16 la Ulaya.
“Tutaendelea kujivunia Uwanja wa Santiago Bernabeu, kama uwanja bora zaidi duniani.
“Ninajivunia kuwa na wachezaji bora zaidi duniani, ninajivunia kumkaribisha tena mmoja wa makocha bora zaidi duniani, Madridista kama Jose Mourinho. Nawahakikishia, nikiwa rais, Real Madrid imekuwa, ni, na itaendelea kuwa mali ya wanachama wake daima.”
Wiki iliyopita, Perez alizua mjadala baada ya kusema kuwa anataka kuisukuma klabu kufanya usajili wa thamani ya euro150 milioni ili kuirejesha timu katika njia ya mafanikio na ushindi.
Ingawa Perez alikanusha kwamba mchezaji aliyekuwa akimzungumzia ni nyota wa Bayern Munich, Michael Olise, vyombo visivyopungua vitatu vya habari viliripoti kuwa alikuwa akijaribu kupotosha umma na kuficha mipango yake halisi. Kwa mujibu wa taarifa hizo, Perez bado ana nia ya kweli ya kumsajili Olise na kumleta Real Madrid.
Mbali ya Mourinho, Olise pia bilione huyo aliwataja Ibrahima Konate na Denzel Dumfries, ambao wote walithibitishwa wakati wa kampeni.Hata hivyo, bado anahifadhi tangazo la usajili mmoja mkubwa wa aina ya “Galáctico”, ambao ameahidi kuufichua leo Jumanne.
Katika uchaguzi wa urais wa Real Madrid uliogusa hisia za wengi Perez alimshinda Enrique Riquelme.
Ushindi wa mfanyabiashara huyo wa Madrid ulithibitishwa muda mfupi baada ya saa 6:30 usiku wa manane, kama ilivyotabiriwa na tafiti nyingi za maoni, ingawa ulilazimika kuthibitishwa rasmi kutokana na ushindani mkubwa wa mpinzani wake, ambaye sasa ameonekana kuwa mbadala imara wa baadaye kwa nafasi ya urais wa klabu hiyo.
Kama ilivyoripotiwa na Bodi ya Uchaguzi muda mfupi baada ya saa 8:00 usiku wa manane, baada ya kura zote kuhesabiwa, tiketi iliyoongozwa na Florentino Perez ilipata kura 21,741, sawa na asilimia 65 ya kura halali. Wakati huo huo, mgombea Enrique Riquelme alipata kura 11,814, sawa na asilimia 35.
Uchaguzi utasubiri angalau hadi mwaka 2030, pale muhula uliorefushwa wa Perez utakapoisha. Rais huyo wa Real Madrid, ambaye ameiongoza klabu hiyo tangu mwaka 2000 isipokuwa kipindi cha 2006 hadi 2009.
Uchaguzi wa Jumapili hii ni ushindi wa tatu wa Florentino Perez katika uchaguzi wa Real Madrid. Jaribio lake la kwanza mwaka 1995 lilishindwa dhidi ya Ramon Mendoza, lakini mwaka 2000 alimshinda Lorenzo Sanz kwa kupata asilimia 55 ya kura, huku kura za posta zikichangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo. Mwaka 2004 alishinda tena kwa kishindo, akipata zaidi ya asilimia 90 ya kura.
Tangu kurejea klabuni mwaka 2009 baada ya kuondoka kwa utata kwa Ramon Calderon ambaye Florentino amehusisha na kampeni ya Riquelme. Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa kwanza ambao alilazimika kushindana. Mwaka 2009 hakupata mpinzani, na hali hiyo ilijirudia katika uchaguzi wa 2013, 2017, 2021 na 2025, ambapo hakukuwa na wagombea wengine hivyo hakuna kura zilizopigwa.