Prime
Mwamnyeto apewa mbinu Yanga
WATAALAMU wa saikolojia na wadau wa soka wameamua kumkingia kifua nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto baada ya tukio la beki huyo kujifunga dhidi ya Dodoma Jiji katika kichapo cha mabao 3-2, hali iliyofanya kushambuliwa katika mitandao ya kijamii na mashabiki, huku wakitoa mbinu ya kukabiliana na ishu hiyo.
Mwamnyeto aliyeitumikia Yanga kwa msimu wa sita sasa tangu 2020 akitokea Coastal Union ya Tanga, katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Mei 13, 2026, alijifunga dakika ya 29 akiwa katika haraka za kuokoa shambulizi lililopigwa na William Edgar.
Tukio hilo limezua minong’ono mingi, ingawa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alilizungumzia: “Mwamnyeto amekosekana mechi dhidi ya JKT Tanzania (Kombe la FA) kwa sababu hayupo sawa kiakili, nifikishe ujumbe kwa wanachama wa Yanga, hakuna mchezaji anaweza akatoka kwenda uwanjani ili kuifunga timu, ni makosa yanatokea kwa bahati mbaya.
“Baada ya mechi ya Dodoma Jiji, alipokea ujumbe mwingi katika simu yake hadi ikaingizwa familia yake, hivyo akazungumza na benchi la ufundi na wachezaji wenzake ili asicheze dhidi ya JKT Tanzania ajiandae na mechi nyingine inayokuja mbele.”
Wakati Kamwe akisema hayo, mtaalamu wa saikolojia, Lusajo Kajuna alisema jambo la kwanza mchezaji anapopitia changamoto kama hiyo, anapaswa kujisamehe na waajiri wake wamsaidie kumlinda dhidi ya mashabiki na kumtafutia mtaalam wa saikolojia.
“Hakuna kosa jipya, kila binadamu anaweza akakosea, mfano tukio la Mwamnyeto yeye siye wa kwanza kujifunga na hatakuwa wa mwisho,” alisema Lusajo aliyefanya kazi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa miaka 18 na sasa ana taasisi yake.
Alisema: “Ninachoweza kuzishauri klabu za Ligi Kuu Bara, ziingie mikataba na hospitali zenye wataalamu tofauti, ili inapotokea mchezaji kapata changamoto anapelekwa moja kwa moja kwa mtaalamu husika na siyo kubahatisha.”
Mwanasaikolojia mwingine anayejulikana kwa jina la Charles Nduki, alisema: “Wachezaji kama binadamu wanapitia vitu vingi nje ya uwanja, ambavyo vinaweza vikasababisha afanye makosa ya kiufundi, jambo la msingi linapotokea hilo, viongozi wasiende na hisia za mashabiki, bali wawe msaada kwa mchezaji kutojisikia vibaya, mchezaji mwenyewe ajitahidi kukabiliana na changamoto na asijisikie yeye ndiye wa mwisho kufanya makosa, yanafanyika kila siku na huko Ulaya, lakini makocha wanawasaidia kuwaweka sawa na katika mabenchi ya ufundi wapo wataalamu wa saikolojia.”
Kocha wa zamani Azam FC, Meja mstaafu wa jeshi, Abdul Mingange, alisema wachezaji wanapitia mambo magumu nje ya uwanja, ambayo wakikosa mtu wa kuwasaidia yanaweza yakawatoa mchezoni na maisha yao kuharibika kiuchumi.
“Wakati naifundisha Lipuli, kuna mchezaji mmoja alinifuata akanipa simu yake nisome ujumbe alikuwa ameandika mkewe na ukubwa wangu wote sikuwahi kuona mwanamke anayemwandikia mume wake maneno mazito na mabaya kiasi kile, nikamtia moyo kisha nikamruhusu akatengeneze na mwenzake, mchezaji kama huyo ukimpanga mechi na kama hajakwambia changamoto lazima atafanya vibaya uwanjani, wakati mwingine akasababisha kadi,” alisema.
Mwamnyeto siyo mchezaji wa kwanza kufanya kosa, iliwahi kumtokea aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi kukosa penalti ya kuipa timu hiyo ushindi dhidi ya Al Ahly nchini Misri ikiwa ni mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka 2014, tukio hilo lilimpitisha katika nyakati ngumu kama anavyosimulia.
“Nilipigiwa simu na familia yangu wakati bado tupo Misri kunijulisha mashabiki wamekwenda nyumbani kufanya fujo, niliwaomba wasitoke nje, baada ya kufika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julias Nyerere, nilinyamaza kimya na kuomba Mungu, nilijihisi mkosaji nisiyestahili, roho ya kutamani kuacha soka ilinivaa, kiongozi aliyenisaidia wakati huo ni Hussein Ndama alinijenga kiakili na kuniambia haikuwa riziki yako, himili mtikisiko unaokupata baada ya hapo alinipa Dola 500, aliona wenzangu walivyokuwa wanapewa pesa na mashabiki halafu mimi wakawa wananibagua,” alisema Banahuzi na kuongeza;
“Siku ya mazoezi mashabiki walijaa uwanjani, kuna shabiki mmoja aliniita na kutaka nitoke uwanjani nikatii, akanipeleka katikati ya mashabiki wengine, akawauliza huyu nani wakaitikia Bahanuzi, hapo nilikuwa natetemeka na mwili kuvuja jasho, akawauliza tena tumsamehe au tusimsamehe, wakajibu tumsamehe, kisha wakaniruhusu nikaendelee na mazoezi, kusema ukweli kukosa hiyo penalti ikawa mwanzo wa nuksi kwangu kutong’ara tena,” alisema Bahanuzi.
Kuhusu ishu ya Mwamnyeto, Bahanuzi alisema: “Ili Mwamnyeto akae sawa, anahitaji hekima ya viongozi wake na wachezaji wenzake kumsaidia asijisikie vibaya, yeye siye wa kwanza kukosea, tupo wengine ambao tuliwahi kupitia ari hiyo ukiachilia mbali kiongozi aliyekuwa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro alinisaidia pi kurejea katika ari ya kujiamini.”
Staa mwingine aliyewahi kuichezea Yanga na sasa yupo Al-Talaba SC, Simon Msuva aliwahi kukumbana na mazingira ya namna hiyo, lakini hata hivyo aliamua kuwajibu uwanjani kwa kufanya vizuri zaidi huku akiibuka mfungaji bora wa mabao 12 msimu wa 2016-2017 kabla ya kutimkia Morocco kuichezea Difaa El Jadida.