Prime
Okello ‘amchongea’ Pedro Goncalves, asema kinachomkwamisha
KIUNGO Allan Okello ameanza kumchongea kocha wake, Pedro Goncalves juu ya namna anavyotumika katika timu hiyo, akionyesha matumaini kwenye mechi aliyochezeshwa eneo tofauti analotumiwa kwa muda mrefu.
Ndani ya Yanga, Okello amecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara ambako ndiko amehusika kwenye mabao mawili akifunga moja na akihusika kutengeneza moja wakati Yanga ikitoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.
Okello amefunga bao moja tu akiwa na Yanga tena la penalti wakati Yanga ikishinda ugenini 3-0 dhidi ya Singida Black Stars.
Okello amecheza zaidi ya dakika 603, kwenye ligi lakini bado namba zake bora zimekuwa ngumu kuonekana haraka tofauti na matarajio makubwa wakati akisajiliwa akitokea Vipers ya Uganda.
HESABU ZILIKUWAJE
Wakati Yanga inamsajili Okello ilikuwa katika msako wa nani anaweza kupatikana akacheza namba 10 baada ya kufeli kwa kina Selestin Ecua, Mamadou Doumbia ambao walisajiliwa mwanzo wa msimu huu kuja kuziba nafasi ya fundi Stephanie Aziz KI, ambaye awali aliuzwa Wydad Athletic ya Morocco mwishoni mwa msimu uliopita.
THE CRANES, VIPERS ALITUMIKAJE
Mpaka anaondoka Vipers Okello alikuwa ameshafunga mabao matatu lakini akiwa na asisti tano ndani ya kikosi hicho, kiwango ambacho Yanga bado hakijaonekana.
Kinachomchelewesha Okello kufanya makubwa Yanga ni namna alivyokuwa anatumika akiwa na Vipers pia The Cranes na ni tofauti na anachokifanya akiwa hapa nchini na mabingwa hao wa soka Tanzania.
Kule Uganda Okello alikuwa akitumika kama namba 10 akicheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho ambapo ndio eneo ambalo anapenda kulitumikia kuliko lolote lingine.
YANGA VIPI
Akiwa Yanga Okello mechi nyingi amekuwa akitakiwa kushambulia akitokea pembeni akicheza kwa mtindo wa nusu eneo (half space) majukumu ambayo yanamtaka kuwa na mambo mawili makubwa kasi na nguvu.
Okello hawezi kumgomea Goncalves namna anachotakuwa akifanye na kocha wake badala yake atajilazimisha kucheza akitokea pembeni lakini ukweli ni matumizi hayo yatawafanya mashabiki wa Yanga kuchelewa kuona makali yake halisi.
OKELLO VS MTIBWA SUGAR
Akiwa kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, Goncalves alimpa jukumu la kucheza kama namba 10 Okello angalau hapo alianza kuonyesha kile ambacho angekionyesha muda mrefu kama kocha huyo angeshtuka haraka.
Kwenye mchezo huo Okello alihusika kwenye bao pekee la timu yake wakati ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na dakika ya 23 alipokea pasi kutoka kwa mwenzake Duke Abuya akakimbia kidogo tena akielekea lango la Mtibwa kisha akaachia shuti kali lililotemwa na kipa Constantine Malimi kisha kipa huyo kuutema na mpira kuwahiwa na mshambuliaji Emmanuel Mwanengo ambaye alimuwekea mfungaji wa bao Pacome Zouzoua na kuipatia timu hiyo bao.
Bao hilo ukitafuta nani alifanya kazi kubwa alikuwa Okello kutokana na maamuzi yake ya kujaribu akiwa mbali wakati ukuta wa Mtibwa ukiwa haujajiandaa sawasawa kama isingekuwa akili hiyo isingekuwa rahisi kwa timu yake kutenegeza nafasi hiyo nzuri.
Achana na tukio hilo, lingine lilikuwa dakika ya 71 na Mwanengo alipokea mpira akiwa amezungukwa na mabeki wa Mtibwa akachagua kupiga pasi nyuma yake baada ya kugeuka na mpira kumkuta Okello ambaye alipiga shuti lingine kali kipa akapangua lakini safari hii mabeki walikuwa imara na kuwahi kuokoa wakimuwahi Duke aliyekuwa anakimbia kwenda kuuweka wavuni.
Matukio haya mawili yalikosekana kwenye mechi nane zilizopita na Okello alionekana ni wa kawaida uwanjani akikosa kuonyesha makali ambayo alikuwa anayaonyesha huko nyuma kabla ya kuja Yanga.
MSIKIE KOCHA
Kocha wa zamani wa Okello Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye anamfuatilia kiungo wake huyo wa zamani amesema angalau kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa alianza kuona vitu ambavyo anavifahamu kutoka kwa kiungo huyo.
Robertinho amesema kama Pedro ataendelea kumtumia Okello kama kiungo namba kumi anaweza kuitengenezea Yanga mabao mengi lakini pia hata kufunga kwenye mechi za namna hiyo.
“Nimeona Okello akicheza kama namba 10 kwenye mchezo uliopita (dhidi ya Mtibwa), angalau nilianza kuona vile vitu bora ambavyo navijua kutoka kwake, kama ataendelea kutumika eneo hilo,” amesema Robertinho.