Prime
‘Mzimu wa Bangala’ kumng’oa mmoja Yanga
WAKATI dirisha la usajili likiendelea kupamba moto, mabosi wa Yanga wameanza harakati za kusaka kiungo mkabaji wa kigeni mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbili kwa wakati mmoja, akifanya kazi ya kiungo wa ulinzi na pia kushuka kucheza beki wa kati pale inapohitajika.
Iko hivi, Yanga inahesabu kali za kupata mchezaji mwenye sifa zinazofanana na zile za aliyekuwa nyota wao, Yannick Bangala, ambaye aliwahi kuwa tegemeo kubwa kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja ndani ya kikosi.
Inaelezwa benchi la ufundi la timu hiyo linaamini kupata mchezaji wa aina hiyo kutawaongezea nguvu katika eneo la ulinzi na kiungo, huku likitoa nafasi ya kufanya mabadiliko ya kiufundi bila kuathiri uwiano wa timu wakati wa mechi.
Taarifa za ndani ya klabu hiyo zilieleza kuwa tayari majina kadhaa ya viungo wa kigeni yanafanyiwa kazi na endapo watampata mchezaji anayekidhi mahitaji yao, huenda wakafikia uamuzi wa kuachana na beki Frank Assinki ambaye mustakabali wake ndani ya kikosi hicho unaendelea kuwa wa mashaka.
“Yanga wanataka kiungo mkabaji ‘holding’ wa kigeni mwenye uwezo wa kucheza pia kama beki wa kati, mtu wa aina ya Bangala. Hilo ndilo eneo linalopewa kipaumbele kwa sasa. “Usajili huo ukikamilika, nafasi ya Assinki ndani ya kikosi inaweza kuwa ndogo na klabu ikaamua kufanya maamuzi mengine kulingana na mipango ya msimu ujao.”
KINACHOMUONDOA ASSINKI
Ikumbukwe kuwa, beki huyo Mghana alitua Yanga msimu huu akitoka Singida Black Stars ambako alitolewa kwa mkopo wa msimu mmoja, hivyo mwishoni mwa msimu huu anamaliza safari yake ndani ya Jangwani akiwa hajapata nafasi ya kutosha kwenye timu hiyo. Tangu atue Yanga Assinki amekutana na ugumu wa nafasi kutokana na uwepo wa mabeki watatu wa kati Dickson Job, Bakari Nondo Mwamnyeto pamoja na Ibrahim Bacca ambao wamekuwa kwenye kiwango cha juu kwenye michezo yote ambayo wameitumikia timu hiyo kwa misimu kadhaa.. Katika mechi 25 ambazo Yanga imecheza ni 11 tu ambazo Assinki amepata nafasi ya kucheza, kwa sababu ya Dickson Job kupata jeraha la goti linalomfanya akose mechi zote za msimu huu.
Licha ya kupata muda huo wa kucheza, lakini bado Yanga haijaridhishwa na kiwango chake, huku akiweka rekodi ya kuruhusu mabao mawili pekee katika mechi zote alizokuwa uwanjani.
Yanga imekuwa ikifanya maboresho katika maeneo mbalimbali ya kikosi chake kwa lengo la kuendelea kuwa na ushindani mkubwa kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa, huku benchi la ufundi likihitaji wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi ili kuongeza nguvu ndani ya timu.