Canada ilivyojinasua katika jinamizi la miaka 40
Muktasari:
- Kwa mataifa makubwa ya soka duniani, ushindi katika mechi za Kombe la Dunia ni jambo la kawaida lakini kwa Canada, ushindi huo umebeba uzito wa historia, maumivu na subira ya vizazi vya wachezaji na mashabiki.
VANCOUVER, CANADA: DAKIKA 90 dhidi ya Qatar zimeibadilisha historia ya soka la Canada, ushindi wa mabao 6-0 uliopatikana mbele ya maelfu ya mashabiki waliofurika Vancouver haukuwa tu ushindi wa kwanza katika Kombe la Dunia, ulikuwa mwisho wa safari ya miaka 40 ya kutafuta matokeo ambayo kwa muda mrefu yalionekana kama ndoto.
Kwa mataifa makubwa ya soka duniani, ushindi katika mechi za Kombe la Dunia ni jambo la kawaida lakini kwa Canada, ushindi huo umebeba uzito wa historia, maumivu na subira ya vizazi vya wachezaji na mashabiki.
Taifa hilo lilicheza kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico baada ya kufanya vizuri katika ukanda wa CONCACAF hata hivyo, ushiriki wao wa kwanza uligeuka kuwa somo gumu.
Walipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi dhidi ya Ufaransa, Hungary na Umoja wa Kisovieti, wakiondoka bila bao wala pointi. Kilichofuata ni ukame wa miaka 36.
Katika kipindi hicho Canada ilishindwa kufuzu fainali saba mfululizo za Kombe la Dunia huku majirani zao, Marekani na Mexico, wakizidi kujijengea heshima katika soka la kimataifa. Mara nyingi Canada ilionekana kuwa taifa la mchezo wa Ice Hockey kuliko soka.
Lakini nyuma ya pazia kulikuwa na mabadiliko makubwa. Mfumo wa kukuza vipaji ulianza kuzaa matunda huku kizazi kipya kikitokea katika ligi kubwa za Ulaya. Alphonso Davies, Jonathan David, Tajon Buchanan, Ismael Kone, Stephen Eustaquio na wengine wakaanza kuibadilisha sura ya timu ya taifa.
Mwaka 2022 walirejea katika Kombe la Dunia nchini Qatar. Ingawa waliondolewa mapema baada ya kupoteza mechi zote tatu, walionyesha kuwa walikuwa wanakaribia kuvunja ukuta uliokuwa mbele yao kwa miongo mingi.
Walifunga bao lao la kwanza kabisa katika historia ya Kombe la Dunia kupitia Alphonso Davies dhidi ya Croatia, lakini ushindi waliendelea kuusikia kwenye bomba kufuatia kutandikwa mabao 4-1.
Ndiyo maana mashindano ya mwaka 2026 yanaonekana kuwa maalum kwao. Wakiwa wenyeji pamoja na Marekani na Mexico, Canada iliingia katika michuano hiyo ikiwa na matarajio makubwa ya kuandika historia mbele ya mashabiki wao.
Mchezo wa kwanza dhidi ya Bosnia-Herzegovina uliisha kwa sare ya bao 1-1. Kwa mara ya kwanza katika historia yao walipata pointi katika Kombe la Dunia. Lakini hata baada ya matokeo hayo, bado kulikuwa na kazi moja kubwa iliyokuwa haijakamilika ambayo ni kupata ushindi wa kwanza.
Dhidi ya Qatar walifanya kila kitu kwa usahihi. Walitawala mchezo tangu dakika za mwanzo na kufunga mabao matatu kabla ya mapumziko. Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa na tukio baya la kiungo Ismael Kone kuvunjika mguu katika kipindi cha pili baada ya kuchezewa faulo mbaya.
Tukio hilo liliwaumiza wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki. Lakini badala ya kuvunjika moyo, Canada ilitumia maumivu hayo kama nguvu ya ziada. Waliongeza mabao mengine matatu na kukamilisha ushindi wa kihistoria wa 6-0.
Kwa mara ya kwanza tangu walipoingia katika ramani ya Kombe la Dunia mwaka 1986, Canada imeondoka uwanjani ikiwa mshindi.
NINI KINAFUATA?
Licha ya sherehe kubwa zilizotawala Vancouver, kazi ya Canada bado haijamalizika.
Ushindi huo umeiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya 32 bora lakini bado ina mchezo muhimu dhidi ya Uswisi ambao unaweza kuamua nafasi yao ya kumaliza kileleni mwa kundi.
Kumaliza kileleni kutakuwa na faida kubwa kwa sababu kutawapa nafasi nzuri zaidi katika hatua ya mtoano na kuongeza uwezekano wa kuendelea kucheza nchini Canada mbele ya mashabiki wao.
Iwapo watafuzu, Canada itaingia katika eneo ambalo halijawahi kufika katika historia yake ya Kombe la Dunia. Hilo pekee litakuwa rekodi mpya kwa taifa hilo. Lakini matarajio yameongezeka zaidi.
Kwa kiwango walichoonyesha dhidi ya Qatar, wengi wanaamini Canada inaweza kuwa moja ya timu za kushangaza katika mashindano haya. Kikosi hicho kina mchanganyiko wa vijana wenye kasi, uzoefu wa kucheza Ulaya na kocha Jesse Marsch ambaye amejenga utambulisho wa timu yenye kasi ya kushambulia na mshikamano katika kujilinda.
Changamoto kubwa sasa itakuwa namna ya kukabiliana na pengo lililoachwa na Kone ambaye hatarajiwi kuendelea na mashindano baada ya kuvunjika mguu.
Kone amekuwa mmoja wa viungo muhimu wa Canada katika miaka ya karibuni na kupoteza huduma yake kunaweza kuathiri mipango ya Marsch katika hatua zinazofuata.
Hata hivyo, tukio hilo limeonekana kuifanya timu kuwa karibu zaidi. Wachezaji wameonyesha mshikamano mkubwa na kuapa kupigania mafanikio zaidi kwa ajili ya mwenzao.
JE, WANAWEZA KUTOBOA?
Kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, lengo kuu la Canada lilikuwa kuvuka hatua ya makundi. Sasa baada ya kupata ushindi wa kwanza katika historia yao, matarajio yamebadilika.
Ikiwa itaendelea kucheza kwa kiwango kilichoonekana dhidi ya Qatar, Canada inaweza kufika hatua ya 16 bora na hata robo fainali, jambo ambalo lingekuwa mafanikio makubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la taifa hilo.
Kwa sasa jambo moja ni hakika baada ya miaka 40 ya kusubiri, Canada imevunja laana ya ushindi katika Kombe la Dunia na kama ushindi huo wa mabao 6-0 ni ishara ya kile kinachokuja, basi safari yao ya kihistoria inaweza kuwa ndio kwanza inaanza.