Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba Queens yaichapa Yanga Princess, yalinda rekodi yake

SIMBA Q Pict

Muktasari:

  • Simba Queens imeichapa Yanga Princess mabao 2-1 katika dabi ya ligi hiyo iliyochezwa jioni ya leo Mei 15, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

MABAO mawili ya mshambuliaji wa Simba Queens raia wa Kenya, Jentrix Shikangwa aliyofunga dhidi ya Yanga Princess, yameendelea kuiweka timu hiyo kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu huu huku ikiwa ndiyo timu pekee haijapoteza ikishinda 15 na sare moja.

Simba Queens imeichapa Yanga Princess mabao 2-1 katika dabi ya ligi hiyo iliyochezwa jioni ya leo Mei 15, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Simba Queens kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 16, huku ikipeleka presha kubwa kwa mabingwa watetezi, JKT Queens yenye mlima mrefu katika harakati za kutetea taji lao.

SIMBA 01

Simba Queens imeendelea kuonyesha ushindani mkubwa msimu huu baada ya kutopoteza mchezo wowote hadi sasa, jambo linaloifanya timu hiyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa iwapo itaendeleza mwenendo huo katika mechi sita zilizobaki.

Katika dabi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa, Simba Queens ilianza mchezo kwa kasi huku safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Shikangwa, Aisha Mnunka na Vivian Corazone ikiwapa wakati mgumu wapinzani wao.

Shikangwa aliandika bao la kwanza dakika ya 19 baada ya kutumia vyema nafasi iliyotengenezwa na Corazone, kabla ya kuongeza la pili dakika ya 37 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Yanga Princess ilirejea kipindi cha pili ikionyesha mabadiliko ya kiuchezaji huku benchi la ufundi likifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Aregash Kalsa dakika ya 45 na kumuingiza Diana Mnally. Dakika ya 49 Lydia Akoth naye aliingia kuchukua nafasi ya Asha Djafar katika jitihada za kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

Mabadiliko hayo yaliipa uhai Yanga Princess na dakika ya 57 ikapata bao kupitia kwa Ritticia Nabbosa aliyefunga baada ya kupiga faulo uliotokana na madhambi aliyofanyiwa Precious Christopher.

SIMBA 02

Licha ya Yanga kucheza vizuri kipindi cha pili na kupeleka presha langoni mwa Simba Queens, wekundu hao wa Msimbazi walisimama imara na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu zilizoendelea kuiweka kileleni.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga Princess kubaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 39 sawa na JKT Queens.

Kwa upande wa JKT Queens, mabingwa hao watetezi walijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Mashujaa Queens, matokeo yaliyozidi kuifanya Simba kujikita  kileleni kwa tofauti ya pointi saba.

Katika mchezo huo, Simba Queens ilianza na Ruth Aturo, Zanga Brice, Ruth Ingosi, Fasila Adhiambo, Zainah Nandede, Elizabeth John, Asha Omary, Elizabeth Wambui, Vivian Corazone, Aisha Mnunka na Jentrix Shikangwa.

Yanga Princess ilianza na Rita Akarekor, Igwe Uzoamaka, Jeaninne Mukandayisenga, Aregash Kalsa, Wincate Kaari, Ester Akudo, Precious Christopher, Agnes Pallangyo, Ester Mabanza, Asha Djafar na Ritticia Nabbosa.